Facebook Comments Box

Sunday, August 11, 2013

SERIKALI YADHIBITI UAGIZAJI NA USAMBAZAJI WA TINDIKALI

Kutokana na kukithiri kwa matukio ya uhalifu kwa kutumia tindikali, Serikali imeamua kudhibiti uingizaji, usambazaji na uuzaji wa rejareja wa tindikali zinazotumika viwandani, katika maabara na vyombo vya usafiri.

Kwa kuanzia, wameanza kutoa leseni maalumu kwa watumiaji halali kwa kuwasajili katika ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali huku wakipeleka mrejesho wa mauzo katika ofisi hiyo kila mwezi.

Hayo yalisemwa jana na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manywele alipozungumza na waandishi wa habari akiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Elieza Feleshi.

Alisema kwa kuanzia, vibali vya kuagiza kemikali hizo lazima kuombwa upya ili kusimamia na kudhibiti huku takwimu za mauzo na jina la mnunuzi, tarehe aliyonunua, kiasi na ukali wa tindikali vikioneshwa.

Alisema taarifa hizo zitakuwa zikitumwa kwa Mkemia Mkuu kila mwezi kuanzia mwezi huu huku wauzaji wa rejareja wakipewa miezi mitatu kujisajili kwenye ofisi hizo: "Pia wauzaji wanatakiwa kuwa na kumbukumbu za mauzo na alizonunua, namba ya leseni, kiasi na
tarehe huku watumiaji katika vyombo vya usafiri wakitakiwa watoe malipo ya huduma kwani hawatatakiwa kununua na kuondoka na tindikali," alisema Manywele.

Aliongeza kuwa huduma hizo zitatolewa kwa wauzaji wa rejareja waliosajiliwa ambapo tindikali zitakuwa katika ujazo wa lita tano na kuendelea na kuanzia sasa hairuhusiwi kuuzwa chini ya ujazo huo.

Mkemia huyo alisisitiza kuwa wanajiandaa kuongeza uelewa kwa wauzaji wa tindikali nchini  huku wakitarajia kuanzisha kituo maalumu cha kuratibu matumizi ya sumu.

"Katika kituo hicho tutahakikisha taarifa zinapelekwa kwa Mkemia haraka na kufanyiwa uchunguzi haraka ili kuhakikisha tunakabiliana na majanga haya ya matumizi mabaya ya tindikali," alisema.

Mwema alisema katika kudhibiti tindikali kutumika kama silaha, itatumika sheria  iliyopo kudhibiti aina hiyo mpya ya uhalifu na kutaka wananchi kusaidia kutoa taarifa mapema ili kupata ushahidi.

Alisema kwa kutumia mikakati iliyopo ya ofisi ya Mkemia Mkuu, aliagiza makamanda wote mikoani kufuatilia waagizaji, wasambazaji, wauzaji wa rejareja na watumiaji kwa kushirikiana na jamii ili kutokomeza uhalifu huo.

Feleshi alisema changamoto iliyopo katika kukabiliana na uhalifu huo mpya ni pamoja na usimamiaji kesi kwa kufuata sheria inayoagiza ushahidi, lakini unakosekana.

Aliomba wananchi kushirikiana na kuacha matumizi ya tindikali kutumika kama ugaidi, kwani kwa sheria ya ugaidi ya mwaka 2002 inategemea jinsi uhalifu wa kigaidi unavyotendeka.

Hivyo aliomba wanajamii kutoa taarifa, kwani si hiari na ikibainika mtu alijua sehemu ya uhalifu na lakini akaficha naye atakuwa sehemu ya uhalifu huo.

Feleshi alisema kwa mujibu wa sheria, wahalifu wa makosa hayo ya tindikali wakibainika iwapo mwathirika ameumizwa kiasi cha kupata ulemavu atahukumiwa kifungo cha maisha jela, na kama mwathirika atakuwa ameumia kidogo basi kifungo kitakuwa ni miaka saba jela. (Taarifa via gazeti la HABARI LEO)


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU