Facebook Comments Box

Friday, June 7, 2013

KIEMBA: MIMI NI MCHEZAJI HURU NA BADO SIJASAINI YANGA

KWA mara ya kwanza, kiungo Amri Ramadhani Kiemba ameibuka na kukanusha kusaini Yanga SC, ingawa amesema yeye bado mchezaji huru, kwa kuwa hadi sasa hajasaini timu yoyote baada ya kumaliza Mkataba wake Simba SC. Akizungumza  Kiemba alisema kwamba hajasaini timu yoyote hadi sasa na anajitambua kama mchezaji huru. Alipoulizwa kuhusu mustakabali wake, Kiemba alisema kwa sasa akili yake ipo kwenye kuisaidia timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars iweze kukata tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia. “Sasa hivi ukiniuliza mambo ya klabu, utakuwa unanionea tu. Nipo katika kambi ya timu ya taifa, fikra zangu ni majukumu yangu ya kitaifa. Nadhani baada ya hapa, nitazungumzia hayo mambo,”alisema Kiemba. Kiemba aliibua wasiwasi mkubwa kwa wapenzi wa Simba SC, baada ya kuvuma kwa habari amesaini Yanga SC, huku Mkataba wake ukiwa umemalizika Msimbazi. Na anaonekana mtu asiye na wasiwasi kabisa kuhusu mustakabali wake- pengine inatokana na kiwango chake cha juu hivi sasa. Stars inashika nafasi ya pili katika Kundi C, kuwania tiketi ya Kombe la Dunia mwakani Brazil, ikiwa na pointi sita nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba, ambayo kesho itakuwa ugenini ikimenyana na Gambia katika mchezo mwingine wa kundi hilo. Stars ilitua hapa Jumatatu ikitokea Ethiopia ambako iliweka kambi ya wiki moja na kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Sudan, ulioisha kwa sare ya bila mabao. Kabla ya kuja hapa, Stars iliweka kambi ya wiki moja katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ikijifua Uwanja wa Karume na siku chache kabla ya kuondoka ilialikwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete, aliyewapa hamasa kwa hotuba nzuri.

SOURSE: BIN ZUBEIRY


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU