Facebook Comments Box

Friday, November 1, 2013

MRAGE KABANGE AWASHANGAA SIMBA

KOCHA Msaidizi wa Kagera Sugar, Mrage Kabange amewashangaa mashabiki wa Simba kufanya fujo jana baada ya refa kuongeza dakika nne kipindi cha pili katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya timu hizo, ambazo timu yake ilizitumia kupata bao la kusawazisha na kutoa sare ya 1-1 ugenini. Akizungumza n BIN ZUBEIRY leo, Kabange aliyewahi kuchezea Simba SC miaka ya 1980, alisema kwamba katika kipindi cha kwanza refa Mohamed Theofile wa Morogoro aliyesaidiwa na Said Mnonga na Charles Chambea wote wa Mtwara, aliongeza dakika tano ambazo Simba SC walizitumia kupata bao la kuongoza.
Mrage Kabange amewaona Simba SC wa ajabu sana
Mrage Kabange kocha msaidizi wa kagera sugar


“Simba walipata bao lao baada ya dakika 45 za kipindi cha kwana, lakini hawakuona, ila sisi kipindi cha pili tulipopata bao la kusawazisha ndani ya dakika nne za nyongeza, wameleta fujo, huo siyo uungwana,”alisema.
Kabange alisema anawaheshimu Simba SC ni timu kubwa, lakini anaomba wawe tayari kukabiliana na changamoto za Ligi Kuu na wajue pia mpira ni dakika 90.
“Wao walitakiwa kulinda bao lao hadi filimbi ya mwisho, ni kweli tulipata nafasi nyingi tukashindwa kuzitumia kwa muda mrefu wa mchezo, lakini hatimaye dakika za  mwishoni tukafanikiwa kupata sare ya ugenini ambayo sio mbaya,”alisema.
Baada ya Kagera kusawazisha dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimia kwa dakika 90, Uwanja wa Taifa, uligeuka eneo la vita baina ya Polisi mashabiki wa Simba SC.
Baada ya Salum Kanoni kukwamisha nyavuni mkwaju wake wa penalti, mashabiki wa Simba waliokuwa viti vya Rangi ya Bluu na Chungwa, walianza kung’oa viti na kuvitupia uwanjani.
Mara moja, Polisi walianza kupambana na mashabiki hao kwa kuwatupia mabomu ya machozi, ndipo wakaanza kukimbia. Makocha na wachezaji wa Simba kwa pamoja waliwafuata waamuzi kuwalalamikia- hali ambayo ilifanya watolewe kwa kusindikizwa na Polisi.
Bao la Simba lilifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amisi Tambwe dakika ya 45 baada ya kupokea pasi nzuri ya Betram Mombeki na kumpiga chenga beki Salum Kanoni, kabla ya kumchambua kipa Hannington Kalyesebula.
Kagera ilipata pigo mapema dakika ya 22 kipa wake Agathon Anthony kuumia katika harakati za kuzuia shambulizi la Tambwe na nafasi yake ikachukuliwa na Mganda, Kalyesebula.  
Kwa ujumla timu zote zilishambuliana kwa zamu kipindi cha kwanza, ingawa Simba SC ndiyo waliotengeneza nafasi nyingi zaidi za kufunga.
Kipindi cha pili, Simba SC iliendelea kusukuma mashambulizi mengi langoni mwa Kagera, lakini washambuliaji wake walikosa umakini wa kutumia nafasi.
Kagera nayo iliendelea kushambulia na kwa ujumla mchezo ulizidi kunoga kadiri muda ulivyokuwa ukisonga mbele kutokana na ushindani mkali.
Wakati refa wa akiba, Hussein Kalindo wa Kinondoni, amekwishaonyesha dakika nne za nyongeza, Kagera ikafanya shambulizi langoni mwa Simba na Daudi Jummane akaangushwa kwenye eneo la hatari na beki wa Simba SC, Joseph Owino na refa akaamuru penalti.
Beki wa zamani nwa Simba SC, Salum Kanoni akaenda kumchambua vizuri kipa Abuu Hashimu kuisawazishia Kagera dakika ya 90+2.
CHANZO: BIN ZUBEIRY


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU