Mwasisi wa Chadema Edwin Mtei (mwenye kofia) akizungumza kwenye mkutano wa siku tatu wa Baraza la Kanda ya Kaskazini ya chama hicho jijini Arusha juzi |
Mkutano
wa Baraza la Uongozi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Kanda ya Kaskazini juzi uligeuka ukumbi wa ngumi, baada ya Mwenyekiti wa
chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kushushiwa kipigo.
Mwigamba
alishushiwa kipigo hicho na baadhi ya viongozi wenzake wa chama kwa
madai ya usaliti na tayari amesimamishwa uongozi kwa muda usiojulikana.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas jana alithibitisha kutokea kwa
vurugu hizo na viongozi hao wa Chadema kufikishana polisi.
Alikutwa
na zahama hiyo mbele ya viongozi wakuu wa Chadema Taifa, Mwenyekiti,
Freeman Mbowe na mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei katika Hoteli ya
Coridal Spring.
Viongozi
hao wamekuwa wakifanya ziara za aina hiyo nchi nzima, kuimarisha chama
na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na
uchaguzi mkuu ujao wa Rais na wabunge mwaka 2015.
Habari
kutoka ndani ya mkutano huo zinaeleza kuwa hatua hiyo ilifuatia tuhuma
kwamba Mwigamba alituma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii
Forums, unaodaiwa kukichafua chama hicho.
Tukio
hilo la aina yake lilitokea wakati viongozi wote wa juu wa chama hicho,
wakiongozwa na Mbowe walipokuwa wakijadili mustakabali wa chama hicho,
mkutano ambao ulihudhuriwa na wabunge karibu wote wa Chadema wa kanda
hiyo.
Hata
hivyo, wakati mijadala ikiendelea baadhi ya viongozi wa chama hicho,
akiwamo Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema walimtuhumu
Mwigamba kutuma ujumbe kwenye mtandao huo, uliokuwa ukizungumzia ufisadi
ndani ya chama hicho, wakidai alitaka Mwenyekiti Mbowe kukubali
kuchunguzwa.
Akizungumza
na Mwananchi Jumapili jana, Mwigamba alisema kuwa baada ya Lema kutoa
tuhuma hizo aliungwa mkono na viongozi wengine na vijana waliokuwa
wameimarisha ulinzi, kumvamia na kuanza kumpiga pamoja na kumnyang'anya
kwa nguvu kompyuta mpakato (Laptop), aliyokuwa nayo, kisha kumpeleka
Kituo Kikuu cha Polisi, mjini Arusha.
"Wamenipiga
sana na kuniweka ndani, ila nashukuru Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya
Arusha (OCCID), alikuja na kunitoa saa 5:00 asubuhi," alisema Mwigamba.
Alisema
kuwa leo katika mkutano wake na waandishi wa habari ataeleza yote
yaliyotokea na hatua atakazochukua, kwa kuwa yeye ni kiongozi wa juu wa
chama.
Hata hivyo, alieleza kwamba bado anashauriana na wanasheria wake kuona kama anaweza kuwachukulia hatua waliompinga.
Kauli ya polisi
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema polisi wameona hakuna
kosa la kisheria lililotokea hasa kutokana na malalamiko yaliyofikishwa
kwao dhidi ya Mwigamba ya kukichafua chama kwenye mitandao.
"Hili
suala la mitandao ni kubwa na lina taratibu zake sasa kusema tu
umechafuliwa na iwe kesi nadhani uchunguzi unahitajika kwao, sisi
tumeona haya ni mambo yao wanaweza kuyamaliza wao ndiyo sababu
tulimwachia, Mwigamba," alisema Sabas.
Kosa analodaiwa kufanya Mwigamba
Akizungumzia
sakata hilo jana, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema kwamba
Mwigamba alibainika kutuma ujumbe kwenye mtandao wa Jamii Forums
uliokichafua chama hicho, akieleza haikuwa mara yake ya kwanza kwa
kiongozi huyo kufanya hivyo na kwamba walikuwa wakimfuatilia kwa muda
mrefu.
"Kilichotokea
ni hicho, vijana wa Red Brigade ndio waliomtoa ukumbini, baada ya
kumbaini kukichafua chama, kwani laptop yake baada ya kuchunguzwa na
wataalamu wetu walijiridhisha ni yeye ndiye aliyetuma ujumbe huo,"
alisema Lema.
Katibu wa
Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alitaja tuhuma zinazomkabili
Mwigamba kuwa ni pamoja na kusema uongo, kupotosha taarifa za chama na
kuchonganisha viongozi kupitia mtandao wa kijamii ya Jamii Forums.
Katika
andiko lake kwenye mtandao, Mwigamba anadaiwa kuwatuhumu viongozi wa juu
wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu,
Dk Wilbrod Slaa kuwa wamechakachua katiba ya chama hicho kuhusu ukomo wa
nafasi za uongozi ili kujinufaisha binafsi.
Golugwa
alisema kuwa baada ya kubanwa kwenye kikao, Mwigamba alikiri kuandika na
kurusha taarifa hizo kwenye mitandao, lakini alipotakiwa kukabidhi
kompyuta yake ili ichunguzwe na wataalamu wa mawasiliano wa chama hicho
aligoma, hali iliyozua tafrani kati yake na walinzi wa chama hicho (Red
Brigade), waliolazimika kutumia nguvu kumdhibiti.
Purukushani zilivyotokea
Habari
zaidi zinaeleza kuwa katika harakati za kutaka kumnyang'anya Mwigamba
kompyuta yake, mwenyekiti huyo wa Chadema mkoani Arusha alianza
kushambuliwa na baadhi ya viongozi wa Chadema, kabla ya kufanikiwa
kumdhibiti.
Zinaeleza
kuwa katika tukio hilo kulitokea pia kurushiana maneno na matusi ya
nguoni kati yake na viongozi wengine wa chama hicho akiwamo Lema.
Baadaye Lema aliliambia gazeti hili kwamba katika purukushani hizo Mwigamba alimrushia ngumi ambayo hata hivyo aliikwepa.
Alisema kuwa wanakusudia kumfungulia kesi Mwigamba ya kukichafua chama chao katika mitandao ya kijamii.
Hata
hivyo, alisema kikao chao kiliendelea jana bila ya vurugu zozote na
kuweka mikakati ya kushinda majimbo yote ya Kanda ya Kaskazini mwaka
2015 na kuchukua nchi katika uchaguzi huo ujao.
Adhabu kwa Mwigamba
Katika
hatua nyingine Chadema, kimemsimamisha uongozi Mwigamba kwa tuhuma za
kukisaliti, kukihujumu chama hicho na viongozi wake.
Akitangaza
uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari jijini Arusha jana, Mwenyekiti
wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Israel Natse alibainisha kuwa uamuzi wa
kumsimamisha Mwigamba katika nyadhifa zote za uongozi ndani ya chama
ulifikiwa na kikao cha Baraza la Uongozi wa Kanda ya Kaskazini
kilichokutana juzi.
Alisema
kuwa Mwigamba amesimamishwa kwa muda usiojulikana kupisha uchunguzi wa
tuhuma dhidi yake na kuonya kuwa iwapo tuhuma zitathibitishwa, hatua
nyingine za kinidhamu zitafuata kulingana na kanuni na katiba ya
Chadema.
"Kwa sasa
Mwigamba anatuhumiwa kuvunja sura ya kumi, kifungu cha 10.1 kifungu
kidogo cha 8, 9 na 10 ya katiba ya Chadema inayozungumzia maadili ya
uongozi," alisema Natse.
Akifafanua
zaidi alisema kuwa sura na vifungu hivyo vinakataza kiongozi wa chama
hicho kutoa tuhuma dhidi ya viongozi wenzake bila kufuata vikao halali
vya kikanuni na kikatiba.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog