Facebook Comments Box

Thursday, September 5, 2013

WAZEE YANGA WAMKATAA KATIBU NA MHASIBU MHINDI

akilimalii_6c882.jpg
WAZEE wa Yanga waliokasirika na 'kuipiga laana' timu baada ya kutofautiana na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu wakati huo, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga ikapigwa 5-0 na Simba SC mwaka juzi, wameingia katika mgogoro mwingine na uongozi wa sasa chini ya Mwenyekiti, Alhaj Yussuf Mehboob Manji.
 
Wazee hao chini ya kinara wao, Ibrahim Ally Akilimali wanaingia katika mtafaruku na uongozi wa Manji, kiasi cha mwezi mmoja na ushei kabla ya mchezo mwingine dhidi ya watani wa jadi, Simba SC Oktoba 20, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Hatumtaki huyo Mkenya; Kutoka kulia Mzee Bilal Chakupewa, Ibrahim Akilimali na Hashim Muhika. Wazee hao wamesema hawatambui ajira ya Mkenya.
 
Katika Mkutano wao na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, Wazee hao wanapinga mambo mawili yaliyofanywa na uongozi wa Manji; kuleta Mhasibu mwenye asili ya Kiasia na kuajiri Katibu mpya kutoka Kenya.
 
Katibu Mkuu mpya wa Yanga SC, Patrick Naggi yupo tayari nchini kuanza kazi akirithi mikoba ya Lawrence Mwalusako aliyemaliza Mkataba wake.
 
Akizungumza na Waandishi wa jhabari klabu leo, Mwenyekiti wa Wazee hao, Ibrahim Akilimali amesema kiongozi yeyote ambaye anapaswa kuiongoza Yanga, lazima awe mwanachama wa klabu hiyo, hivyo walivyofanya uongozi ni kinyume kabisa na Katiba inavyotaka.
 
"Mpaka sasa sisi hatumtambui, kwani hatuna vielelezo vyake vya kuwa mwanachama wa klabu hii, endapo atatuletea vielelezo hivyo sisi tutamtambua na kumpa ushirikiano.
"Kazi za Wanayanga zitafanywa na wanachama wetu pekee na si wa nje ya klabu yetu, hatutakubali hata chembe kuona katiba yetu ikikanyagwa na viongozi wetu, tutasimama kidete mpaka mwisho kuona jambo hili halifanikiwi," alisema Akilimali
 
Alisema wao wakiwa kama wanachama wa Yanga hawatambui ajira ya raia huyo wa Kenya na anatakiwa kuondoka ndani ya saa 24 klabuni hapo.
Akilimali alisema hawataki kumwona katika klabu hiyo, kwani Yanga ina wasomi wengi ambao wanaweza kuifanya kazi hiyo.
 
Alimfananisha Mkenya huyo ni mtu aliyeingia kwa njia za panya katika klabu hiyo, kwa kuwa hawana mwanachama wa aina yake kwenye leja ya wanachama wa Yanga.
Alisema wamekuwa na kawaida ya kupewa taarifa na Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Manji kama kunakuwa na jambo lolote ambalo wamepanga kulifanya kwa maslahi ya Yanga, lakini hawakuambiwa kuhusu ajira ya Mkenya huyo.
 
"Huyu mtu tunamwona ni 'kanjanja' aondoke haraka sana, sisi wana Yanga hatumuitaji kabisa," alisema Akilimali.
 
Wakati huo huo, mwanachama wa klabu hiyo, Said Motisha alisema Yanga itagawanyika kwa hilo, kwani hawatakubali wazawa kunyimwa ajira wakati wanasifa ya kufanya kazi.


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU