Hatimaye
Barack Obama, Rais wa Marekani anatembelea tena bara la Afrika. Hii
itakuwa ni mara ya pili Obama kutembelea Bara hili alikotoka baba yake
baada ya ziara yake ya kwanza mwaka 2009. Mwaka huo alitembelea Ghana na
Misri ilhali mwaka huu anatembelea Senegali, Afrika Kusini na Tanzania.
Ziara hiyo itakayoanza tarehe 26 mwezi Juni, itamfikisha Tanzania
tarehe 1 Julai na kuondoka siku ya pili yake.
Uchaguzi wa Obama
kuwa Rais wa Marekani ulipokolewa kwa shangwe Afrika nzima. Wakati
Waziri wa mambo ya nje wa Nigeria alilia kwa furaha, nchi ya Kenya
ilitangaza siku ya mapumziko na Rais wa zamani wa Afrika Kusini ndugu
Nelson ‘Madiba’ Mandela alisema ‘ushindi wa Obama unawafanya Waafrika
wathubutu kuota ndoto (Jarida la The Economist). Hapa Tanzania kulikuwa
kuna shamra shamra za kila namna na magazeti yaliweka vichwa vya habari
kana kwamba ni Rais wa Tanzania aliyechaguliwa.
Waafrika walikuwa na matumaini makubwa sana na bwana Obama. Yamefikiwa?
Ni vema ifahamike kuwa Barack Obama ni Rais wa Marekani na siku zote
atalinda maslahi ya Marekani tu. Kuwa na matumaini makubwa kwamba labda
yeye angeliweza kuiweka Afrika mbele sana ilikuwa ni kujifurahisha tu
nafsi. Maslahi ya Marekani ni ya kipaumbele kuliko kitu kingine chochote
kwa Rais Obama. Kwa wengi Obama amekuwa kama amewavunja moyo.
Tanzania inapokea kiongozi wa Taifa kubwa duniani wa pili sasa ndani ya
kipindi cha miezi 3 tu. Kwanza alikuja Rais wa China na sasa wiki hii
anakuja Rais wa Marekani. Maneno ya mtaani na kwenye mabaraza ya
majadiliano ni kwamba viongozi hawa wanakuja kugombea maliasili tulizo
nazo kama gesi asilia na madini. Nadhani haya ni maneno ya kusema katika
kupiga soga maana kunyonywa kwa rasilimali hakuhitaji Rais wa Marekani
aje Tanzania. Makampuni yote makubwa yanayochimba dhahabu hapa nchini ni
makampuni ya nje na marais wao hawakuja ili waweze kupata mikataba
minono ya kuvuna utajiri wetu. Katika kitalu namba 2 cha utafutaji wa
mafuta na gesi huko Bahari Kuu kampuni ya kimarekani ya ExxonMobil ina
ubia na kampuni ya Norway ya StatOil. Kampuni hiyo haikusubiri Rais wa
Marekani aje ili wapate mikataba.
Kuna makampuni mengi sana ya
kichina yanajenga barabara zetu hapa nchini yakiwa na mikataba minono
sana. Kule Mchuchuma na Liganga kuna kampuni ya kichina inajiandaa na
uchimbaji wa chuma na makaa ya mawe. Makampuni yote haya hayakusubiri
Rais wao aje.
Hoja inayojengwa hapa ni kwamba ujio wa Marais
mbalimbali nchini ni ujio wa kujijenga kidiplomasia na wakati mwingine
kama sehemu ya kutuma ujumbe Fulani kwa dunia. Nchi inayotembelewa pia
inaweza kuona kuwa diplomasia yake inaheshimiwa na mataifa
yanayoitembelea.
Hata hivyo hii haiondoi ukweli kwamba Obama
anakuja kwa ajili ya maslahi ya nchi yake kama ilivyo kwa wachina
walivyokuja. Tumesikia Rais Obama ataambatana na mamia ya wafanyabishara
kutoka Marekani kwa ajili ya kupata fursa za kuwekeza nchini. Pia
tutasikia matangazo kuhusu msaada wa pili wa Millenium Challenge ambapo
Wamarekani wanaendelea kumwaga pesa nchini kusaidia miundombinu lakini
pia kushawishi kuungwa mkono na nchi zetu kwenye maamuzi Fulani Fulani
jumuiya za kimataifa.
Tumesikia Obama atakwenda kutembelea
mitambo ya kampuni ya Symbion. Hii ni mitambo ambayo miaka 4 iliyopita
ilipigiwa kelele kuwa ni mitumba na hivyo TANESCO wasiinunue.
Hawakununua na badala yake kampuni hiyo ya kimarekani ikainunua,
wakaingia mkataba na TANESCO kuwauzia umeme unaozalishwa na mitambo
hiyo hiyo chakavu. Wakati tunasuburi kulipa takribani tshs 105 bilioni
kwa Dowans baada ya kutubwaga kwenye kesi, tunasubiri kuona wanasiasa
watakaokwenda kumsindikiza Obama kwenye matembezi hayo ya kutembelea
mitambo chakavu.
Kampuni kubwa ya kutengeneza mitambo ya
kuzalisha umeme ya GE imetangaza kuingia ubia na kampuni ya Symbion
kuzalisha umeme nchini. Takribani 400MW zitazalishwa kutoka Mtwara na
kuingizwa kwenye gridi ya Taifa. Pia sehemu kubwa ya umeme
utakaozalishwa Mtwara tayari umepata soko kwenye kiwanda cha kuzalisha
udongo ulaya (simenti) cha bwana Dangote kule Mtwara. Mtendaji Mkuu wa
GE bwana Jeff Immelt ametangaza kuwa kampuni yake itauza mitambo ya
kuzalisha umeme kwa kutumia gesi mingi zaidi Afrika Mashariki kuliko
Marekani katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Ni biashara tu!
Nishati naona ni kipaumbele kikubwa sana kwa ziara ya Rais Obama. Kwa
nchi kama yetu yenye watu asilimia 21 tu wenye umeme, ni dhahiri
kipaumbele hiki watu wengi watakiiunga mkono. Hata hivyo Obama ni lazima
asimame kidete kuhakikisha kuwa kampuni za nchini mwake zinazopata
miakataba hapa nchini ziweke wazi mikataba hiyo na kulipa kodi
inavyostahili. Makampuni ya mafuta kutoka Marekani hayana historia nzuri
duniani na hivyo ni lazima tulisisitize mapema kabisa. Uwazi wa
mikataba na uwezo wa kupambana na ukwepaji kodi ni muhimu sana katika
vita dhidi ya Ufisadi na ubadhirifu.
Rais Obama atambue kuwa
iwapo Tanzania ingekuwa inakusanya nusu ya kodi zinazokwepwa na
makampuni makubwa yanayotumia mbinu kali, basi tungehitaji misaada ya
Marekani na hapa nchini angekuja kama mbia wa kweli na sawa katika
dunia. Hivyo ni vema aungane na Waziri Mkuu wa Uingereza kuhakikisha
kuwa makampuni makubwa hayatumii ‘tax havens’ kukwepa kodi katika nchi
kama Tanzania. Uwazi wa mapato yao na kilicholipwa kwa Serikali ni vema
usisitizwe sana na Obama mwenyewe ili makampuni yao yasikie na yaache
kupora utajiri wa Afrika kiujanja ujanja.
Mwisho ni vema kama
Rais Obama ataomba radhi kwa ushiriki wa Marekani kwenye mauaji wa
Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo Patrice Lumumba. Hivi Tanzania
inahangaika zaidi ya uwezo wake kupeleka majeshi huko mashariki ya Kongo
kulinda amani. Waafrika wengi tunaamini kuwa mauaji ya Lumumba ilikuwa
ni kama laana kwa Taifa lile na hivyo limekuwa ni taifa la vurugu na
vita licha ya utajiri mkubwa ulioko nchini humo. Nyaraka za CIA
zinaonyesha dhahiri kuwa Rais wa Marekani wa wakati huo Lyndon Johnson
aliagiza kuuwawa kwa mwanamapinduzi Patrice Lumumba. Kuwaomba radhi
Waafrika na hasa Wakongo kuhusu mauaji ya Lumumba ni jambo litakaloweza
kusaidia sana kurejesha amani Kongo.
Karibu Afrika, Karibu Tanzania ndugu Barack Hussein Obama.
Zitto Z Kabwe
Makala haya yanatarajiwa kutoka kwenye gazeti la MWANANCHI, mfululizo wa makala kuhusu ziara ya Obama.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog