Facebook Comments Box

Saturday, March 2, 2013

SIMBA WAPOKELEWA VIZURI NA LIBOLO

Kipa wa Simba, Abel Dhaira na mlinzi, Said Nassor Chollo mara baada ya kuwasili Uwanja wa Calulo ambao uko kilomita 300 kutoka Luanda. Ndege inayoonekana pichani ni ya tajiri wa Libolo, Lui Compos ambayo Simba ilitumia kutoka mji mkuu wa Angola, Luanda. Picha na Edo Kumwembe, Angola
SIMBA imetua salama mjini Calulo nje kidogo ya jiji la Luanda, Angola, lakini vifaa vyake muhimu vya kufanyiamazoezi vimepotea katika mazingira ya kutatanisha.
Hata hivyo, Simba wamefikia katika hoteli ya tajiri wa Libolo huku wakipandishwa katika ndege mbili ambazo pia zinamilikiwa na kipoba huyo.

Wekundu hao wa Msimbazi wanacheza na Recreativo Libolo ya hapa kesho Jumapili katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Simba ilifungwa bao 1-0 kwenye mchezo wa awali jijini Dar es Salaam.

Simba ilitua Luanda jana Ijumaa saa 5.30 asubuhi za Tanzania na kupakiwa kwenye ndege mbili kwenda mjini Calulo ambako ni umbali wa dakika 30 kutoka Luanda. Ndege ilizopanda Simba zinamilikiwa na tajiri wa Libolo, Rui Campos.

Baada ya kutua Simba walipokewa vizuri na wenyeji wao lakini walilazimika kuhaha kwa dakika kadhaa kutafuta vifaa vyao ambavyo ni bips (vizibao vinavyovaliwa juu ya jezi za mazoezi), koni na mipira ambayo wahumudu wa ndege ya Kenya Airways hawakuwa na jibu zaidi ya kuahidi kuvitafuta zaidi na huenda leo Jumamosi Simba wakavipata.

Mbali na vifaa hivyo hata begi la beki Amir Maftah halikupatikana. Simba iliwasili Calulo saa sita mchana na kufikia hoteli ya Ritz inayomilikiwa na wapinzani wao ambao waliwaazima vifaa kwa ajili ya mazoezi na hali ya hewa na hapa ni joto kali sawa na Dar es es Salaam.

Kiraka Haruna Moshi hayupo na Simba Angola baada ya kupimwa jijini Dar es Salaam na kubainika kwa ana malaria 19 huku kocha wa viungo Moses Basena akibaki kumuuguza mkewe.

Kwenye Uwanja wa ndege wa Calulo, Simba ilipokelewa na wanajeshi na kusindikiwa hadi hotelini ambapo mazingira ya mjini hapa hayajaendelea sana kama ilivyo Luanda na hata uwanja itakapochezwa mechi wa Manispaa ya Calulo Estadio Municipal de Calulo unabeba mashabiki 10,000 tu.

Kocha wa Simba, Patrick Lieweg alisema kikosi chake kipo katika hali nzuri na wako safi kisaikolojia tayari kwa ushindi na kusonga mbele kwenye mashindano hayo.
Nitalazimika kumuanzisha Seseme kwavile Haruna Moshi hayupo lakini kimsingi timu imekuja hapa kushinda na nimewasisitiza wachezaji hilo na wakanielewa, tutapambana mpaka dakika ya mwisho,alisema Mfaransa huyo mwenye miaka 60 ambaye hii itakuwa mechi yake ya 54 kuiongoza klabu kwenye michuano ya kimataifa ya CAF.


SOURCE: MWANASPOTI

Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU