Facebook Comments Box

Saturday, March 23, 2013

SERIKALI HAINA MPANGO WA KUBINAFSISHA TANESCO

Serikali imesema haina mpango wa kuuza au kubinafsisha Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa sababu za kiusalama, licha ya shirika hilo kushindwa kutimiza baadhi ya majukumu yake.

Mbali na TANESCO, mashirika mengine ambayo pamoja na kufanya vibaya yataendelea kubaki mikononi mwa serikali ni Mamlaka ya Bandari, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na mengine ambayo kiutendaji yanahusishwa na usalama wa Taifa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, muda mfupi baada ya kuzungumza na wafanyabiashara kutoka Uingereza.

Wafanyabiashara hao wamekuja nchini baada ya Waziri huyo kutembelea Uingereza na kuwaeleza kuwa Tanzania imefungua milango ya uwekezaji. Wameonyesha nia ya kuwekeza kwenye nishati hasa ya gesi.

Profesa Muhongo alisema kinachoendelea sasa ni kuliboresha shirika kwa kufanya marekebisho makubwa. “Watanzania subirini kidogo, mambo mazuri ya TANESCO yanakuja muda si mrefu,” alisema.

Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, madhara ya kuachia mashirika nyeti mikononi mwa wawekezaji ni makubwa kuliko faida, huku akitoa mfano kwa Bandari kuwa inaweza kuingiza meli iliyosheheni silaha za kupindua nchi huku usalama wa Taifa ukiwa hauna taarifa zozote.

“Lazima mashirika nyeti yaendelee kuwepo mikononi mwa serikali ili kujihakikishia usalama,” alisema. Aliongeza kuwa TANESCO itaendelea kununua umeme kutoka kwa wawekezaji kwani haiwezi kuwa wafuaji umeme na wasambazaji.

Alisema TANESCO imekuwa ikinyooshewa vidole kila wakati kwa kuwa inagusa maisha ya watu, huku akisisitiza kuwa mashirika karibu yote yanafanya vibaya lakini hayanyooshewi vidole kama shirika hilo, “mbona watoto wamefeli vibaya...”

Hata hivyo, Profesa Muhongo alisema uchumi wa nchi hauwezi kuimarishwa na serikali pekee, bali kwa kushirikiana na sekta binafsi. Kuhusu wawekezaji wa nje kuja kuwekeza nchini, alisema hawawezi kuachiwa wenyewe ni lazima waingie ubia na kampuni za ndani.

Kuhusu kuwepo wanataaluma waliobobea katika masuala la gesi,  Waziri Muhongo aliwaondoa wasiwasi kwa kuwaeleza kuwa baada ya muda si mrefu wataalamu wa fani hizo watakuwa zaidi ya 200.

Aliwaambia kuwa vipo vyuo vikuu kama cha Dodoma vimeshaanzisha masomo ya masuala ya gesi lakini pia wapo wanafunzi wanaosoma nje ya nchi na kwamba muda si mrefu.

via gazeti la Nipashe



Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU