Facebook Comments Box

Monday, March 18, 2013

RAGE APINDULIWA SIMBA

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage. 
 


Mkutano mkuu wa dharura wa wanachama wa Klabu ya Simba umemwondoa madarakani mwenyekiti wao Ismail Rage na kuivunja Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kwa madai ya kukiuka katiba ya klabu yao.
Awali uongozi wa Simba ulipiga marufuku mkutano huo usifanyike kwa sababu haukuwa halali, lakini jana wanachama wa Simba walifanya mkutano huo kwenye Hoteli ya Starlight jijini Dar es Salaam na  kuhudhuriwa na wanachama zaidi ya 600.
Hata hivyo, kwa mujibu wa katiba ya Simba, ni mwenyekiti aliye madarakani kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji ndiye mwenye mamlaka ya kupanga ajenda, mahali na wakati wa kufanyika kwa mkutano mkuu.
Mbali ya kumtimua Rage, mkutano huo pia ulimpendekeza aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Simba, Rahma Al Kharoos kuongoza Kamati Maalumu ya kuiongoza Simba hadi pale uchaguzi mkuu wa klabu hiyo utakapofanyika.
Mkutano huo uliokuwa chini ya uenyekiti wa Mohamed Wandi na katibu wake Maulid Said ulikuwa na ajenda iliyojadili mwenendo mbovu wa klabu ya Simba kwenye Ligi Kuu inayoendelea na kutokuwa na imani na viongozi wa Simba.
Akizungumza wakati akifungua mkutano huo uliokuwa na utulivu mkubwa huku ukilindwa na askari polisi wachache, Wandi alimlaumu Rage kwa madai kwamba amekuwa akiiendesha klabu yao bila kufuata katiba.
“Ibara ya 16 kipengele G inasema kutakuwa na mkutano kila baada ya miezi minne kujadili maendeleo ya klabu, lakini haujafanyika mpaka leo.
Alisema,“Ibara ya 22 ya katiba ya klabu ya Simba inatupa wanachama haki ya kuitisha mkutano endapo mwenyekiti na makamu mwenyekiti hawatakuwapo na Ibara ya 19 kifungu cha tatu inatupa mamlaka ya kumwandikisha na kumfukuza mwanachama.”
Baada ya kumaliza kusoma sehemu ya katiba ya klabu ya Simba aliyodai imekiukwa, Wandi aliwataka wanachama wenzake kuamua kama Rage na kamati yake ya utendaji ipewe muda zaidi au iondolewe ndipo wote waliponyoosha mikono juu wakitaka watimuliwe na kuunda kamati ya muda chini ya Hans Pope na Rahma Al Kharoos.
Hata hivyo, Hans pope alikataa kuchukua jukumu hilo akisema “Sijapewa taarifa yoyote juu ya uteuzi huo, hata hivyo siafiki suala hilo kwa vile hawajaomba hata ushauri kabla ya kufikia uamuzi wao.”
Juhudi za Mwananchi kuwapata viongozi wa Simba akiwamo ziligonga mwamba huku simu zao zikiita bila kupokelewa.

SOURSE: MWANANCHI


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU