HALMASHAURI ya Manispaa ya Kigoma Ujiji imeanza mchakato wa
kuwakusanya watoto wadogo walemavu wanaoomba mitaani na kuwapeleka katika kituo
cha walemavu Kabanga, wilayani Kasulu kwa ajili ya kuanza masomo ya shule ya
msingi.
Ofisa Elimu Shule ya Msingi wa
Manispaa ya Kigoma Ujiji, Shaaban Bane aliyasema hayo wakati wa kuwasafirisha
watoto wanane waliotambuliwa kwenda Kasulu kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa
mchakato huo.
Bane alisema baada ya kufika kwenye
manispaa hiyo, aligundua tatizo la watoto wengi wadogo wenye ulemavu kutumika
kama vitega uchumi na familia zao kwa kuomba fedha mitaani badala ya kwenda
shuleni.
Kimsingi alisema kuwa hiyo inaonesha
kuwa uduni wa kipato (umasikini) wa familia hizo ambazo haziwezi kuwapeleka
watoto hao shuleni na kwamba wao kama Serikali wameona wachukue jukumu la
kuhakikisha watoto hao wanapata haki yao ya kupata elimu.
Kwa sasa, Ofisa Elimu huyo alisema
kuwa jumla ya watoto wanane wamepatikana kutoka maeneo mbalimbali ya manispaa
ya Kigoma Ujiji na mchakato wa kuwafanya wajiunge na shule maalumu ya Kabanga
wilayani Kasulu umekamilika na jana walisafirishwa kuelekea huko.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma
Ujiji, Alfred Luanda alisema wazazi wanalo jukumu la kuhakikisha watoto wao
wanapata elimu badala ya kuchukulia ulemavu wao kama kigezo cha kuwafanya wao
ni masikini na kuanza kuzunguka mitaani kuomba fedha kwa wasamaria wema.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog