SHULE ya Sekondari ya Kichangachui katika Manispaa ya Kigoma
Ujiji imetoa mwanafunzi bora wa masomo ya sayansi kwa Kanda ya Magharibi katika
mtihani wa majaribio (Mock Test) wa kidato cha nne uliofanyika hivi karibuni.
Akitoa taarifa kwa Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Chung IL aliyefika
shuleni hapo kukabidhi rasmi maabara kwa uongozi wa shule hiyo Mkuu wa Shule
hiyo, Harles Lugenda alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na kuanzishwa kwa
maabara ya masomo ya sayansi katika shule hiyo.
Lugenda alimtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Justus Ferdinand
ambaye aliongoza katika masomo ya Fizikia na Kemia ambapo alisema kwamba kuwepo
kwa maabara hiyo iliyoanza kufanya kazi Januari mwaka huu kumeinuka ari ya
wanafunzi wa shule hiyo kusoma masomo ya sayansi na kuahidi kufanya vizuri.
Maabara hiyo imetolewa na serikali ya Jamhuri ya Watu wa Korea kupitia Shirika lake la Maendeleo (KOICA)
ambapo kiasi cha Sh milioni 25 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa vyumba
viwili vya madasara vinavyotumika kama vyumba
vya maabara na vifaa vyake.
Sambamba na ujenzi wa vyumba hivyo vya maabara pia Serikali
ya Korea kupitia shirika hilo inagharamia masomo ya wanafunzi wanane wanaosoma
masomo ya sayansi shule hapo ambapo tayari wameshalipiwa ada kwa miaka minne
ahadi watakapomaliza masomo yao
ya sekondari.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Balozi Chung IL alisema
kuwa msaada huo umelenga kunaimarisha ushirikiano wa kindugu uliopo baina ya
serikali hizo mbili na watu wake.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispa ya Kigoma Ujiji ,
Alfred Luanda alisema kuwa pamoja na msaada huo bado Manispaa hiyo inakabiliwa
na upungufu wa maabara za sayansi na vifaa vyake katika shule zake mbalimbali
na kwamba kama ipo fursa ya kupata tena msaada zaidi aliomba serikali ya Korea
kuangalia uwezekano huo.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog