Facebook Comments Box

Thursday, October 25, 2012

POLISI AGOMBEA UONGOZI UVCCM-NEC

WAKATI Mkutano Mkuu wa Nane wa Uchaguzi wa Umoja wa Vijana (UVCCM) ukimalizika, mmoja wa wagombea wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho nafasi sita Tanzania Bara, Stanley Mdoe, ametiwa mbaroni na Polisi akibainika kuwa askari Polisi.

Askari huyo mwenye namba F 7961 wa cheo cha Konstebo, anatoka kituo cha Polisi Mvomero, Morogoro ambaye alibainika jana akijihusisha na siasa hata kuingia kinyang’anyiro cha kuwania ujumbe wa NEC kupitia Vijana.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana Morogoro, askari huyo alijitambulisha kwa baadhi ya wajumbe kuwa yeye ni mtoto wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, akijiita Stanley Bendera.

Wapambe waliofuatana naye kutoka Morogoro wakiwa Dodoma waliarifu kuwa mgombea huyo alikamatwa juzi jioni akiwa amevalia sare za chama hicho akiomba kura kwa wajumbe ili wamchague kwa nafasi hiyo.

Hata hivyo, ilielezwa na baadhi ya wanachama waliofuatana naye na wengine wanaotambua kazi yake uaskari, waliwajulisha maofisa usalama waliokuwa eneo hilo nao kufikisha taarifa hizo Polisi na kukamatwa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, askari huyo alikuwa ameomba likizo isiyo na malipo, wakati wengine wakidai kuwa ameacha kazi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile akizungumzia tukio hilo alisema alipata taarifa ya kukamatwa kwa askari huyo Dodoma na kwamba wakati huo alikuwa akimtafuta kwa siku mbili kwa ajili ya shughuli za kikazi bila mafanikio.

“Sina uhakika kama askari huyu amejiingiza katika siasa ... nimetuma askari wengine kwenda Dodoma kufanya uchunguzi wa suala hilo,” alisema Kamanda Shilogile na kuongeza:

“Iwapo itabainika kuwa kweli, atachukuliwa hatua stahiki na kinidhamu kulingana na taratibu za kijeshi. Hata hivyo siwezi kuzungumzia suala la ugombeaji wake, sijathibitisha ukweli wake, isipokuwa hakuwa kazini kwa siku mbili na ni utovu wa nidhamu kwa Jeshi letu kutoonekana eneo la kazi,” alisema Kamanda Shilogile.

Kwa mujibu wa Kamanda, sheria za nchi na Katiba kuna vifungu vinavyohusu majeshi ya ulinzi na usalama vikitamka kuzuia na kupiga marufuku mwanajeshi kujihusisha na siasa.

Alisema iwapo jambo hilo litabainika, litakuwa limefanyika kinyume na kanuni na taratibu za kazi ya uaskari. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bendera, hakupatikana ofisini kwake wala kwa njia ya simu ya mkononi ili kufafanua kadhia hiyo.

Hata hivyo wasaidizi wake walidai kuwa yuko nje ya nchi kwa shughuli za kikazi.





Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU