Yondan wa pili kutoka kulia waliosimama katika kikosi cha Yanga jana |
Yanga wapo
Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo hivi sasa wakifanya mazoezi, lakini
Yondan anajiandaa kwenda hospitali kufanyiwa uchunguzi wa maumivu yake.
Habari kutoka
Yanga, zimesema kwamba tangu jana beki huyo anasikia maumivu makali na hatima
yake itajulikana baada ya vipimo hivyo.
Yanga jana
ilitoka nyuma na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wapinzani wao wa
jadi, Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, uliopigwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuanzia saa 1:02 usiku.
Habari
kutoka ndani ya Simba, zimesema kwamba wachezaji waliahidiwa asilimia ya 60 ya
mgawo wa timu kutokana na mapato ya milangoni na asilimia 20 ya kiwango hicho
kuongezwa na Friends of Simba, lakini kwa sare hiyo, ahadi hiyo imeota mbawa.
Hata hivyo,
uongozi wa Simba unafikiria kuwapa ‘kifuta jasho’ wachezaji wake kwa angalau
kulinda hadhi ya klabu kwa kutokubali kufungwa na wapinzani wao hao wa jadi
jana.
Yanga ambao
walimaliza mechi hiyo wakiwa pungufu baada ya Simon Msuva kutolewa nje kwa kadi
nyekundu dakika ya 77 kwa kumrudishia rafu Juma Nyosso, ndio waliohaha
kusawazisha bao, baada ya kutanguliwa kwa bao la mapema la kiungo Amri
Kiemba.
Hadi
mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na kiungo
Amri Kiemba dakika ya pili.
Simba
walicheza vizuri kipindi chote cha kwanza wakigongeana pasi za uhakika na
kuwazidi kasi uwanjani wapinzani wao, wakati Yanga pamoja na kuzinduka baada ya
kufungwa bao, lakini makosa yalikuwa mengi.
Pasi zao zilikuwa
nyingi hazifiki, walikuwa wanapokonyeka mipira kirahisi, wanazidiwa nguvu na
wapinzani wao katika kugombea mipira na hata mashambulizi yao hayakuwa ya
mpangilio, zaidi ya kuonekana kubahatisha zaidi.
Katika
kubahatisha huko, Mbuyu Twite alifumua shuti zuri dakika ya 38 kutoka wingi ya
kulia, ambalo lilitoka nje sentimita chache.
Kabla hata
ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika, kocha Mholanzi Ernie Brandts
alimtoa Hamisi Kiiza na kumuingiza Frank Domayo ili kuimarisha safu ya kiungo,
ambayo ilionekana kuzidiwa na Simba inayofundishwa na Mserbia, Milovan
Cirkovick.
Kipindi cha
pili, Yanga walianza na mabadiliko, kocha Ernie Brandts akimtoa kiungo Nizar
Khalfan na kumuingiza mshambuliaji Didier Kavumbangu, ambaye alikwenda kuongeza
nguvu ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Angalau,
kipindi cha pili Yanga walionekana kucheza vizuri na kupeleka mashambulizi
yenye uhai langoni mwa Simba, ingawa safu imara ya ulinzi ya Wekundu wa
Msimbazi ilikuwa kikwazo.
Katika
dakika ya 63, beki Paul Ngalema aliunawa mpira katika harakati za kuokoa na
refa Mathew Akrama akaamuru penalti, ambayo ilikwamisha kimiani kiufundi na
Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Katika
dakika ya 77 Mathew Amkrama alimtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja
Simon Msuva, baada ya kumkita Juma Nyosso, aliyemkanyaga ‘kwa bahati mbaya’.
Msuva alichezewa rafu na Nyosso na tayari refa alikwishapuliza filimbi na kumpa
kadi ya njano beki huyo wa Simba, lakini kiungo huyo wa Yanga akaponzwa na
hasira za kitoto.
Pamoja na
Yanga kubaki pungufu, waliendelea kucheza vema na mashambulizi yalikuwa ya
pande zote mbili. Refa Akrama alishindwa kuumudu mchezo na maamuzi yake mengi
yalikuwa chungu kwa Yanga, mfano Haruna Moshi ‘Boban’ alipomchezea rafu mbaya
beki Kevin Yondan hadi akashindwa kuendelea na mchezo, na nafasi yake
ikachukuliwa na Juma Abdul alimpoza kwa kadi ya njano.
Hakumchukulia
hatua yoyote kipa Juma Kaseja aliyeonekana kupoteza muda tangu mwanzo, na
alimpa onyo tu zaidi ya mara tatu.
Alipingia
Abdul alikwenda kucheza beki ya kulia na Mbuyu Twite akahamia katikati kucheza
na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Baada ya
mchezo huo, kocha wa Simba, Milovan alisema kwamba ulikuwa mchezo mzuri na
Yanga walicheza vizuri, lakini timu yake ilicheza vizuri na anajivunia. Alisema
Yanga imeimarika tofauti na ilivyokuwa awali na kwamba hizo ni dalili Ligi Kuu
msimu huu itakuwa ngumu.
Kwa upande
wake, kocha wa Yanga, mwanzoni hawakucheza vizuri, lakini baadaye walitulia na
kucheza vizuri. “Hii ni mechi ya kweli ya upinzani, unaweza kuona rafu na kadi
nyingi,”alisema Brandts.
Kwa matokeo
hayo, Simba imefikisha pointi 13, ndani ya mechi tano na kuendelea kuongoza
Ligi Kuu, wakati Yanga imefikisha pointi nane na kubaki nafasi ya tano, kwani
Coastal Union imetoa sare ya 2-2 na JKT Oljoro mjini Arusha na kufikisha pointi
tisa.
SIMBA: Juma
Kaseja, Nassor Chollo, Paul Ngalema, Juma Nyosso, Shomary Kapombe, Jonas Mkude/Haruna
Moshi, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Edward Christopher/Daniel
Akuffo na Mrisho Ngassa.
YANGA: Yaw
Berko, Mbuyu Twite, Stefano Mwasyika, Nadir Cannavaro, Kevin Yondan/Juma Abdul,
Athumani Iddi, Simon Msuva, Haruna Niyonzima,
Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza/Frank Domayo na Nizar Khalfan/Didier Kavumbangu.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog