Facebook Comments Box

Wednesday, December 31, 2014

HAKIMU AJITOA KESI YA UAMSHO




 Sheikh Farid Katikati ya Askari Magereza.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hellen Liwa amejitoa kusikiliza kesi ya ugaidi inayowakabili viongozi 23 wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI).
 
Hakimu huyo amefikia uwamuzi huo baada ya wakili wa washtakiwa hao wa ugaidi, Abubakar Salim kumtaka ajitoe kuisikiliza kesi hiyo ili iweze kupangiwa hakimu mwingine ambaye atatoa uamuzi juu ya hoja zao walizozitoa mahakamani hapo Septemba 19,2014.

Salim aliiambia mahakama kuwa baada ya kushauriana na wateja wao na uamuzi uliotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu, Dk Fauzi Twaib wakaona kuwa ni ukweli kuwa Hakimu Liwa alikwisha toa uamuzi wake juu ya hoja zao Oktoba Mosi, 2014 kuwa mahakama hiyo ya kisutu haina mamlaka ya kusikiliza hoja hizo. 

Alidai Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Twaib umeelekeza kuwa Mahakama ya Kisutu inayo mamlaka ya kuzisikiliza hoja za washtakiwa hao wa ugaidi na hata kuzitolea uamuzi.

"Mahakama Kuu imeelekeza mawakili wa upande wa utetezi kama tutakuwa na hoja mpya ama  zile za awali tuzitoe kwenye mahakama hii ya Kisutu ili ziweze kutolewa maamuzi hivyo naona ni bora ujitoe tupate neno kutoka kwa hakimu mwingine."Alisisitiza kusema wakili huyo mahakamani hapo.

Wakili wa Serikali Mkuu, Benard Kongola alimuomba Hakimu Liwa asijitoe katika kuisikiliza kesi kwa madai sababu zilizotolewa na upande wa utetezi za kumtaka ajitoe hazina msingi.

Kongola alieleza kuwa uamuzi uliotolewa na Jaji Twaib aliamuru utekelezaji wa hoja za upande wa utetezi katika kesi hii ya ugaidi zisikilizwe na kutolewa uamuzi katika Mahakama ya Kisutu.

"Tukiendekeza hii tabia tutamaliza mahakimu wote wa mahakama hii tunasisitiza upande wa utetezi utoe sababu za msingi za wewe kujitoa."Alisema Kongola.
Akijibu hoja hizo, Wakili Salim alieleza kuwa ili haki ionekane inatendeka wewe Hakimu Liwa ujitoe ili hakimu mwingine atoe maamuzi wa hoja zetu.

Hakimu Liwa alisema ni kweli nilikwisha toa uamuzi wangu juu ya maombi ya washtakiwa lakini Mahakama Kuu imeona kivingine kuwa sijatumia mamlaka yangu vizuri nakubaliana na uamuzi huo.
Lakini uamuzi huo wa Jaji Twaib haukufafanua nini kifanyike, umetuacha hoi, ila alitoa angalizo kuwa ushahidi wa kesi hauwezi kutoka hewani na kwamba maelezo yaliyomo katika hati ya mashtaka ya kesi hiyo yapo sahihi.

"Kitu ambacho hata mimi nilikuwa nakishangaa ni hii hati ya mashtaka kuletwa Tanzania Bara badala ya Visiwani, lakini nilipoisoma sheria ya ugaidi nikabaini mtu anaweza kushtakiwa mahali popote." Alisema Hakimu Liwa.Alisisitiza kuwa kwa mujibu wa sheria Mahakama Kuu ndiyo yenye uwezo wa kuisikiliza kesi hii na siyo mahakama ya Kisutu hivyo yeye hawezi kusema kitu labda kesi ingekuwa imefikia kwenye mwenendo wa uhamishaji shauri (Committal Preceding).

Hatua hiyo inafikiwa baada ya upelelezi wa kesi kukamilika inahamishwa kutoka mahakama ya Kisutu kwenda Mahakama Kuu ambayo inamlaka ya kusikiliza kesi hizo.

"Mimi nimejifunza kitu hapa, kuwa mimi najua nini na wenzangu wanajua nini hivyo siwezi kuendelea na kesii haitakuwa haki najitoa."Aliongeza kusema Hakimu Liwa na akajitoa na kuiahirisha hadi Januari 13,2015 ili ipangwe kwa hakimu mwingine.


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU