Facebook Comments Box

Thursday, August 14, 2014

UGONJWA WA EBOLA WAZUA TAFRANI SHINYANGA


Wakazi wa Manispaa ya Shinyanga, kwa siku mbili mfululizo
walikumbwa na kiwewe, baada ya kuenea uvumi kwamba kuna
mgonjwa wa mwenye homa hatari ya ebola, aliyefikishwa katika
Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga.
Taarifa za kuwepo kwa mgonjwa huyo, zilidai kuwa mgonjwa huyo
alitoka katika moja ya mitaa ya Manispaa ya Shinyanga na  alikuwa
akitokwa damu puani na mdomoni kabla ya kuzimia.
Akizungumzia hali hiyo jana, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,
Dk Ntuli Kapologwe alisema mgonjwa huyo ambaye alikuwa
akitokwa damu mdomoni na puani, alifika hospitalini hapo juzi na
baada ya kufika wauguzi na madaktari walitaharuki.
Kwa mujibu wa Dk Kapologwe, mgonjwa huyo alipelekwa chumba
cha wagonjwa mahututi (ICU), huku baadhi ya wauguzi na
madaktari wakimkimbia hali iliyotia hofu kwa baadhi ya wahudumu
na hata wagonjwa hospitalini hapo.
Hata hivyo, Dk Kapologwe alisema baada ya uchunguzi wa awali,
ilibainika kuwa mgonjwa huyo ana matatizo ya kutokwa damu mara
kwa mara na hajaambukizwa virusi hao wa ebola.
Akielezea namna mkoa ulivyojiandaa kukabiliana na ugonjwa huo
uliokwishaua zaidi ya watu 1,000 katika nchi za Afrika Magharibi,
Dk Kapologwe alisema waganga wakuu katika halmashauri zote sita
za wilaya mkoani Shinyanga, wameshajiandaa.
Alisema wamekubaliana atakapogundulika mtu mwenye dalili za
ugonjwa huo, taarifa itolewe mara moja katika ngazi ya mkoa,
ambako kuna timu maalumu ya wataalamu iliyoandaliwa
kushughulika na ugonjwa huo hatari.
Baada ya taarifa kutolewa kwa mujibu wa Dk Kapologwe, timu hiyo
itathibitisha kama mgojwa ana dalili zote za ebola na taarifa
kutolewa kwa umma.
Wakati ugonjwa huo ukisababisha kiwewe mkoani Shinyanga,
mkoani Kagera, Mkuu wa Mkoa, Fabian Massawe ameshauri wakazi
wa mkoa huo kuwa macho na tayari kutoa taarifa kwenye vituo vya
afya vilivyo jirani waonapo mtu mwenye dalili  za ugonjwa huo.
Alitoa mwito huo kupitia kwa waandishi wa habari aliozungumza
nao jana ofisini kwake mjini hapa, baada ya kuibuka taarifa kuwa
Rwanda kulikuwa na mtu anayehisiwa kuwa na ebola.
Hata hivyo, Waziri wa Afya wa Rwanda, Agnes Binagwaho alisema
juzi kuwa mwanafunzi mmoja wa Ujerumani aliyefika nchini humo
akitokea Liberia,  alihisiwa kuwa na ugonjwa huo lakini baada ya
sampuli ya damu yake kupimwa katika maabara za kimataifa,
hakukutwa na ugonjwa huo.
Massawe alisema Mkoa wa Kagera unapakana na nchi mbalimbali
za Afrika Mashariki na pia upo mwingiliano wa watu na shughuli
mbalimbali za kijamii.
Alisema nchi jirani zikipata mlipuko wa ugonjwa huo, upo
uwezekano wa kuvuka mipaka na kuingia mkoani Kagera, hivyo ni
wajibu wa kila mmoja kutoa taarifa akiona mtu anayedhaniwa kuwa
na ugonjwa huo.
Dalili za ugonjwa huo unaoenezwa na virusi vya ebola ni pamoja
na kutokwa na damu sehemu mbali mbali za mwili, kuumwa na
kichwa, mwili kuishiwa nguvu, maumivu ya misuli na hatimaye kifo.
Ugonjwa huo unaambukizwa kwa kugusa damu na majimaji ya
mgonjwa pamoja na kugusa vifaa au nguo za mgonjwa.
Massawe alisema Kagera wamechukua hatua kwa kuweka mikakati
kuhakikisha mlipuko wa ugonjwa  hauingii nchini  kupitia mipakani.
Miongoni mwa halmashauri ambazo zimeelekezwa kuchukua
hadhari kutokana na kuwa mpakani mwa nchi, ni wilaya ya Bukoba,
Missenyi, Karagwe, Kyerwa na Ngara.


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU