Katika siku za hivi karibuni, kumekuwapo na mjadala kuhusiana na hatua ya
klabu ya Yanga kupinga udhamini wa Ligi Kuu ya Tanzania unaotarajiwa
kufanywa na Azam Media.
Tumeona ni vema tukatoa msimamo wetu wa pamoja kuhusiana na hatua hiyo ya wenzetu kwa lengo la kuweka rekodi sawa. Tunataraji hatua hii ya vilabu hivi 13 itafunga mjadala huu na
tungependa wana habari, kama mtaamua kuuendeleza, basi muundeleze katika
mlengo ambao wadau, yaani sisi vilabu vinavyoshiriki mashindano hayo,
zimeamua kuufuata.
Tunapenda kukumbusha kwamba kwa muda mrefu, kilio cha vilabu vya Ligi
Kuu ya Tanzania kilikuwa ni ukosefu wa wadhamini na kwa bahati nzuri
kuna dalili kwamba Mungu ameanza kukisikia kilio hicho msimu huu.
Kwa faida ya umma, tungependa kutoa takwimu za nchi jirani
zinazotuzunguka. Kenya, kila klabu hupata Sh milioni saba za Kenya (sawa
na Sh milioni 125 za Kitanzania) kwa mwaka –fedha ambazo zimeifanya
ligi ya Kenya kuwa na uwiano na ushindani wa kweli (fedha hizo ni
mjumuisho wa gharama za matangazo ya televisheni na udhamini wa bia ya
Tusker).
Tanzania leo tunajivunia kuwazidi Kenya kutokana na udhamini wa Azam
ambapo kwa mwaka huu, kila klabu itapata zaidi ya Sh milioni 170 (Jumla
kutoka milioni 100 za Azam na milioni 70 za Vodacom).
Hatuna sababu ya kutaja viwango vya udhamini kwa nchi nyingine jirani
kama Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia nk kwa vile zote zina udhamini wa
chini kuliko Kenya. SuperSport, ambao wanaliliwa na baadhi yetu, udhamini wao kwa ligi ya
Uganda ni dola 350,000 ambazo ni pungufu kulinganisha na dola milioni
moja zilizotolewa na Azam Media hapa nchini.
Ni imani yetu kwamba udhamini huu utaifanya ligi ya Tanzania kuwa bora
kuliko zote za Afrika Mashariki. Hili litasaidia kutengeneza timu bora
ya Taifa ya Tanzania. Tungependa kutoa ufafanuzi wa masuala machache ambayo yaliongelewa na wenzetu wa Yanga kama sababu za kupinga udhamini huu.
BODI YA TPL
Kwa mujibu wa Katiba za FIFA, CAF na TFF, Haki za Televisheni zipo chini ya FA ya nchi husika. TFF iliamua kukasimu shughuli ya majadiliano kwa Kamati ya Ligi ambayo ilishirikisha vilabu vyote 14, ikiwamo Yanga na wawakilishi wake walihudhuria mchakato mzima hadi mwisho.
Kwa mujibu wa Katiba za FIFA, CAF na TFF, Haki za Televisheni zipo chini ya FA ya nchi husika. TFF iliamua kukasimu shughuli ya majadiliano kwa Kamati ya Ligi ambayo ilishirikisha vilabu vyote 14, ikiwamo Yanga na wawakilishi wake walihudhuria mchakato mzima hadi mwisho.
Hoja ya Yanga kuwa bodi haina nguvu/Mamlaka kisheria kwa kuwa ni ya
mpito inakosa mashiko kwa sababu kimsingi ni TFF ndiyo iliyoingia
mkataba kwa sababu ndiyo iliyopewa mrejesho na Kamati ya Ligi kwamba
mchakato umekwenda sawasawa.
Hoya ya kuwa Bodi ya TPL iliyoko sasa hivi haina mjumbe hata mmoja
aliyeteuliwa kutoka YANGA. Hili si kweli hata kidogo. Mmoja wa wajumbe
wa TPL ni Seif Ahmed almaarufu Seif Magari; ambaye vyeo vyake ndani ya
Yanga vinajulikana.
Kama alikuwa hahudhurii vikao vya TPL, hilo ni suala la Wanayanga
wenyewe kumuhoji kwanini alikuwa hahudhurii hivyo na hivyo kuinyima
klabu yake ushiriki katika mijadala muhimu kwa maslahi ya soka hapa
nchini. Ifahamike pia kwamba TPL haikuhodhi mchakato huu bali ilitoa fursa kwa
vilabu vyote vya Ligi Kuu kushiriki ambapo Yanga ilikuwa ikiwakilishwa
na Makamu Mwenyekiti wake, Clement Sanga na Katibu Mkuu, Lawrance
Mwalusako.
Hii maana yake ni kwamba hoja kuwa Yanga haikushirikishwa ni mfu. Yanga walitumia neno UTARATIBU WA DUNIA NZIMA wakisema eti hakuna
mahala duniani ambapo kampuni yenye klabu inayocheza ligi husika kupewa
mkataba wa udhamini au urushwaji wa matangazo.
Inaonekana Yanga hawakufanya utafiti kwani ligi ya Afrika ya kusini ina
timu inayoitwa Super Sports United na inarushwa na kituo cha TV
chaSupersports. Pia majirani zetu Kenya wana timu inayoitwa Tusker FC huku ligi hiyo ikidhaminiwa na bia ya Tusker.
Tunawashauri Yanga kuwa ni vema kufanya utafiti kabla ya kuibuka na hoja za namna hii ili kuepuka kuwapotosha wanachama wao. Yanga pia katika hoja zao wamepinga utaratibu wa kugawana mapato sawa.
Hoja hii ni ya msingi na majadiliano yetu yalilitazama hili kwa kina
lakini tukaona kwa mazingira ya Tanzania na uchanga wa ligi yenyewe kwa
sasa ni heri kugawana sawa ili pesa kwa usawa ili itoke kwa wakati na
kusaidia vilabu kujiendesha.
Yanga wanakosea wanaposema eti wao
wanastahili kupewa zaidi kwa sababu ni klabu kubwa na yenye mashabiki
wengi kwa kuwa sababu hii haitumiki sehemu yoyote duniani.
Tuchukulie mfano wa nchi ya England ambako ingawa Liverpool ina
washabiki wengi kuliko Manchester City na Chelsea, imezidiwa kwenye
mapato ya televisheni na timu hizo.
Hii ni sababu kinachoamu mapato mwisho wa siku ni kiasi cha mechi za
timu ambazo zimeonyeshwa na televisheni kwenye msimu husika na nafasi ya
timu kwenye msimamo wa ligi.
Hata hivyo, ikumbukwe kwamba nchini England, malipo haya hufanyika
baada ya msimu kumalizika na hapo ndipo watu hukaa chini na kupigiana
hesabu za nini kilipatikana. Sasa ukitumia mfumo huu, ina maada timu
zitalazimika kusubiri ligi iishe ili kuangalia msimamo ya ligi kisha
kugawana mapato. Sote tunajua jinsi timu zinavyoteseka kwa kukosa nauli,
posho, mishahara, pesa za kambi nk.
Kwa mazingira yetu ya Tanzania kwa sasa, mfumo kama huu haufai. Hii ni
kwa sababu timu zinahitaji fedha kuanzia kwenye maandalizi ya mechi ya
kwanza na hazikopesheki fedha kwenye mabenki. Tanzania inachohitaji kwa sasa ni ligi yenye ushindani tofauti na sasa
ambapo ushindani uko kwa timu chache zenye uwezo wa kifedha.
Tukizijengea uwezo timu zote taifa litakuwa na ligi nzuri na hatimaye
timu nzuri ya taifa. Pia itawezesha wadhamini wengi zaidi kuingia kwenye
mpira na hivyo timu nyingi zaidi kufaidika.
Tukifikia huko, tunaweza kukaa chini na kutazama mfumo wa kugawana mapato utakaokuwa bora zaidi wakati huo.
Mambo ya Kuzingatia.Tangu ligi ianze hapa nchini takribani miaka 50
iliyopita, hakuna timu iliyowahi kulalamikia mfumo wa kugawana mapato
sawa kwa kila mechi ambao umekuwa ukitumika. Mfano mapato ya mlangoni
tumekuwa tukigawana sawa na Yanga haijawahi kulalamika, Pesa za udhamini
wa Vodacom tangia ilipokuwa ikidhaminiwa na TBL hadi leo hii tumekuwa
tukigawana sawa na Yanga haijawahi kulalamika kutaka kupata zaidi kwa
kuwa eti ina mashabiki wengi, pia hata pesa za haki ya matangazo ya
Televisheni zilizowahi kutolewa huko nyuma nailiyokuwa ikiitwa GTV, na
Star TV kwa nyakati tofauti pesa ziligawiwa sawa kwa kila timu.
Hii ni kwa sababu kikanuni, timu zote zinazoshiriki kwenye ligi ni sawa na zote zinaweza kuwa bingwa au kushuka daraja. Ni mdudu gani huyu aliyeingia kwenye soka ya Tanzania na kuanza kuleta
siasa za kubaguana? Baba wa Taifa alipata kutuasa kwamba dhambi ya
ubaguzi ni sawa na kula nyama ya mtu. Ikianza, haitaishia kwenye ligi
pekee na itakwenda hadi mahali tusipotaka.
MGOGORO WA MASLAHI.
Yanga imekuwa ikilalamikia uwepo wa kiongozi mwandamizi wa makampuni ya
Bakhresa kwenye bodi ya Ligi na kusema inaleta mgongano wa maslahi. Sisi vilabu tunaamini kwamba uwepo wa kiongozi huyu ndiyo umesaidia
makampuni yake kuwekeza fedha kwenye mpira. Na mifano ipo hai tukianzia
na michuano ya Vijana ya Uhai Cup, ujenzi wa kituo cha michezo cha
Chamazi ambacho kinatumiwa na timu nyingi za Tanzania.
Na sasa tunafaidika na udhamini huu mnono ambao haujapata kutokea katika historia ya Tanzania. Tungependa viongozi wengi zaidi wa makampuni yanayoheshimika hapa
nchini wakijitokeza kuongoza mpira badala ya kuanza kuwapinga. Kwa mfano tungependa kuona Mkurugenzi wa Benki ya CRDB akiwa kiongozi
wa Ashanti, bosi wa Barrick akiongoza Mbeya City na Mkurugenzi wa Tanga
Cement akiongoza Coastal Union.
Hivi ndivyo namna mpira unavyoweza kuvutia wawekezaji. Ndiyo maana tulifurahi wakati Yusuf Manji, alipoomba uongozi Yanga.
Bado tunataraji kwamba naye atajitosa kuingiza fedha zake kwenye ligi
ya Tanzania (mpira) kama alivyofanya Bakhresa ambaye pamoja na kutumia
fedha zake Azam FC, bado ameamua kusaidia na timu nyingine kwa ujumla. Tunapenda kumuahidi Yusuf Manji kwamba iwapo naye atataka kudhamini
Ligi Kuu iwe kibiashara au kiufadhili, sisi tutamuunga mkono na
hatutajali suala la mgongano wa maslahi.
UPOTEVU WA MAPATO
Wenzetu Yanga wamedai kwamba kwa kuonyesha mechi kwenye televisheni, mapato yake ya mlangoni yatapungua.
Wenzetu Yanga wamedai kwamba kwa kuonyesha mechi kwenye televisheni, mapato yake ya mlangoni yatapungua.
Hili pia halikufanyiwa utafiti wa kutosha. Katika siku za karibuni,
mechi zilizoingiza mapato makubwa zaidi ya milangoni ni zile ambazo
zilionyeshwa Live kwenye televisheni za ndani na nje ya nchi. Mifano ni mechi za watani wa jadi msimu uliopita zilizoonyeshwa Live na
SuperSport na mechi za Kombe la Kagame zilizoonyeshwa wakati huo.
Hata mechi ya Taifa Stars na Ivory Coast iliyoonyeshwa Live pia,
ilijaza uwanja. Ulaya ambako karibu kila familia inamiliki televisheni
na umeme wa uhakika, bado watu wanajaa katika viwanja vya soka. Mpira kuonyeshwa kwenye televisheni unaufanya utangazike zaidi na watu
watake kuona. Kuna faida nyingi za mpira kuonyeshwa kwenye televisheni
kuliko hasara moja ya kufikirika ambayo Yanga wanaiona.
Ingekuwa vema iwapo Yanga wangetoa takwimu za kuonyesha ni kwa namna
gani mechi kuonyeshwa kwenye televisheni kuliwahi kupunguza mapato ya
milangoni. Kwa faida ya umma, mpira kuwa kwenye televisheni kuna faida zifuatazo;
jezi kuongezeka thamani na hivyo kuvutia makampuni makubwa kutaka
kudhamini klabu wakitumia fursa ya kutangaza bidhaa zao, matangazo ya
viwanjani (touchline fence) kuwa na thamani zaidi ambapo kwa sasa vilabu
havipati chochote, kuchochea michezo ya kubahatisha, kutabiri matokeo
na kupata habari kupitia simu za mkononi na hivyo vilabu vitaanza
kutengeneza fedha za kutosha.
Ulaya wamesonga mbele kutokana na televisheni. Anayekataa mpira
kuonyeshwa kwenye televisheni ni sawa na mtu anayegoma kutumia mfumo wa
digitali katika ulimwengu wa leo.
UWAZI KWENYE MCHAKATO WA KUUZWA KWA HAKI ZA MATANGAZO
Yanga wameandika kwenye taarifa yao rasmi eti hakukuwa na uwazi kwenye mchakato wa kuipata kampuni ya kurusha matangazo ya Televisheni. Sote tunajua kuwa vituo vya televisheni vilivyopo nchini kama Star TV ambayo iliwahi kurusha mechi kadhaa msimu uliopita vilikuwa vikijua kuwa kuna nafasi hiyo na TFF mara kadhaa wamekuwa wakitangaza hilo kupitia idara ya Habari ya TFF.
Yanga wameandika kwenye taarifa yao rasmi eti hakukuwa na uwazi kwenye mchakato wa kuipata kampuni ya kurusha matangazo ya Televisheni. Sote tunajua kuwa vituo vya televisheni vilivyopo nchini kama Star TV ambayo iliwahi kurusha mechi kadhaa msimu uliopita vilikuwa vikijua kuwa kuna nafasi hiyo na TFF mara kadhaa wamekuwa wakitangaza hilo kupitia idara ya Habari ya TFF.
TFF kwa mfano walikwenda mbali kwa kuialika Supersports kuja kuonesha
mechi bure kwa kilichokuwa kikiitwa Super Week ili kuwashawishi waje
kuwekeza na mara ya mwisho ni Yanga hawa hawa walioongoza harakati za
kuikataa Supersports kuonesha mechi bure wakisema kuwa kama ni kuwavutia
inatosha. Katika mazingira kama haya tunastaajabishwa na ukigeugeu wa Yanga leo
kusema eti tenda haikuwekwa wazi. Sote tunajua kuwa ni Super Sports
pekee tuliokuwa tukiwategemea na kuwashawishi ambao hawakuonesha
kuhitaji kuja kuwekeza. Kwa nini leo tuikatae Azam TV?
Yanga wanaposema eti TFF/Kamati ya Ligi imeipa haki za matangazo
kampuni ambayo haina ofisi wala kituo cha televisheni kilicho hewani kwa
sasa wanasahau kuwa huko nyuma TFF iliwahi kuwapa haki za matangazo GTV
ambao hawakuwa na ofisi wala kituo cha TV na baada ya miezi michache
walifungua ofisi zao na kuleta vingamuzi na kuaza kurusha mechi zetu.
Vilabu vilifaidi udhamini ule kabla ya ile kampuni kufilisika. Kwa hiyo
hii si mara ya kwanza kwa jambo hili kufanyika na kama Azam TV
hawataonesha mechi za ligi hiyo sisi kama vilabu haituhusu kwani ni
hasara yao.
Tunachowaomba Azam Media sisi kama vilabu ni kuhakikisha wanatulipa
pesa zetu kwa haraka ili zitusaidie kwenye maandalizi,Tunawaomba Yanga
wasichafue hali ya hewa kwa kuwa wao hawana shida ya Pesa.
Sisi Umoja wa Vilabu 13 vinavyoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania tunapinga,
kwa nguvu zote, madai ya Yanga kwamba hatukushirikishwa kama vilabu
kwenye mchakato huu. Mfumo wa ugawanyaji wa mapato tuliouchagua, tuliuchagua wenyewe bila
kushurutishwa na yeyote na tunadhani ndiyo mfumo unaotufaa kwa sasa hadi
hapo ligi yetu itakapokuwa na nguvu maana kwa sasa inaruhusiwa klabu
kupata fedha mwanzoni kulingana na hali halisi ya vilabu vyetu.
Tunawashauri wenzetu wa Yanga waanze kuamini kwenye kitu kinachoitwa
Uwajibikaji wa Pamoja (Collective Responsibility). Mambo yanayoamuliwa
kwenye vikao hayapaswi kupingwa nje ya vikao. Kama hoja ililetwa kwenye vikao na ikazidiwa nguvu na hoja nyingine,
hakuna sababu ya kuikataa kwa sababu tu hukubaliani nayo. Mfumo wa
kidemokrasia una kanuni moja kuu; Wengi Wape.
Imetolewa na
Vilabu 13 vya Ligi Kuu ya Tanzania
Vilabu 13 vya Ligi Kuu ya Tanzania
Simba SC, Azam FC, Ashanti United, JKT Ruvu, Ruvu Shooting Stars, Mgambo JKT, JKT Oljoro, Rhino Rangers, Mbeya City, Tanzania Prisons, Mtibwa Sugar, Coastal Union na Kagera Sugar.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog