KOCHA Ernie Brandts hana chake tena Yanga na ndani ya siku mbili, uongozi wa klabu hiyo utatangaza kumtimua.
Taarifa za uhakika ambazo blog hii imezipata kutoka ndani ya Yanga, zimeeleza Brandts ameshafukuzwa kazi.
“Kweli Brandts ameonekana hafai na wakubwa walikaa jana kikao mara tu baada ya mechi ya Simba na Yanga, wamefikia hatua ya kumuachisha kazi.
“Mimi ninavyojua tayari mawasiliano na makocha kadhaa yameanza na Brandts atapewa muda kidogo tu ili akusanye virago vyake na kurejea kwao Uholanzi,” kilieleza chanzo cha uhakika.
Lakini viongozi wa Yanga walikuwa wagumu kulizungumzia suala hilo, ingawa mtu mwingine wa karibu na uongozi wa Yanga, alisema huenda leo Yanga wakatangaza.
“Wanaweza kutangaza kesho (leo), nimeelezwa kuwa wamefikia uamuzi huo na kuna bosi mmoja atatangaza leo au kesho,” alisema na kuongeza: “Kama mtaandika wanaweza wasitangaze.”
Brandts amejikuta katika wakati mgumu baada ya kikosi chake kulambwa na Simba kwa mabao 3-1 katika mechi ya Nani Mtani Jembe iliyopigwa juzi jijini Dar.
Inaelezwa baada ya mechi hiyo, kocha huyo aliyeipa Yanga ubingwa msimu uliopita, alishindwa kuwaridhisha mabosi wake baada ya kuulizwa sababu za kufungwa.
Mbali na Brandts, inadaiwa kuwa uongozi wa timu hiyo una mpango wa kutimua benchi zima la timu hiyo, akiwemo Kocha Msaidizi, Fred Felix Minziro.
Kocha wa sasa wa Mbeya City, Juma Mwambusi, ndiye anapewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi ya Minziro kwenye kikosi hicho cha Jangwani.
Yanga inatarajia kwenda kuweka kambi na inaelezwa zitakuwa nchi kati ya Hispania, Uturuki au Ureno na taarifa zinasema kuwa inataka kwenda na benchi zima la ufundi.
Na katika tofuti ya Yanga wameeleza muda huu kuwa kocha huyo amepewa notisi ya siku thelathini ya kusitisha mkataba wake kuanzia tarehe 22 mwezi huu..
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog