Facebook Comments Box

Saturday, September 21, 2013

MBEYA CITY YAENDELEA KUTESA VIGOGO WA LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA


Mshambuliaji wa Simba SC, Amisi Tambwe akimtoka beki wa Mbeya City Anthony Matogolo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo. Timu hizo zimetoka sare ya mabao 2-2.  
 
Timu ya Mbeya City imetoka sare kama kawaida yake katika uwanja wa Taifa leo ilipokuwa inacheza na Timu mwenyeji wa uwanja huo Simba SC ya Msimbazi Jijini Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo jioni. 

Simba ambayo hata baada ya sare hiyo inaendelea kuwa kileleni mwa ligi hiyo baada ya kufikisha alama 11 kibindoni huku Mbeya City ikifikisha alama 7 baada ya michezo mitano iliyocheza.

Simba ndiyo ilikuwa yakwanza kupata bao katika dakika ya 29 kupitia kwa mshambuliaji wake hatari kutoka Burundi Amis Tambwe aliyepokea pasi kutoka kwa Haruna Chanongo na baadae kuongeza bao lingine katika dakika ya 33 kwa shuti kali baada ya pasi kutoka kwa Betram Mombeki, Tambwe aliwadhihirishia mashabiki wa timu hiyo na timu pinzani kuwa hakubahatisha kufunga Hat Trick katika mechi iyopita dhidi ya Mgambo Shooting ya Tanga iliyochapwa bao 6 kwa Ubuyu na Simba.

Mbeya City, timu ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya inayofundishwa na Juma Mwambusi ilijipatia bao katika kila kipindi ambapo bao lake la kwanza lilifungwa na Paul Nonga dakika ya 37 kwa shuti kali ambalo lilimshinda kipa wa Simba Abbel Dhaira, wakati la kusawazisha lilifungwa na Richard Peter dakika ya 69 akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Mwigane Yeya.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga, Charles Mbilinyi na Juma Mwita wa Mwanza, Simba SC inafundishwa na mshambuliaji wake wa zamani, Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’,

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Abbel Dhaira, William Lucian ‘Gallas’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Kaze Gilbert/Hassan Hatibu dk66, Joseph Owino, Jonas Mkude, Twaha Ibrahim/Ramadhani Chombo ‘Redondo’ dk50, Amri Kiemba/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk79, Betram Mombeki, Amisi Tambwe na Haroun Chanongo. 

Mbeya City; David Burhan, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Deogratius Julius, Antony Matogolo, Yohana Morris, Mwigane Yeya/Richard Peter dk59, Steven Mazanda, Paul Nonga, Deus Kaseke na Yussuf Willson.   

Katika mechi nyingine, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wenyeji Mgambo Shooting Stars wametoka sare ya 1-1 na Rhino Rangers ya Tabora, Prisons imetoka 1-1 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya, wakati Kagera Sugar imeshinda 3-0 dhidi ya Ashanti United ya Dar es Salaam Uwanja wa Kaitaba.

Ligi hiyo itakamilisha mzunguko wake wa tano kesho kwa mechi tatu ambazo ni Azam na Yanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku JKT Ruvu ikikwaruzana na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Azam Complex na mechi kati ya Ruvu Shooting inayokamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi itakuwa mgeni wa Coastal Union katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU