Kituo cha reli cha Kigoma |
Mji wa Ujiji ulioko Magharibi
mwa Tanzania una historia ndefu miongoni mwa miji ya kale ya Afrika
Mashariki na Kati ukihusishwa na biashara ya watumwa kutoka Burundi,
Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Ni katika eneo hilo la Ujiji ndiko mvumbuzi wa
kimataifa, Dr David Livingstone, alipofikia akiwa katika safari zake
zilizomtoa pwani ya Afrika mashariki hadi Kongo. Kwa sasa kuna
makumbusho maalum kwa heshima yake na kumbu kumbu ya vizazi vijavyo.
Lakini nusu karne baada ya uhuru wa
Tanzania, umaarufu wa mji huo mkongwe umeporomoka na hali ya maisha ya
watu wake imeendelea kuwa duni. Mwandishi wa BBC Baruan Muhuza
ametembelea mji huo na kujionea hali ilivyo.
Kwenye kituo cha makumbusho ya Dr David
Livingstone katika eneo la Mnazi Mmoja-Kabondo Ujiji ni eneo ambalo kuna
majengo mazuri yenye vyumba kadhaa vilivyobeba alama za ujio wa
Mvumbuzi huyo aliyechangia kukomeshwa kwa biashara ya utumwa, lakini pia
kumbukumbu za asili za vitu na watu wa mji huo.
Kufifia kwa umaarufu wa eneo kongwe la Ujiji
kulichangiwa na sababu nyingi, ikiwemo kuanzishwa kwa mji mpya wa
Kigoma. Kurejea kwa Ndiyunze Msherwampamba aliyekuwa kiongozi wa watu wa
kabila la wagoma kutoka Kongo kuliibua jina la mji mpya Kigoma.
Alhaj Mikdad bin Ibrahim Tawfiq Malilo mwenye
miaka 79 mkaazi maarufu wa Ujiji, ameiambia BBC kuwa Msherwampamba
alipokelewa pamoja na wafuasi wa kabila lake na wakapewa eneo la
kujitawala ambalo wakati huo lilikuwa likiitwa Rusambo , na sasa ndilo
linaloitwa Kigoma.
Mji wa ujiji unakumbwa na umaskini si haba |
„Walipompokea Msherwampamba wakapewa kanchi,
eneo lenyewe ni sehemu hivi sasa wanasema ikulu ndogo zamani tulikuwa
tunasema Kaizahofu, eneo lote lile kabla ya hapo lilikuwa linaitwa
Rusambo.
Sasa wenyeji warundi ndiyo wanajiita wajiji
wakawa wanakwenda kuwatembelea wanasema 'tugende kubagoma,' likaendelea
likabadilika ndiyo ikawa Kigoma basi ndiyo kitovu cha mahala kuitwa
Kigoma asili Rusambo”
Kwa miaka mingi nguvu za kiuchumi za wakazi wa
mji huo imekuwa ikitegemea Ziwa Tanganyika kwa uvuvi na usafiri wa
kwenda na kutoka maeneo mbali mbali ya mwambao wa ziwa hilo zikiwemo
nchi jirani za Burundi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Pamoja na kupoteza uimara wake, Mji wa Ujiji na
Kigoma kwa ujumla umeibuka upya katika miaka ya karibuni kwa kutoa watu
waliojipatia umaarufu mkubwa katika eneo lote la Afrika Mashariki na
kati ikiwa ni pamoja na wasanii wa muziki wakiwemo Naseeb Abdul
anaejulikana zaidi kama Diamond, Wanasoka wastaafu Kitwana Manara,
Kassim Manara, Edibily Lunyamila na hata nahodha wa sasa wa Timu ya
Taifa ya Tanzania Juma Kaseja .
Tangu enzi za Ukoloni watu kutoka maeneo
mbalimbali ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Burundi, Rwanda na
Zambia waliingia mji wa Ujiji hasa kipindi cha utawala wa biashara ya
watumwa.
CHANZO: BBC SWAHILI
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog