Facebook Comments Box

Friday, September 20, 2013

YANGA YADAIWA KARIBIA NUSU BILIONI


Yanga inayokabiliwa na kazi nzito ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara inapaswa kutafuta Sh. 428.5 milioni (karibu nusu bilioni) kwa ajili ya kuwalipa wachezaji wanne, viongozi wawili na kumpa fedha mmoja akailipe fidia klabu ya Simba. (HM)

Wachezaji wanaoidai Yanga ni aliyekuwa nahodha wa siku nyingi wa klabu hiyo, Shadrack Nsajigwa na beki Stephano Mwasyika. Hao wanadai malimbikizo ya fedha za usajili zinazofikia Sh. 15.5 milioni.

Nsajigwa peke yake anadai shilingi milioni tisa (9) wakati Mwasyika anadai shilingi milioni 6.5.

Utaratibu wa klabu hiyo ni kwamba wachezaji wapya wanaposajiliwa hupewa fedha taslimu wakati wa zamani hupewa wanapoongeza mikataba yao ila wengi wao hawalipwi mara moja.

Ndiyo maana leo hii Nsajigwa na Mwasyika wanaidai Yanga malimbikizo ya fedha walizopaswa kulipwa walipokuwa bado wanaichezea klabu hiyo.

"Bado Yanga naidai na hakuna lolote nililoambiwa kuhusu malipo yangu, kama wangekuwa wamenilipa nadhani umma wa Tanzania ungejua," alisema Nsajigwa ambaye ni kocha mkuu wa timu ya soka ya Lipuli ya Iringa inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Wachezaji wengine wanaoidai Yanga ni Wisdom Ndlovu raia wa Malawi na Steven Malashi ambao wanadai Sh. 106 milioni kwa kukatishiwa mikataba yao 16 Julai 2010 miezi minne tu tangu watie saini kuendelea kuichezea timu hiyo ya Mtaa wa Jangwani 18 Machi 2010.

Baada ya kudai bila mafanikio stahili zao Ndlovu na Malashi, kupitia kwa wakili Godwin Muganyizi, waliamua kufungua kesi katika Mahakama Kuu kitengo cha Kazi ambako walishinda.
Hivi karibuni Yanga walikwenda Mahakama ya Rufaa kuomba kesi hiyo ipitiwe upya lakini ilitupwa kwa maelezo ilishamalizika hivyo walipe deni hilo.

Ndlovu anadai Sh. 57 milioni na Malashi Sh. 37 milioni. Kabla ya kufungua kesi hiyo mahakamani, wachezaji hao walipeleka malalamiko yao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambalo baada ya kupitia vielelezo liliamuru Yanga iwalipe wachezaji hao. Fedha nyingine wanazodai ni gharama za kesi yao.

"Tuliishinda Yanga mahakamani, wakaamriwa watulipe fedha zetu, wakaona si haki kutulipa wakaenda kukata rufaa nako wamegonga mwamba. Lakini bado wanatusumbua kutulipa," anasema Malashi ambaye ni kipa wa zamani wa klabu hiyo.

"Sisi tunafuata sheria na sasa tupo Mahakama ya Rufaa na wakili wetu kuomba ikazie hukumu ili tulipwe haki yetu."

Kundi lingine la watu wanaoidai Yanga ni waliokuwa watendaji wake; aliyekuwa katibu mkuu wake Celestine Mwesigwa na Louis Sendeu aliyekuwa ofisa habari .

Septemba mwaka jana, watendaji hao waliondolewa katika ajira zao kwa kile kilichoelezwa kuwa uongozi haukuridhika na utendaji wao.

Mwesigwa na Sendeu waliomba bila mafanikio walipwe na Yanga fidia ya Sh. 262 milioni ambapo kati ya hizo, Sendeu anadai Sh. 79 milioni na Mwesigwa anadai Sh. 183 milioni.

Watendaji hao walifikisha suala hilo katika Baraza la Kazi ambao walishinda madai yao na hivyo Yanga imeamriwa kuwalipa kiasi hicho cha fedha.

"Nashangaa Yanga inajipanga kuajiri watu wengine wakati sisi waliotufukuza bado tunawadai. Hiki si kitendo cha kiungwana, wao walipaswa kumalizana nasi kwanza halafu wakaendelea na ustaarabu mwingine na watu wengine," anasema Mwesigwa.

Mbali ya madeni hayo, Yanga inalazimika kubeba deni la usajili wa mshambuliaji wake Mrisho Ngassa anayedaiwa na klabu ya Simba Sh. 45 milioni yaani Sh. 30 milioni alizochukua Simba na fidia ya Sh. 15 milioni.

Ngassa aliyekuwa amesajiliwa na Azam, aliichezea Simba kwa mkopo msimu uliopita na aliingia makubaliano ya kuingia mkataba kamili wa miaka miwili wa kuichezea timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi msimu huu. Akapewa Sh. 30 milioni lakini ulipofika muda wa usajili akatia saini Yanga.

TFF ilimwidhinsha kuichezea Yanga kwa vile alikamilisha taratibu zote, lakini kwa vile nyaraka zinaonyesha alimwaga wino akachukua fedha Simba, shirikisho hilo limemfungia mechi sita na hataruhusiwa kukipiga Yanga hadi alipe deni hilo. Habari zimesema Yanga watalipa.

Akizungumzia madeni hayo, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, anasema, "Tunakubali deni la akina Nsajigwa ambalo lazima tulipe, pia hao akina Malashi bado tunafuatilia mambo ya kisheria ili tuweze kujua nini tunafanya."

Kuhusu madeni mengine anasema, "Hata hayo madeni ya watu wengine (akimaanisha akina Mwesigwa) nayo tunayajua na kuna vitu tunafuatilia ili tuweze kujua tufanyacho, lakini kuhusu Ngassa sina jibu la kukupa maana ni kitu kinachoweza kujadiliwa na kamati ya utendaji."

 Chanzo: shaffihdauda


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU