Facebook Comments Box

Thursday, August 22, 2013

KITUO CHA MABASI YA KUTOKA DAR KWENDA MIKOANI KUJENGWA MBEZI LUIS NA BASIHAYA: JIJI







TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:

Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itajenga vituo vya mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani katika maeneo ya Mbezi Luis na Boko-Basihaya. Ujenzi wa vituo hivyo ni utekelezaji wa mipango ya Jiji ya kuimarisha huduma za usafiri Dar es Salaam.

Kituo cha Mbezi Luis kitahudumia wasafiri wa Kanda ya Kati na Nyanda za Juu wakati Kituo cha Boko Basihaya kitatoa huduma kwa wasafiri wa Kanda ya Kaskazini. Kwa Kanda ya Kusini Halmashauri ya Jiji itajenga Kituo cha Mabasi Kongowe.

Kituo kitakachoanza kujengwa ni Mbezi Luis ambacho kitajengwa sambamba na Boko Basihaya. Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo kimepangwa kutoa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka kwa wasafiri wote watakaokuwa wakitumia vituo hivyo vya mabasi yaendayo mikoani. Ujenzi wa vituo vya Mbezi Luis na
 Boko Basihaya, kutokana na upembuzi yakinifu wa awali, unakadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 40 kwa kila kituo.

Ujenzi wa vituo hivyo unahitaji upembuzi yakinifu wa kina kwa lengo la kupata gharama halisi za utekelezaji wake, kubaini vyanzo vya fedha na kuangalia uwezekano wa kuzishirikisha taasisi mbalimbali za fedha na wawekezaji wanaoonyesha nia ya kushirikiana na Halmashauri ya Jiji katika ujenzi wa vituo hivyo ambavyo vitakapokamilika vitakuwa pia ni chanzo cha ajira kwa wananchi.

Katika kipindi hiki cha maandalizi ya ujenzi wa vituo hivyo, bado Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT) kitaendelea kutoa huduma kwa wasafiri waendao mikoani na nchi za jirani. Halmashauri ya Jiji inapenda wananchi wafahamu kwamba UBT,

 kama ilivyopangwa na Serikali, itakuwa ni kituo kitakachotoa huduma ya usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka(Dar Rapid Transit-DART) baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu yake. Pamoja na hilo Halmashauri ya Jiji pia itajenga “shopping malls” na hoteli katika kituo hicho cha UBT

Kukamilika kwa ujenzi wa vituo hivyo vya mabasi ni mafanikio makubwa katika jitihada za serikali za kuimarisha huduma za usafiri katika Jiji la Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo katika sekta hii, wananchi na taasisi mbalimbali wanategemewa kuendelea kutoa mapendekezo yao ya kuimarisha huduma za usafiri Dar es Salaam.

Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU