KOCHA Msaidizi wa timu ya Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amedai
kuondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kulitokana na maandalizi
hafifu na wachezaji hawapaswi kutupiwa lawama.
Mabingwa hao wa Tanzania, walijikuta wakitolewa kwenye michuano hiyo
na Recreativo de Libolo ya Angola kwa jumla ya mabao 5-0. Awali
ilifungwa bao 1-0 nyumbani kabla ya kutandikwa 4-0 ugenini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Julio alisema timu yake
haikupata maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kushiriki michuano ya
kimataifa, tofauti na wenzao ambao waliipa umuhimu mkubwa michuano hiyo.
Alisema, hali hiyo ndiyo ilisababisha kikosi chake kuondolewa katika
raundi ya kwanza tu, kitu ambacho ni cha kusikitisha na kutia uchungu
kwa timu kubwa kama Simba.
Julio aliongeza kuwa kutokana na matokeo hayo, hakuna haja ya
kuwatupia lawama wachezaji, kwani walijitahidi kutimiza majukumu yao kwa
kucheza kwa kiwango kinachostahili, lakini walizidiwa na wapinzani wao.
Alisema matokeo yameshakuwa hayo, hivyo kwa sasa hawana budi kuachana
nayo na kuelekeza nguvu zao Ligi Kuu Bara ili kuweza kujiweka katika
mazingira mazuri zaidi.
“Tutahakikisha tunafanya maandalizi ya hali ya juu ili tuweze kushinda
michezo yetu iliyobaki na hivyo kupata nafasi nzuri itakayotuwezesha
kushiriki michuano ya kimataifa mwakani,” alisema.
Simba kwa sasa inashika nafasi ya tatu ya ligi hiyo ikiwa na pointi
31 huku Azam FC ikiwa ya pili na pointi 36 na Yanga inayoshikilia
usukani ina pointi 42.
Katika hatua nyingine, uongozi wa Simba jana ulikuwa na kikao na
wachezaji kwa ajili ya kujadili mustakabali wa timu yao, ambayo imekuwa
na mwenendo mbaya katika mechi zake za hivi karibuni, zikiwemo za
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Habari zilizopatikana jana jioni zinaeleza kwamba, Kamati ya Utendaji
ya Simba, pamoja na viongozi wa Kamati ya Ufundi, walikutana na
wachezaji baada ya mazoezi ya jioni na kujadili kiini cha kufanya kwao
vibaya.
Kiongozi mmoja wa Simba, aliliambia Tanzania Daima kwamba, lengo la
kikao hicho ni kubaini tatizo ili kulitatua na hatimaye kuondokana na
mwenendo mbaya.
Hivi karibuni, kumekuwepo na ‘sintofahamu’ ndani ya klabu hiyo, ambapo
kuna taarifa za mgomo wa chini chini unaofanywa na wachezaji kwa madai
ya kubaguliwa na baadhi ya viongozi, huku pia wakilalamikia benchi la
ufundi.