Facebook Comments Box

Thursday, February 21, 2013

MUHIMBILI WAKANUSHA KUVAMIA OFISI YA MKURUGENZI


 
Gazeti la Mwananchi ISSN-0856-7573 Na.4621 la tarehe 20 Februari 2013
lilichapisha habari katika ukurasa wake wa pili iliyokuwa na kichwa cha habari “Muhimbili Wavamia Ofisi ya Mkurugenzi”. Awali ya yote tunapenda ieleweke kuwa  wafanyakazi hawakuvamia ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kwa kuwa kulikuwa na mawasiliano na wafanyakazi waliotaka kumuona kupitia kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi TUGHE Tawi la Muhimbili na alikuwa amekubaliana na ombi la kukutana nao.

Pili, tunapenda kutoa ufafanuzi kwamba wafanyakazi hawa hawakuvamia kama gazeti linavyodai. Aidha, tunakanusha sababu zilizotolewa na Gazeti la Mwananchi kwamba wafanyakazi walivamia ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wakishinikiza kulipwa mishahara ambayo kwa mujibu wa taarifa za gazeti hili ni kuwa haijalipwa kwa muda wa miezi mitatu tangu mwaka jana mwezi wa 11.

Tunapenda kuueleza umma kwamba taarifa hizi ni upotoshaji wa hali halisi ya ulipaji wa mishahara kwa wafanyakazi na taarifa hizi hazijatafitiwa kutoka mamlaka za Hospitali kuthibisha ukweli wake. Habari hizi siyo za kweli kwa kuwa Hospitali haijawahi kukosa mishahara ya wafanyakazi, hususan katika kipindi kinachodaiwa wafanyakazi hawakupata mishahara. Tumebaini pia gazeti hili limetumia majina ya watu likidai ni wafanyakazi wa Hospitali hii wakati siyo kweli kwa nia ya kuufanya umma uamini kwamba habari hizi ni halali na za kweli wakati ni kinyume chake. Watu wenye majina Anna Msigwa alitajwa kama Muuguzi na Anthony Semukasi siyo miongoni mwa wafanyakazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili hivyo ni majina bandia. Kwa hiyo habari hii ni ya uzushi usio na ukweli wowote. Ni mtu mmoja tu aliyetajwa kwa jina la Ndg. Faustine Fidelis, ndiye tunamtambua kuwa mfanyakazi katika Hospitali hii na Katibu wa tawi la TUGHE Muhimbili.

Tunapenda umma uelewe kwamba kama kuna mfanyakazi hapati mshahara basi atakuwa ni mfanyakazi mpya ambaye taratibu za kupata mshahara wake kutoka serikalini zinafanyika. Wafanyakazi wa aina hii ni wachache na tunaamini kwamba hawakulengwa na taarifa hizi ambazo zilitaka umma uamini kwamba wafanyakazi wote wa Hospitali ya Taifa Muhimbili hawajapata mishahara tangu Novemba 2012 hadi sasa.

Tunapenda kutoa ufafanuzi kwamba wafanyakazi walienda kwenye ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kudai motisha iliyotokana na mapato kupitia huduma iliyotolewa kwa wagonjwa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Taifa (NHIF) ambayo iliahidiwa kulipwa na Uongozi wa Hospitali. Malipo haya siyo sehemu ya mishahara bali ni motisha kwa wafanyakazi yenye lengo la kuongeza tija. Malipo haya yalichelewa kulipwa kwa baadhi ya wafanyakazi lakini yalikuwa katika hatua za mwisho za maandalizi ya kulipwa. Wafanyakazi walielezwa hili na walielewa na kuendelea na kazi.

Hospitali ya Taifa Muhimbili iko tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo vya habari kuviwezesha kutoa taarifa sahihi kwa umma. Tunawasihi waandishi wa habari kupata ufafanuzi wa taarifa zozote wanazopata kuhusu Hospitali kabla ya kuandika na kupotosha umma.


Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano
Februari 21, 2013



Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU