Facebook Comments Box

Monday, February 18, 2013

MPASUKO WAIKUMBA UVCCM

Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Sadifa Juma Khamis

 Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM), limeingia katika mpasuko mkubwa baada ya baadhi ya wajumbe kukusudia kutoa hoja ya  kumwondoa Mwenyekiti wa umoja huo, Sadifa Juma Khamis, kwa madai ya kukiuka  kanuni na hotuba  ya ufunguzi wa kikao cha baraza hilo iliyoonyesha kuwadhalilisha.
 
Chanzo kutoka ndani ya kikao hicho kilichotarajiwa kumalizika jana katika ukumbi wa White House, mjini Dodoma, kilisema hali ya kutokuelewana ilitokea mara baada ya Sadifa kutoa hotuba hiyo juzi mchana.
 
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kulikuwa na hali ya kutoelewana ndani ya kikao hicho huku wasemaji wa umoja huo wakikatizwa mara kwa mara na kelele za kuzomeana.
 
“Baadhi ya vijana walikaa katika makundi na kuazimia kumuondoa mwenyekiti kwa kitendo chake cha kuwadhalilisha tena mbele ya waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa kikao hicho,” kilisema chanzo hicho. 
 
Pia vijana hao walikasirishwa na kitendo cha Mwenyekiti wa Taifa  Sadifa kumtimua mmoja wa waliokuwa wagombea wa nafasi ya umakamu mwenyekiti, Paul Makonda,  kwa madai kuwa alikaririwa na vyombo vya habari  mara baada ya uteuzi huo akitaka kupewa nafasi ya kufikiriwa. 
 
Aidha, wajumbe wa Baraza hilo walikerwa na kitendo cha Sadifa kumwachisha kazi mmoja wa watumishi wa umoja huo kutokea Visiwani Zanzibar aliyejulikana kwa jina moja la Jamal. 
Mvutano huo uliodumu kwa zaidi ya saa mbili na kutawaliwa na vikao vya siri, ulifanya kuchelewa kuanza kwa kikao hicho kwani badala ya kuanza saa 5:00 asubuhi kilianza saa 7:00 mchana.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, mjumbe kutoka mkoani Mbeya, David Mwakiposya, alisema hotuba aliyotoa mwenyekiti wao ni mbovu na haifai. 
 
“Kwa mujibu wa kanuni za Umoja wa Vijana wa CCM ya mwaka 2008, Baraza Kuu ndilo linathibitisha uteuzi wa wajumbe wa Baraza, lakini cha kusikitisha aliwafukuza wajumbe wawili ambao  wakati wa mkutano mkuu yeye aliwateua na tena aliwaita mwenyewe waje katika mkutano huu,” alisema na kuongeza kuwa:
 
“Ni kitendo kisichofaa kabisa katika nchi yetu wakati tungali tunatengeneza demokrasia. Bahati nzuri alilizungumza hili mbele yenu, hapa mmeniuliza maoni yangu kuhusiana na hotuba hii maoni yangu ndiyo hayo siiungi mkono hotuba yake.” 
 
Mwakiposya alisema Sadifa aliongea kuhusiana na suala la mapenzi ndani ya baraza hilo kwamba limekuwa likisababisha kuvujishwa kwa siri za vikao, jambo ambalo alisema halina ukweli wowote. 
 
Alisema mwenyekiti huyo katika hotuba yake aliwatuhumu meza kuu (viongozi wa juu wa umoja huo ), kuwa wamekuwa wakijihusisha na mapenzi na hivyo kazi hazifanyiki jambo ambalo halina ukweli.
 
“Mimi kama mjumbe wa Baraza Kuu nimesikitishwa, nimeguswa, sifurahishwi na hayo yaliyojitokeza katika hotuba hiyo, “ alisema Mwakiposya huku akisisitiza kuwa hayo ni maoni yake binafsi.
 
Kuhusu suala Mwenyekiti huyo kutamka wakati akiwania nafasi hiyo aliingizwa katika makundi yanayojiandaa kwa ajili ya urais, Mwakiposya alisema: “Hiyo ndiyo tabu ya kuwa na kiongozi anayeamini katika hili huku anatenda hivi.” 
 
“Alipowateua hawa watu aliowafukuza tuliamini kuwa haegemei katika makundi, lakini katika utekelezaji hakuna….Mimi sifahamu katika UVCCM kama kuna makundi, lakini baada ya kusema hilo nikajua kuwa kumbe kuna makundi,” alisema. 
 
Na kwa upande wa siri kuvuja, alisema yeye ni mmoja wa watu ambao anaamini kuwa kiongozi yoyote anayevujisha siri za vikao hafai katika uongozi. 
 
Hata hivyo, alisema hajawahi kusikia kuhusiana na kuvujishwa kwa siri za vikao na viongozi licha ya kuwafahamu viongozi mbalimbali wa umoja huo. 
 
“Tunaonyana ndani ya vikao halali hatuwezi kuzungumza  kwa waandishi wa habari mambo ambayo tunayaona kuwa hayaendi sawa tutayazungumza ndani ya vikao vyetu,” alisema alipoulizwa kuhusiana na kauli kuwa kuna baadhi ya makundi yalionekana kukaa kabla ya kuanza kwa  kikao cha siku ya jana. 
 
Kuhusu madai ya kutaka kumng’oa mwenyekiti wao, Mwakiposya alisema hajasikia kitu kama hicho na kwamba kama kinakuwapo umoja huo unataratibu za kikanuni za kufuata ili kumng’oa mwenyekiti. 
 
“Kanuni ya mwaka 2008 inasema kama ikithibitika kiongozi yeyote amekiuka kanuni Baraza linaweza kutoa pendekezo katika kikao cha juu kumsimamisha, lakini kama sisi tunataka kumsimamisha kama vijana hatujafikia huko bado,” alisema.
 
Alisema iwapo ikidhibitika kuwa hawawezi kwenda sambamba na kiongozi yeyote yule basi watafukuzana. 
 
Alipoulizwa kama mwenyekiti huyo amekiuka kanuni yoyote, alisema amekiuka kanuni ya kufukuza watumishi wa umoja huo kwa kumfukuza mmoja wa watumishi kutoka Zanzibar. 
Alifafanua kwa mujibu wa kanuni, kikao chenye mamlaka ya kumfukuza mtumishi ni Baraza Kuu la Umoja wa Vijana. 
 
Kwa upande wake, Mjumbe Halmashauri Kuu ya CCM (jina tunasitiri), alisema alisikia tetesi kuhusiana na kung’olewa kwa mwenyekiti, lakini UVCCM ni jumuiya ya muda mrefu ambayo ina taratibu zake za kumuondoa kiongozi. 
 
“Usiwaone hivi, hawa ni viongozi waliokomaa, hakuna ambalo linaweza kuharibika ila inachofahamu hakuna mtafaruku na kama ulikuwapo umeisha,” alisema na kuongeza wajumbe hao wako salama na wanaendelea vizuri. 
 
Alisisitiza kuwa hakuna mkanganyiko utakaotokea mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho cha siku mbili ambacho kitafuatiwa na semina na kwamba hakuna kitu kipya kwa kuwa kila inapokaa jumuiya hiyo kumekuwa na harakati.
 
Katika tukio jingine waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari,  walijikuta wakikalishwa na Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Mboni Mhita, kwa zaidi ya saa tatu katika ukumbi wa mikutano wa sektarieti ya chama hicho. 
 
Mhita aliwaita kwenye chumba hicho, kwa madhumuni ya kuwaeleza kile kilichotokea katika kikao hicho kwa siku mbili za juzi na jana. 
 
“Tukubaliane nitazungumza nitazungumzia agenda za jana (juzi) na kinachoendelea leo (jana), tu, lakini sitazungumzia yatokanayo…ama vinginevyo muendelee kumsubiri Katibu Mkuu aje aongee nanyi,” alisema. 
 
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kuletewa faili aliloliitisha, aliondoka na kuwataka waandishi wa habari kuendelea kusubiri kwa sababu alikuwa akimsubiri mjumbe wa kitengo fulani aje azungumzie mambo ambayo hata hivyo hakuyafafanua.
 
Akijibu madai hayo, Sadifa ambaye pia ni mbunge wa Donge, alisema walipanga kuanza kikao saa 7:00 mchana na kwamba kwa kuwa wajumbe wanafahamiana kukaa katika makundi si kosa.
 
“Maana Katiba yenyewe inaruhusu watu kukaa vikundi ili mradi wawe hawavunji taratibu, sheria na kanuni…baada ya muda kufika si waliingia kwenye kikao kama jana (juzi) kikao kilikuwa kizuri tofauti na vyombo vya habari mlivyokuwa mkisema huko nje,”alisema.
 
Kuhusu hoja ya kumng’oa kwa madai ya kukiuka kanuni, Sadifa alihoji  “ Kanuni namba ngapi?.. Jamal hajafukuzwa sasa wewe utuambie aliyemfukuza ni nani? Jamal ni mjumbe halali wa hiki kikao kama angekuja lakini kwa bahati nzuri ama mbaya, Jamal mwenyewe alinifuata baada ya majina kurudi na kuniambia kuwa amechoka anataka apumzike.”
 
Alisema  kwasababu Jamal anafanya kazi mbili Zeco visiwani  Zanzibar na katika Chama kama Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Vijana, alimuomba apumzike ili aendelee na utumishi wake serikalini. 
 
 Kuhusu hotuba yake kuwadhalilisha, Sadifa aligeuka mbogo: “Nani, wajumbe? Tutajie? ama wewe? Eh, tuthibitishie.”
 
Hata hivyo, alikanusha kuwa hakuna mjumbe aliyedhalilishwa wala aliyelalamikia hotuba yake na kuwalaumu waandishi wa habari kuwa wana matatizo ya kuwagombanisha watu.
 Kuhusu Makonda, alisema kanuni ya Umoja wa Vijana inasema yeye anateua mtu  ambaye anatakiwa kuthibitishwa ndani ya kikao cha Baraza Kuu la umoja huo na kanuni hizo haziruhusu kupeleka kila kitu katika vyombo vya habari.
 
 Alisema baada ya kuona magazeti yamemnukuu Makonda akisema kuwa hawezi kukubali uteuzi huo ili asije kuonekana kuwa amehongwa, alifahamu hizo ni hasira za uchaguzi.
 
 “Kwa hiyo mimi nilimpigia simu mmoja mmoja, Makonda  Msarika, jamani nimeona statement (taarifa), hizi katika magazeti haya, hebu niambieni uteuzi huu mmeukubali ama mmeukataa? Wao wenyewe hakuna aliyekuja kunipa kauli yake kama wamekubali uteuzi,” alisema.
 
 Alimtolea mfano Makonda kuwa amemwita wakutane lakini alikataa,” unajua siasa lazima ukae na mwenzako mzungumze mbadilishane mawazo ndiyo siasa, jana usiku (juzi ), baada ya kumaliza kikao, nilimpigia tukutane…tukae tuvunje migogoro iliyokuwapo, lakini hakuonekana.”
 
Alisema baadhi ya wajumbe walipoona ujio wa Makonda, walitaka kufanya vurugu wakihoji juu ya ujio wake.
 
“Kwa sababu pia baadhi ya wajumbe kwa kuona Paul Makonda, pale walitaka kuanzisha vurugu, kwa busara tukatuliza sijui tumeelewana vizuri?...Alitakiwa baada ya kusomwa kanuni na kujulikana wajumbe, basi wajumbe wabaki kwa wakati ule si mjumbe kwa maana hakuthibitishwa na Baraza Kuu kwa hiyo alitakiwa kwanza atoke ili Baraza Kuu liridhie ama lisiporidhia sawa,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU