Facebook Comments Box

Sunday, December 30, 2012

PROF LIPUMBA: MADAI YA WANANCHI WA MTWARA YASIPUUZWE


Tarehe 27 Desemba maelfu ya wananchi wa Mtwara waliandamana kudai gesi ya Mnazi Bay itumiwe kuendeleza viwanda katika mkoa wa Mtwara kabla ha

ijasafirishwa kwenda kutumiwa maeneo mengine ya nchi. Kwa muda mrefu CUF Chama cha wananchi kimekuwa kikisisitiza kuwa na sera zitakazohakikisha kuwa maliasili na rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote kwa ujumla na hususani wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo maliasili hiyo imegunduliwa.

Katika nchi nyingi utajiri mkubwa wa gesi na mafuta umeleta balaa badala ya kuleta neema. Nchini Nigeria katika delta ya mto Niger ambako ndipo mafuta yanachimbwa kuna ghasia kubwa za kisiasa kwa madai kuwa wananchi wa eneo hilo hawanufaiki na rasilimali yao.

Wananchi wa mikoa ya kusini wana sababu za msingi za kulalamika kuwa  kwa muda wa miaka 51 ya uhuru wa
Tanzania Bara bado hawajatendewa haki. Serikali ya mkoloni wa Kiingereza ilijenga reli kuunganisha Nachingwea na Mtwara ilipoanzisha mradi wa kilimo cha karanga. Mradi huu haukufanukiwa. Badala ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo na kuendeleza uzalishaji wa mazao mengine kama vile korosho, ufuta, alizeti, kunde na mbaazi, Serikali ya TANU baada ya kupata uhuru ikaamua kun’goa reli ya Nachingwea – Mtwara na kuihamishia Kilosa Mikumi.

Zambia ilipokuwa inakabiliwa na tatizo la kusafirisha mizigo yake isipitie Rhodesia iliyokuwa inatawaliwa na wazungu wachache, walipendekeza kwa serikali ya Tanzania kujenga reli kwenda Mtwara kwani bandari ya Mtwara ni nzuri, ina kina kirefu na haina msongamano. Shaba ya Zambia ingepakuliwa kwa haraka na kusafirishwa kwenda nchi za nje. Vile vile mizigo inayoagizwa kutoka nje ingepakuliwa haraka na kusafirishwa kwenda Zambia. Serikali ya Tanzania haikuafiki pendekezo la Zambia na ikasisitiza reli ya TAZARA iende Dar es Salaam.

Gesi ya Songosongo ilikuwa itumiwe kama malighafi katika kiwanda cha mbolea cha Kilwa Ammonium Company. Prof Cleophace Migiro alienda kusomea PhD ya Chemical engineering kwa maandalizi ya kuja kufanya kazi KILAMCO. Ardhi ya kujenga kiwanda ilinunuliwa Kilwa Masoko, kiwanja cha ndege kikatengenezwa, mpango wa kuimarisha bandari ya masoko ukaandaliwa. Mgogoro wa uchumi wa miaka ya 1980 ikatibua mambo.

Dr. Shija waziri wa Nishati na Madini katika kipindi cha kwanza cha Rais Mkapa alizungumzia umuhimu wa kufufua mradi wa KILAMCO lakini hakuna kilichotendeka. Gesi ilipoanzwa kuchimbwa Songosongo likajengwa bomba dogo la nchi 12 kusafirisha gesi chini ya bahari toka Songosongo hadi Somanga. Bomba la nchi 14  lilijengwa toka Somanga hadi Dar es Salaam.

Uwezo wa mabomba haya ni mdogo ukilinganisha na gesi inayopatikana Songosongo na mahitaji yake kwa shughuli ya kufua umeme na kutumia viwandani. Mkopo wa kujengea bomba la Songosongo hadi Dar es Salaam ulighubikwa na tuhuma za ufisadi za ujenzi wa kituo cha kufua umeme cha IPTL kinachotumia mafuta mazito ambacho gharama zake za kufua umeme ni za juu sana. Mkataba wa TANESCO na IPTL uliiwajibisha TANESCO kuilipa IPTL dola milioni moja kila mwezi hata kama haijazalisha umeme wowote. Mkataba huu ulidhoofisha sana hali ya fedha ya TANESCO.

Kampuni ya Artumas iligundua kuwepo kwa gas Mnazi Bay, Mtwara na kuanza utaratibu wa kuichimba mwaka 2006 na kuitumia kufua umeme wa Megawati 18. Kabla ya mtikisiko wa sekta ya fedha na uchumi wa dunia wa mwaka 2008, Artumas ilikuwa na mpango wa kuwekeza kwenye mtambo wa kufua umeme Mtwara wa Megawati 300 na kuunganisha Mtwara kwenye gridi ya taifa. Mpango huu ulikubaliwa na serikali na ukaingizwa katika Mpango Kabambe wa Taifa wa kufua na kusambaza umeme (National Power Development Master Plan). Mradi huu wa kufua umeme MW 300 Mtwara ulipangwa uwe umekamilika mwaka huu wa 2012.

Mtikisiko wa uchumi na fedha duniani wa 2008 uliikumba kampuni ya Artumas. Thamani ya hisa za Artumas iliporomoka katika soko la mitaji Canada na Norway. Artumas iliiomba serikali dola milioni 7 kunusuru Mradi wa Nishati wa Mtwara (Mtwara Energy Project). Uwezo wake wa kutekeleza mpango wa kufua umeme Mtwara ukatetereka pamoja na kuwa mradi huo una faida ya muda mrefu. Kampuni ya Artumas Group Inc. iliamua kubadilisha jina lake na kuwa Wentworth Resources Limited.

Wananchi wa Mtwara wanahitaji kujua kwa nini serikali haikutafuta njia mbadala ya kugharamia mpango wa kufua umeme na kuiunganisha Mtwara na gridi ya taifa?

Wentworth Resources wamefanya upembuzi yakinifu (feasibility study) na kubaini kwamba njia nzuri ya kibiashara na kiuchumi ya kutumia gas wanayoweza kuzalisha Mnazi bay hivi sasa ni kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mbolea na kemikali nyingine Mtwara. Hata hivyo serikali imewamrisha kupeleka gesi watakayozalisha kwenye bomba la gesi la kwenda Dar es Salaam. Gazeti la Financial Time la London la tarehe 6 Desemba 2012 linaeleza

“Bob McBean, executive chairman of Wentworth Resources, which explores in Mnazi Bay, had been planning to use any gas finds together with an existing discovery to power a petrochemical plant to make Africa’s first home-produced fertiliser. “We can supply 80[bcf] right away but we’d have made more money with the plant,” anasema Bw.Mc Bean ambaye kampuni yake imetakiwa kusafirisha  gesi kwenda Dar es Salaam.

Kampuni inayochimba gesi inaamini kuwa kujenga kiwanda cha kutengeneza mbolea Mtwara kitakuwa na faida kubwa kwa kampuni yake. Isitoshe kiwanda hicho kitaongeza ajira kwa vijana wa Mtwara. Kitaanza kuijenga Mtwara kama kituo cha sekta ya gesi na viwanda vyake. Upatikanaji wa mbolea ya bei inayotengenezwa hapa nchini utasaidia kuendeleza kilimo na kuifanya kaulimbiu ya Kilimo Kwanza kutekelezwa kwa vitendo. Hatua ya serikali kuilazimisha Wentworth Resources kuipeleka gas ya Mnazi Bay kwenye bomba la gesi ili isafirishwe Dar es Salaam kunaathiri maendeleo ya Mtwara na Tanzania kwa ujumla.

Ujenzi wa bomba la Mtwara umeanza bila kuwa na mipango ya kuhakikisha kuwa kutakuwepo na gesi ya kutosha kuisafirisha hadi Dar es Salaam. Bomba hili litakuwa na uwezo wa kusafirisha futi za ujazo bilioni 200. Uwezo wa gesi ya Mnazi Bay kwa hivi sasa ni futi za ujazo bilioni 80. Hakuna mpango unaoeleweka wa kupata futi za ujazo bilioni 120 ili bomba la gesi liweze kutumiwa kikamilifu. Mpaka hivi sasa gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni 33 imegunduliwa hasa katika bahari yenye kina kirefu. Kuna uwezekano wa kugundua mafuta. Uchimbaji wa gesi hii bado haujaanza. Inaweza kuchukukua miaka 7 – 10 kabla ya shughuli ya uchimbaji wa gesi kukamilika na kuanza kuitumia ndani ya nchi au kuiuza nje ya nchi.

Upatikanaji wa mkopo wa masharti nafuu kutoka China wakujenga bomba la gesi ndiyo umeishawishi serikali kutekeleza mradi  huu haraka bila maandalizi ya uzalishaji wa gesi ya kutosha.Ni vyema serikali ingetekeleza mradi wa kufua umeme Mtwara na kuunganisha Mtwara na gridi ya taifa na kuruhusu kiwanda cha mbolea kuanzishwa Mtwara.

CUF Chama cha wananchi tunaitaka serikali kuzingatia kuwa, kwa kuwa mradi wa kujenga bomba la gesi uko katika hatua za mwanzo ni vyema serikali ikatathmini upya mantiki na faida za mradi huo. Mradi unaweza kutekelezwa kwa awamu. Awamu ya kwanza iwe kujenga bomba la gesi had Somanga Kilwa ili kuongeza uwezo wa kusafirisha gesi ya Songosongo kuja Dar es Salaam.

Kama nchi bado tuna udhaifu mkubwa wa kuandaa mipango na kusimamia utekelezaji wake. Serikali itufahamishe utekelezaji wa National Power Development Master Plan umefikia wapi? Vipi Mtwara development Corridor bado ipo?

Katika kusimamia sekta ya gesi tujifunze toka nchi ya Norway, Ili kuendesha shughuli za mafuta kwa ufanisi, Norway iliamua mapema kuwa makao makuu ya shughuli za mafuta utakuwa Stavange na siyo mji mkuu wa Oslo. Uamuzi huu umeufanya mji wa Stavange kukua na kuwa kituo cha biashara ya mafuta. Mtwara uwe mji mkuu wa shughuli zote za mafuta na gesi kwa sababu ina bandari asilia yenye kina kirefu na gesi imeanza kugunduliwa kanda ya kusini ya bahari ya Tanzania.

CUF tunasisitiza kwamba, malalamiko ya wananchi wa Mtwara ni ya msingi na wala hayaathiri umoja wa kitaifa. Maoni yao ya kuwa na viwanda vinavyotumia gesi Mtwara na maeneo mengine ya kusini yana mantiki ya kiuchumi. Serikali iwasikilize isiwabeze. Msimamamo wa CUF wa Dira ya Mabadiliko ni kuhakikisha kuwa maliasili na raslimali za nchi zinatumiwa vizuri kuleta neema kwa wananchi wote. Wananchi wa Mtwara wana haki ya kunufaika na neema ya gesi ya Mnazi Bay.

Mwisho Watanzania wote heri ya mwaka mpya – Happy New Year.

Imetolewa na

Mwenyekiti wa CUF-Chama cha wanachi, Taifa
Mhe. Prof. Ibrahim Lipumba


Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU