BEKI wa Azam FC, Aggrey Morris Ambroce amefukuzwa kwenye kambi
ya timu hiyo leo mjini Tanga, baada ya kuthibitika naye alipokea rushwa kutoka
klabu ya Simba ili kuihujumu timu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara.
Aggrey ameondolewa kambini leo, siku moja tu baada ya kipa
Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Said Mourad na Erasto Nyoni nao kusimamishwa kwa
tuhuma hizo.
Azam ilifungwa na Simba mabao 3-1 Oktoba 27, Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam katika mechi za Ligi Kuu na baada ya hapo ikamfukuza kocha wake
Mserbia, Boris Bunjak na kumrejesha Muingereza, Stewart Hall.
Habari kutoka ndani ya Azam zimesema kwamba baada ya kupata
taarifa hizo, uongozi ulizifanyia kazi taratibu na kujiridhisha kabisa
wachezaji hao watatu walikula njama za kuihujumu timu katika mechi hiyo.
Kwa sababu hiyo, uongozi kwanza umewasimamisha wachezaji hao
na hatua zaidi zitafuatia baadaye.
Hata hivyo, Dida hakucheza mechi hiyo, kwani Oktoba 27,
kikosi cha Azam kilikuwa;
Mwadini Ali, Ibrahim Shikanda, Samir Hajji Nuhu, Said Mourad, Aggrey Morris,
Abdulhalim Humud, Jabir Aziz aliyempisha Abdi Kassim, Himid Mao aliyempisha
Kipre Balou, John Bocco ‘Adebayor’ aliyempisha Khamis Mcha ‘Vialli’, Kipre
Herman Tcheche na Salum Abubakar.
Siku hiyo,
Azam walitangulia kufunga dakika ya nne, kupitia kwa Adebayor ambaye alimtoka
beki Mkenya Paschal Ochieng na kumchambua Juma Kaseja, kabla ya Felix Mumba
Sunzu Jr., kuisawazishia Simba dakika mbili baadaye, akiunganisha kwa kichwa
krosi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya kulia.
Okwi
aliifungia Simba bao la pili dakika ya 40, baada ya kutokea kizaazaa langoni
mwa Azam kufuatia mpira uliopigwa langoni mwa timu hiyo na Mwinyi Kazimoto na
dakika tano tu tangu kuanza kipindi cha pili, Mganda huyo tena akawainua vitini
mashabiki wa Simba, akifumua shuti la umbali wa mita 19, baada ya kuwatoka
mabeki wa Azam.
Habari zaidi
zinasema kwamba, uchunguzi unaendelea kufanywa juu ya wachezaji wengine
wanaotuhumiwa kuwa katika mkumbo huo wa kuihujumu timu na ikithibitika ni
ukweli, watachukuliwa hatua pia bila kujali majina yao.
Azam tayari
iko Tanga tangu jana saa 8:00 mchana wa kwa ajili yao ya mchezo wao wa mwisho
wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho dhidi ya
Mgambo JKT, Uwanja wa Mkwakwani.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog