Facebook Comments Box

Tuesday, October 9, 2012

YANGA WALALA TENA MZUNGU WA NNE

HISTORIA ya wachezaji wa Yanga kulala mzungu wa nne imejirudia tena Bukoba, baada ya kulala kwa kubanana katika kitanda kimoja kama ilivyokuwa Mbeya, licha ya kufikia katika Hoteli ya Smart, yenye hadhi kubwa.

Hali kama hiyo ilijitokeza wakati timu hiyo ikijiandaa kucheza na Prisons, Mbeya, huku aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet akianika ukweli ambao baadaye ulimponza na kufukuzwa.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa wachezaji alisema, mambo ni yale yale kama ilivyokuwa Mbeya.

“Mambo kama ya Mbeya, hoteli ni nzuri, lakini wachezaji tumelala wawili wawili katika hoteli, pamoja na kupata huduma nzuri lakini tatizo lilikuwa ni hilo,” alisema mmoja wa wachezaji hao.

Hata hivyo wachezaji wanatarajiwa kurejea kwa usafiri wa basi, badala ya ndege maalumu ya kukodi ya Kampuni ya Precision Air, iliyotumika kwenda Kagera kwa ajili ya mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, dhidi ya Kagera, uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Habari zilizopatikana kutoka kwa kiongozi mmoja, ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, zinasema wachezaji hao watarejea kwa usafiri huo baada ya mchezo wao dhidi ya Toto African, ambao utachezwa keshokutwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Wachezaji hao wanatarajiwa kuondoka mjini Mwanza Ijumaa, baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya Toto African, kwa basi maalumu walilopewa na wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania TBL kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro.

Hata hivyo, gazeti hili liliweza kuongea na mkuu wa msafara, Mussa Katabaro, ambaye alisema anachojua yeye ni kwamba timu yao itarejea kwa ndege kama ilivyokuja.

Wakati huo huo, uongozi wa Kagera Sugar uliondoa mabango ya wadhamini wa Yanga, Kampuni ya Bia Tanzania, kutokana na kuwa wenyeji wa mchezo huo.

Kagera Sugar ambao ndio wenyeji wa uwanja huo kupitia kwa mratibu wake Mohamed Hussein, ilikataa katu katu mabango hayo kuwekwa katika uwanja huo, kwa kuwa wao ndio wa miliki wake.

Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU