Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba Halmashauri ya Wilaya ya
Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, wametoa mapendekezo ya pamoja
wakitaka mambo matano yaondolewe kwenye Muungano, yabaki kwenye Serikali
washirika.
Waliyopendekeza yaondolewe ni Mambo ya Nje, Uraia
na Uhamiaji, Sarafu na Benki kuu, usajili wa vyama vya siasa pamoja na
ushuru wa bidhaa wakisema kwamba kama yataendelea kuwepo kwenye Muungano
kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba yatasababisha
Serikali shirikishi kuwa dhaifu.Wakizungumza baada ya kuwasilishwa kwa
kazi za makundi yaliyopewa jukumu la kujadili suala la mihimili, wajumbe
hao walisema mambo hayo matano ndiyo yanayoweza kuzipa nguvu Serikali
shirikishi ambazo zitakuwa Tanganyika na Zanzibar.
Walitolea mfano wa mambo ya nje na kusema kuwa
ikiwa Rais wa Serikali ya Tanganyika au Zanzibar ataondolewa jukumu la
kuteua mabalozi na hata kuiwakilisha nchi nje ya nchi atakuwa
ameondolewa meno. “Nchi washirika ziachiwe masuala ya mambo ya
nje,”alisema Kassim Mohamed Kassi, mkazi wa Chimba akiwakilisha vijana.
Kuhusu Sarafu na Benki Kuu, walisema sababu za
kupendekeza iondolewe katika muungano ni kuwa itadhoofisha uchumi wa
nchi washirika.
Aidha kwa upande wa uraia na uhamiaji,
walisisitiza kuwa kila nchi watu wake wana utamaduni usioingiliana na
nchi nyingine washirika, hivyo kila upande uwe huru.
Ushuru wa bidhaa, wajumbe hao walipendekeza ubaki
kwenye nchi washirika na siyo Muungano kama inavyopendekezwa kwa sababu
ikiwa itaachwa hivyo sehemu kubwa ya kodi na ushuru kutoka nchi
washirika zitashindwa kuwanufaisha watu wake.
Kuhusu usajili wa vyama vya kisiasa, wajumbe hao
walisema hiyo ni moja ya kero za muungano iliyojitokeza baada ya kuingia
kwa mfumo wa vyama vingi. Sheria ya chama ili kisajiliwe sharti kipate
wanachama wa mikoa ya Tanzania bara na Zanzibar. Walitaka mambo ya
muungano yabaki mawili tu ambayo ni Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania pamoja na Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano.
SOURSE:MWANANCHI
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog