Jopo la
Madaktari Bingwa Saba wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na
Taasisi ya Mifupa ya hospitali hiyo (Moi), wamefanikiwa kuwatenganisha
pacha waliokuwa wameungana kiwiliwili.Iliwalazimu mabingwa hao kutumia
saa nne kufanikisha upasuaji huo. Mmoja wa watoto hao waliotenganishwa,
amelazwa kwenye Wodi ya Uangalizi Maalumu (ICU) Taasisi ya Mifupa Moi
wakati kiwiliwili kingine kilifariki.
Jopo la madaktari waliofanikisha
upasuaji huo ni; bingwa mstaafu wa watoto ambaye aliitwa maalumu kwa
kazi hiyo, Petronila Ngiloi, Dk Robert Mhina (mifupa) na Profesa Karim
Manji aliyekuwa akifuatilia kwa karibu mapigo ya moyo.
Wengine ni Dk Karima Khalid aliyekuwa
akiratibu dawa ya usingizi, Dk Hamis Shaaban (ubongo na uti wa mgongo),
Dk Zaitun Bokhary (bingwa upasuaji watoto) na Dk Nyangasa (moyo na
mishipa ya fahamu).
Akizungumza baada ya upasuaji huo, Dk
Shaaban alisema walimfanyia vipimo mtoto ambaye hakuwa amekamilika na
kugundulika kuwa hakuwa amekamilika viungo vyote achilia mbali kutokuwa
na kichwa na macho pia hakuwa na moyo, figo, tumbo, maini ila alikuwa na
uti wa mgongo.
"Uti wa mgongo ulikuwepo na ndio
uliokuwa umeshikana na mwenzake na kuna mshipa mmoja wa fahamu ulikuwa
unafanya kazi ndio maana alikuwa ukimgusa anachezesha mguu."
Alisema kinachoratibiwa kwa sasa ni
kuangalia dawa ya usingizi aliyopewa mtoto ambaye anaendelea kupumua na
kwamba ndani ya saa 24, dawa ya usingizi waliyomuwekea mtoto huyo
itakuwa imeisha na ataanza kunyonya kama kawaida.
Upasuaji
Upasuaji
Kazi ya upasuaji huo ilianza saa mbili
asubuhi kwa mtoto huyo wa jinsi ya kike aliyetimia kuchukuliwa vipimo
mbalimbali ikiwemo CT Scan, MRI, Ultra sound na vingine vingi kabla ya
upasuaji kamili kuanza saa tano asubuhi.
Dk Shaaban alisema ni mara ya kwanza
kwa Moi kufanya upasuaji wa aina ile na kwamba mara nyingi wamekuwa
wakifanya upasuaji wa watoto wanaozaliwa na vichwa vikubwa pamoja na
mgongo wazi ambao tatizo hilo linasababishwa na upungufu wa madini ya
folic acid.
Kabla ya upasuaji kuanza, mama wa
mtoto huyo Pili Hija (24) alitumia muda wa nusu saa kufanya maombi
maalumu ya kumwombea mtoto wake kisha kuwaruhusu madaktari kuendelea na
upasuaji huo.
Akizungumza muda mfupi baada ya
kuruhusiwa kumwona mtoto wake, Hija alisema: "Ninamshukuru Mungu kwa
yote na nazidi kumwomba amjalie mwanangu apone kabisa, nawashukuru na
nitazidi kuwaombea madaktari wanaomtibu mwanangu."Alijifungulia nyumbani
Agosti 18 maeneo ya Jang'ombe, Zanzibar watoto pacha walioungana mmoja
akiwa amekamilika viungo vyote na mwingine akiwa na kiwiliwili.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog