![]()  | 
| Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Sadifa Juma Khamis | 
Chanzo kutoka ndani ya kikao hicho kilichotarajiwa kumalizika jana 
katika ukumbi wa White House, mjini Dodoma, kilisema hali ya 
kutokuelewana ilitokea mara baada ya Sadifa kutoa hotuba hiyo juzi 
mchana.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, kulikuwa na hali ya kutoelewana ndani 
ya kikao hicho huku wasemaji wa umoja huo wakikatizwa mara kwa mara na 
kelele za kuzomeana.
“Baadhi ya vijana walikaa katika makundi na kuazimia kumuondoa 
mwenyekiti kwa kitendo chake cha kuwadhalilisha tena mbele ya waandishi 
wa habari wakati wa ufunguzi wa kikao hicho,” kilisema chanzo hicho. 
Pia vijana hao walikasirishwa na kitendo cha Mwenyekiti wa Taifa 
 Sadifa kumtimua mmoja wa waliokuwa wagombea wa nafasi ya umakamu 
mwenyekiti, Paul Makonda,  kwa madai kuwa alikaririwa na vyombo vya 
habari  mara baada ya uteuzi huo akitaka kupewa nafasi ya kufikiriwa. 
Aidha, wajumbe wa Baraza hilo walikerwa na kitendo cha Sadifa 
kumwachisha kazi mmoja wa watumishi wa umoja huo kutokea Visiwani 
Zanzibar aliyejulikana kwa jina moja la Jamal. 
Mvutano huo uliodumu kwa zaidi ya saa mbili na kutawaliwa na vikao 
vya siri, ulifanya kuchelewa kuanza kwa kikao hicho kwani badala ya 
kuanza saa 5:00 asubuhi kilianza saa 7:00 mchana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, mjumbe kutoka mkoani 
Mbeya, David Mwakiposya, alisema hotuba aliyotoa mwenyekiti wao ni mbovu
 na haifai. 
“Kwa mujibu wa kanuni za Umoja wa Vijana wa CCM ya mwaka 2008, 
Baraza Kuu ndilo linathibitisha uteuzi wa wajumbe wa Baraza, lakini cha 
kusikitisha aliwafukuza wajumbe wawili ambao  wakati wa mkutano mkuu 
yeye aliwateua na tena aliwaita mwenyewe waje katika mkutano huu,” 
alisema na kuongeza kuwa:
“Ni kitendo kisichofaa kabisa katika nchi yetu wakati tungali 
tunatengeneza demokrasia. Bahati nzuri alilizungumza hili mbele yenu, 
hapa mmeniuliza maoni yangu kuhusiana na hotuba hii maoni yangu ndiyo 
hayo siiungi mkono hotuba yake.” 
Mwakiposya alisema Sadifa aliongea kuhusiana na suala la mapenzi 
ndani ya baraza hilo kwamba limekuwa likisababisha kuvujishwa kwa siri 
za vikao, jambo ambalo alisema halina ukweli wowote. 
Alisema mwenyekiti huyo katika hotuba yake aliwatuhumu meza kuu 
(viongozi wa juu wa umoja huo ), kuwa wamekuwa wakijihusisha na mapenzi 
na hivyo kazi hazifanyiki jambo ambalo halina ukweli.
“Mimi kama mjumbe wa Baraza Kuu nimesikitishwa, nimeguswa, 
sifurahishwi na hayo yaliyojitokeza katika hotuba hiyo, “ alisema 
Mwakiposya huku akisisitiza kuwa hayo ni maoni yake binafsi.
Kuhusu suala Mwenyekiti huyo kutamka wakati akiwania nafasi hiyo 
aliingizwa katika makundi yanayojiandaa kwa ajili ya urais, Mwakiposya 
alisema: “Hiyo ndiyo tabu ya kuwa na kiongozi anayeamini katika hili 
huku anatenda hivi.” 
“Alipowateua hawa watu aliowafukuza tuliamini kuwa haegemei katika 
makundi, lakini katika utekelezaji hakuna….Mimi sifahamu katika UVCCM 
kama kuna makundi, lakini baada ya kusema hilo nikajua kuwa kumbe kuna 
makundi,” alisema. 
Na kwa upande wa siri kuvuja, alisema yeye ni mmoja wa watu ambao 
anaamini kuwa kiongozi yoyote anayevujisha siri za vikao hafai katika 
uongozi. 
Hata hivyo, alisema hajawahi kusikia kuhusiana na kuvujishwa kwa 
siri za vikao na viongozi licha ya kuwafahamu viongozi mbalimbali wa 
umoja huo. 
“Tunaonyana ndani ya vikao halali hatuwezi kuzungumza  kwa 
waandishi wa habari mambo ambayo tunayaona kuwa hayaendi sawa 
tutayazungumza ndani ya vikao vyetu,” alisema alipoulizwa kuhusiana na 
kauli kuwa kuna baadhi ya makundi yalionekana kukaa kabla ya kuanza kwa 
 kikao cha siku ya jana. 
Kuhusu madai ya kutaka kumng’oa mwenyekiti wao, Mwakiposya alisema 
hajasikia kitu kama hicho na kwamba kama kinakuwapo umoja huo 
unataratibu za kikanuni za kufuata ili kumng’oa mwenyekiti. 
“Kanuni ya mwaka 2008 inasema kama ikithibitika kiongozi yeyote 
amekiuka kanuni Baraza linaweza kutoa pendekezo katika kikao cha juu 
kumsimamisha, lakini kama sisi tunataka kumsimamisha kama vijana 
hatujafikia huko bado,” alisema.
Alisema iwapo ikidhibitika kuwa hawawezi kwenda sambamba na kiongozi yeyote yule basi watafukuzana. 
Alipoulizwa kama mwenyekiti huyo amekiuka kanuni yoyote, alisema 
amekiuka kanuni ya kufukuza watumishi wa umoja huo kwa kumfukuza mmoja 
wa watumishi kutoka Zanzibar. 
Alifafanua kwa mujibu wa kanuni, kikao chenye mamlaka ya kumfukuza mtumishi ni Baraza Kuu la Umoja wa Vijana. 
Kwa upande wake, Mjumbe Halmashauri Kuu ya CCM (jina tunasitiri), 
alisema alisikia tetesi kuhusiana na kung’olewa kwa mwenyekiti, lakini 
UVCCM ni jumuiya ya muda mrefu ambayo ina taratibu zake za kumuondoa 
kiongozi. 
“Usiwaone hivi, hawa ni viongozi waliokomaa, hakuna ambalo linaweza
 kuharibika ila inachofahamu hakuna mtafaruku na kama ulikuwapo 
umeisha,” alisema na kuongeza wajumbe hao wako salama na wanaendelea 
vizuri. 
Alisisitiza kuwa hakuna mkanganyiko utakaotokea mara baada ya 
kumalizika kwa kikao hicho cha siku mbili ambacho kitafuatiwa na semina 
na kwamba hakuna kitu kipya kwa kuwa kila inapokaa jumuiya hiyo kumekuwa
 na harakati.
Katika tukio jingine waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali 
vya habari,  walijikuta wakikalishwa na Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, 
Mboni Mhita, kwa zaidi ya saa tatu katika ukumbi wa mikutano wa 
sektarieti ya chama hicho. 
Mhita aliwaita kwenye chumba hicho, kwa madhumuni ya kuwaeleza kile
 kilichotokea katika kikao hicho kwa siku mbili za juzi na jana. 
“Tukubaliane nitazungumza nitazungumzia agenda za jana (juzi) na 
kinachoendelea leo (jana), tu, lakini sitazungumzia yatokanayo…ama 
vinginevyo muendelee kumsubiri Katibu Mkuu aje aongee nanyi,” alisema. 
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kuletewa faili aliloliitisha, 
aliondoka na kuwataka waandishi wa habari kuendelea kusubiri kwa sababu 
alikuwa akimsubiri mjumbe wa kitengo fulani aje azungumzie mambo ambayo 
hata hivyo hakuyafafanua.
Akijibu madai hayo, Sadifa ambaye pia ni mbunge wa Donge, alisema 
walipanga kuanza kikao saa 7:00 mchana na kwamba kwa kuwa wajumbe 
wanafahamiana kukaa katika makundi si kosa.
“Maana Katiba yenyewe inaruhusu watu kukaa vikundi ili mradi wawe 
hawavunji taratibu, sheria na kanuni…baada ya muda kufika si waliingia 
kwenye kikao kama jana (juzi) kikao kilikuwa kizuri tofauti na vyombo 
vya habari mlivyokuwa mkisema huko nje,”alisema.
Kuhusu hoja ya kumng’oa kwa madai ya kukiuka kanuni, Sadifa alihoji
  “ Kanuni namba ngapi?.. Jamal hajafukuzwa sasa wewe utuambie 
aliyemfukuza ni nani? Jamal ni mjumbe halali wa hiki kikao kama angekuja
 lakini kwa bahati nzuri ama mbaya, Jamal mwenyewe alinifuata baada ya 
majina kurudi na kuniambia kuwa amechoka anataka apumzike.”
Alisema  kwasababu Jamal anafanya kazi mbili Zeco visiwani 
 Zanzibar na katika Chama kama Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Vijana, 
alimuomba apumzike ili aendelee na utumishi wake serikalini. 
 Kuhusu hotuba yake kuwadhalilisha, Sadifa aligeuka mbogo: “Nani, wajumbe? Tutajie? ama wewe? Eh, tuthibitishie.”
Hata hivyo, alikanusha kuwa hakuna mjumbe aliyedhalilishwa wala 
aliyelalamikia hotuba yake na kuwalaumu waandishi wa habari kuwa wana 
matatizo ya kuwagombanisha watu.
 Kuhusu Makonda, alisema kanuni ya Umoja wa Vijana inasema yeye 
anateua mtu  ambaye anatakiwa kuthibitishwa ndani ya kikao cha Baraza 
Kuu la umoja huo na kanuni hizo haziruhusu kupeleka kila kitu katika 
vyombo vya habari.
 Alisema baada ya kuona magazeti yamemnukuu Makonda akisema kuwa 
hawezi kukubali uteuzi huo ili asije kuonekana kuwa amehongwa, alifahamu
 hizo ni hasira za uchaguzi.
 “Kwa hiyo mimi nilimpigia simu mmoja mmoja, Makonda  Msarika, 
jamani nimeona statement (taarifa), hizi katika magazeti haya, hebu 
niambieni uteuzi huu mmeukubali ama mmeukataa? Wao wenyewe hakuna 
aliyekuja kunipa kauli yake kama wamekubali uteuzi,” alisema.
 Alimtolea mfano Makonda kuwa amemwita wakutane lakini alikataa,” 
unajua siasa lazima ukae na mwenzako mzungumze mbadilishane mawazo ndiyo
 siasa, jana usiku (juzi ), baada ya kumaliza kikao, nilimpigia 
tukutane…tukae tuvunje migogoro iliyokuwapo, lakini hakuonekana.”
Alisema baadhi ya wajumbe walipoona ujio wa Makonda, walitaka kufanya vurugu wakihoji juu ya ujio wake.
“Kwa sababu pia baadhi ya wajumbe kwa kuona Paul Makonda, pale 
walitaka kuanzisha vurugu, kwa busara tukatuliza sijui tumeelewana 
vizuri?...Alitakiwa baada ya kusomwa kanuni na kujulikana wajumbe, basi 
wajumbe wabaki kwa wakati ule si mjumbe kwa maana hakuthibitishwa na 
Baraza Kuu kwa hiyo alitakiwa kwanza atoke ili Baraza Kuu liridhie ama 
lisiporidhia sawa,” alisema.
     CHANZO:
     NIPASHE
    
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
