MWANAMUME mmoja katika 
mtaa wa Mwanzo, Eldoret anauguza majeraha baada ya kupigwa na mkewe 
kufuatia mzozo uliotokana na yeye kupatikana akitazama runinga kabla ya 
kumaliza kazi ya nyumbani.
Kwa mujibu wa majirani mkewe mwanamume
 huyo, alirejea nyumbani jioni kutoka kazini mnamo Jumatatu na kumkuta 
akitazama televisheni. Mara moja, alimrukia na kumpiga vibaya.
Mwanaume
 huyo aliokolewa na majirani waliofika kuitika kilio chake na kumkuta 
akigaragara sebuleni kutokana na maumivu. Walimpeleka katika zahanati ya
 kibinafsi alikotibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Majirani walisema wawili hao wamekuwa wakigombana mara kwa mara baada ya mwanamume huyo
  
 
 
kufutwa kazi miezi michache iliyopita.
Wakazi
 wa Mwanzo sasa wanalitaka Shirika la Maendeleo ya Wanaume kuingilia 
kati na kuokoa wanaume ambao wanadai wanadhulumiwa na kuchapwa na wake 
zao kila siku. Wanasema visa hivyo vimeongezeka mtaani humo. Aidha, 
wanataka wanaume hao wapewe ushauri wa kisheria kuwasaidia kutafuta 
usaidizi.
Mmoja wa wakazi, Justus Mwaniki, 
alisema wanaume wengi wanapigwa na wake zao kwa kuonekana kama mzigo 
nyumbani hasa wanapokosa kazi: “Sisi huwatunza wake zetu, na kukidhi 
mahitaji hao hata wakiwa hawana kazi na huleta nyumbani mapato yetu kwa 
matumizi ya familia. Mbona wadhulumu wanaume ambao hawana kazi?” 
alishangaa.
Majuzi, kiongozi wa Maendeleo 
ya Wanaume Nderitu Njoka alijipata taabani baada ya kukaripiwa na 
mwanamke mwenye nyumba kaunti ya Kiambu alipokuwa ameenda kumwoka 
mwanamume aliyedai alikuwa akizuiliwa na kudhulumiwa nyumbani.