Rais Jakaya Kikwete akimjulia hali Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa David 
Msuya Hospitalini, kwa sasa amepelekwa Uingereza kwa matibabu zaidi 
            
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Cleopa David Msuya aliyepelekwa nchini 
Uingereza hivi karibuni kwa matibabu, anatibiwa katika hospitali ya 
kifahari inayomilikiwa na familia ya Malkia Elizabeth wa Uingereza.
 
Msuya anatibiwa katika Hospitali ya ‘The King 
Edward the V11’s Sister Agnes’ ambayo ni binafsi inayoongoza kwa huduma 
bora na gharama nchini humo, ambayo mlezi wake mkuu ni Malkia Elizabeth 
wa Uingereza.
Waziri Msuya aliyekuwa amelazwa katika Hospitali 
ya Muhimbili kitengo cha Mifupa (MOI), alipelekwa nchini Uingereza 
Februari saba kwa ndege maalumu ya kukodi. Hata hivyo, gharama za kukodi
 ndege iliyomsafirisha Msuya kwenda Uingereza hazijajulikana, wala 
aliyemlipia.
Mwananchi Jumapili liliwasiliana kwa simu na 
hospitali hiyo ya The King Edward the V11’s Sister Agnes na kuzungumza 
na idara ya mapokezi, ambayo baada ya kupewa jina la waziri huyo kwa 
herufi moja moja, walimuunganisha mwandishi kwa simu hadi katika kitengo
 cha kuhudumia wagonjwa.
Simu ya pili ilipokelewa na msichana aliyehoji 
maswali kadhaa ambapo baada ya kuridhishwa na majibu ya mwandishi, 
alimuunganisha moja kwa moja na Msuya katika chumba alicholazwa .
Hata hivyo, baada ya kupokea simu ya mwandishi wa 
habari hizi, Waziri Mkuu huyo mstaafu hakuzungumzia lolote kuhusu hali 
yake ya kiafya, bali alimhoji mwandishi, akitaka kujua alikopata 
mawasiliano ya hospitali aliyolazwa.
“Habari yako, nani anazungumza?,?? Msuya aliuliza.
 Baada ya mwandishi kujitambulisha, Msuya alisema: “Nani aliyekupa 
‘contact’ zangu za huku?.” Kisha akakata simu.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein 
Mwinyi alipohojiwa kuhusu gharama za matibabu ya viongozi nje ya nchi 
alisema kuwa zinalipwa na Serikali.
“Mawaziri wakuu wastaafu na waliopo madarakani 
wote ni wafanyakazi wa Serikali, hivyo gharama za matibabu yao zinalipwa
 na Serikali,” alisema Mwinyi na kuongeza:
“Hata hivyo Serikali hulipa gharama hizo kwa 
anayetibiwa nje iwapo kuna sababu ya kufanya hivyo, hii siyo kwa 
viongozi tu, bali kwa Mtanzania yoyote mwenye mahitaji.”
Ofisa Uhusiano wa Kitengo cha MOI , Almas Jumaa 
alisema kuwa Msuya alipewa ruhusa katika hospitali hiyo tangu Februari 
Nne, baada ya kupata nafuu. Hospitali ya Mfalme Edward wa Saba iliyopo 
katika Mtaa wa Beaumont, katika Jiji la Westmister, ilianzishwa mwaka 
1899.
Mtoto wa mfalme wa Wales, ambaye baadaye alikuwa 
Mfalme, Edward wa V11, kimada wake Agness Keyser, pamoja na dada wa 
Agness, aliyeitwa Fanny, walianzisha huduma za matibabu kwa ajili ya 
maofisa wa jeshi.