
Kijana Christopher Kule na babake Dasiel Raul
 
 
Kama kuna rais ambaye watu wengi Uganda wangetaka kukutana naye ni rais wa Marekani Barack Obama.
Kijana Christopher Kule, mwenye umri wa miaka 
kumi na ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi wilayani Kasese, nchini 
Uganda, hajaachwa nyuma katika ndoto hiyo.
                     Bila shaka wengi watasema yuko hatua
 nyingi mbele ya wale walio na ndoto ya kumuona Obama. Hii ni baada ya 
Kule kupokea majibu ya barua aliyomwandikia Rais Barack Obama kutoka kwa
 Obama mwenyewe.
                     Kijana huyo anaamini kuwa baada ya kuandikiana barua na Rais Obama, kuna matumaini kwamba siku moja atakutana naye.
                     Yote haya yanatokana na zoezi la kuandika barua 
ambalo Kule na wanafunzi wenzake walikuwa wanafanya darasani, baada ya 
kuagizwa na mwalimu wamwandikie barua mtu yeyote wakiomba msaada kwa 
jamii yao.
                     Barua ya Kule bila shaka ilimtia hamasa mwalimu wake wa kigeni kutoka Marekani ambaye alikuwa anafunza shuleni humo kwa muda.
                     Mwalimu huyo alisema kuwa nyanyake ni rafiki wa 
mmoja wa wasaidizi katika ikulu ya rais na kuahidi kuhakikisha kuwa 
ujumbe huo utamfikia rais Obama na bila shaka ahadi ikatimizwa , kwani 
barua ilimfikia rais Obama.
                     Kule alisema kuwa katika barua yake, alimwomba Obama kusaidia Uganda kuangamiza uasi na kuhamasisha amani.
                     Katika majibu yake kwa Kule, rais Obama alisema 
kuwa Marekani imejitolea kuangazia maswala kadhaa muhimu kote duniani 
kama haki za binadamu kwa sababu Marekani inapinga vikali ghasia na 
ukandamizaji dhidi ya watu wote. Pia alimtumia kijana huyo picha yake 
aliyokuwa ametia saini.