Katibu wa Muda wa Kamati ya Uratibu Kanda ya 
Kaskazini, Amani Golugwa alisema mkutano huo utafanyika katika Viwanja 
vya Shule ya Msingi Ngarenaro na utahudhuriwa na wabunge wote wa Chadema
 kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini na kuhutubiwa na Mwenyekiti wa 
Taifa, Freeman Mbowe. Kwa mujibu wa Golugwa, Kanda ya Kaskazini 
inajumuisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
“Tunazindua Kanda ya Kaskazini kutekeleza uamuzi 
wa Baraza Kuu lililoagiza mfumo na shughuli za uendeshaji wa chama 
ushuke hadi ngazi ya majimbo ambayo ndiyo sera ya Chadema,” alisema 
Golugwa.
Kabla ya mkutano wa leo, viongozi zaidi ya 200 wa 
Chadema kutoka mikoa na majimbo 30 ya Kanda ya Kaskazini wakiwamo 
wabunge, wenyeviti, makatibu, wenyeviti na mameya wa Halmashauri 
zinazoongozwa na Chadema,walifanya vikao vya ndani kuweka mikakati na 
mfumo wa utendaji kikanda. Kwa mujibu wa Golugwa, ambaye pia ni Katibu 
wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, kikao cha ndani pia kilihudhuriwa na 
mwasisi na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Mzee Edwin Mtei.
Mbowe ambaye ni mmoja wa wajumbe waliohudhuria 
vikao vya ndani, ndiye atakuwa mgeni rasmi na mzungumzaji mkuu kwenye 
mkutano wa hadhara ambao pia utatumika kuwatambulisha wajumbe wa timu ya
 uratibu ya Kanda ya Kaskazini.
Mkutano huo ni wa pili kwa Chadema ndani ya wiki 
mbili zilizopita baada ya kufanya mkutano mkubwa Dar es Salaam 
uliotumika kuueleza umma udhaifu wa mhimili wa Bunge na ukandamizaji  
unaodaiwa kufanywa dhidi ya wabunge wa chama hicho na uongozi wa mhimili
 huo wa dola.
Katika mkutano huo, viongozi wa Chadema 
waliutangazia umma namba za simu za Spika Anne Makinda na Naibu wake, 
Job Ndugai ili wananchi wawapigie au kuwatumia ujumbe mfupi 
kuwashinikiza kufuata Katiba, Sheria na Kanuni za bunge katika 
uendeshaji na maamuzi ya chombo hicho.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog