Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi 
Nchini (IGP) Said Mwema (kulia) Waziri wa Mambo ya ndani Emmanuel 
Nchimbi na Kamnda wa Pilisi Zanzibar Ally Mussa kwenye moja ya mikutano 
na waandishi wa habari.           
SIKU chache baada ya kutokea kifo cha Padri Evarist Gabriel Mushi kupigwa risasi na 
watu wasiojulikana kichwani eneo la Beit el Raas, 
Jana Imamu wa Msikiti wa Mwakaje ameuawa baada ya kupigwa 
mapanga hadi kufa.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, 
Ahmada Khamis amethibitisha kutokea kwa tukio hilo hapo jana mchana 
majira ya saa 8 na kumtaja aliyefariki kuwa ni Sheikh Ali Khamis 
ambaye ameuawa na watu wasiojulikana.
 
Kamanda Ahmada alisema Sheikh Khamis mbali ya kuwa ni Imamu wa 
Msikiti lakini pia ni mkulima na ameuliwa wakati akiwa katika mazingira 
ya kazi zake ndani ya shamba lake huko Kidoti Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akielezea mazingira ya tukio hilo Kamanda Ahmada alisema tukio hilo 
limetokea baada ya Sheikh Khamis kwenda shambani kwake katika shmba la 
minazi Kidoti ambapo wakati akiwa shambani hapo ndipo walipotokea watu 
kadhaa na kumpiga mapanga sehemu za shingoni mwake na kusababisha kifo 
chake muda mfupi baada ya kipigo hicho.
 
Alisema baada ya tukio hilo, watu walimchukua na kumkimbiza 
hospitali lakini kutokana na kupoteza damu nyingi alifariki dunia wakati
 akiwa njiani na hivyo harakati za mazishi zinafanyika baada 
ya kuchukuliwa vipimo na wataalamu wa afya.
Kamanda Ahmada ametoa wito kwa wananchi kutopuuzia taarifa za watu 
ambao wanawashuku na wenye kuleta maafa yakiwemo mauaji hapa nchini, 
kwani kuwaficha wahalifu ni kuendeleza utamaduni usiofaa katika jamii 
ambayo imeanza kuharibika kutokana na mauaji hayo yanayoendelea kila 
kukicha.
Hili ni tukio la nne kwa viongozi wa dini kuhujumiwa ambapo tukio la 
kwanza Sheikh Fadhil Suleiman Soraga kumwagiwa tindi kali na watu 
wasiojulikana na kujeruhiwa vibaya wakati akifanya mazoezi nyakati za 
asubuhi karibu na nyumbani kwake Magomeni, tukio la pili ni lile la 
Padri Ambrose Mkenda aliyepigwa mapanga shingoni na kurejuhiwa vibaya na
 watu wasiojulikana wakati akitaka kuingia nyumbani kwake huko Tomondo 
Mjini Unguja. matukio hayo mawili yalitokea mwaka jana.
Katika mwaka huu nako kumetokea matukio mawili kwa kuuawa kwa Pardi 
Evarist Mushi huko Beit El Raas wakati akitaka kuingia Kanisani na pia 
kuuawa kwa Sheikh Ali Khamis huko Kidoti shambani kwake Mkoa wa 
Kaskanizini Unguja.  Inna lillahi wainna ilayhi rajiiun.