Facebook Comments Box

Tuesday, December 18, 2012

NDEGE KUBWA KUANZA KUTUA KIGOMA




NDEGE kubwa za abiria za kimataifa zinatarajiwa kuanza kutua Uwanja wa Ndege wa Kigoma kuanzia Desemba 15 mwaka huu baada ya uboreshaji wake kufikia hatua nzuri.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na blog hii mjini Kigoma, Meneja wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama wa Anga (TCAA), Godlove Hongore amesema hadi kufikia katikati ya mwezi ujao meta 1,450 za kuruka na kutua ndege zitakuwa zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami kati ya meta 1,800 zinazotarajia kujengwa.
Alisema mkataba wa ujenzi wa mkandarasi wa uwanja huo unaisha Juni mwakani lakini ujenzi umeelezwa na msimamizi wa Kampuni ya Synohydro ya China kwamba unaweza kukamilika mapema zaidi ya muda uliopangwa.
Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mkoani Kigoma, Elipid Tesha alisema mazungumzo yanaendelea vizuri ili kampuni hiyo ya Synohydro ya China iendelee na sehemu ya pili ya mradi huo katika mwaka ujao wa fedha utakaohusisha ujenzi wa njia ya kurukia ndege kufikia meta 3,000 na jengo la utawala na abiria uwanjani hapo.
Alisema tayari fedha za fidia kwa ajili ya eneo la makaburi ambalo litatumika kwa upanuzi huo, ipo na mazungumzo yanaendelea ni kuwezesha mkandarasi huyo kuendelea na sehemu hiyo ya pili ya mradi huo.
Meneja huyo wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Mkoa, alisema kukamilika kwa Awamu ya Pili ya ujenzi wa awanja huo kutaufanya Uwanja wa Ndege wa Kigoma kuwa na hadhi ya kimataifa na kuruhusu ndege kubwa zaidi ya tani 70 kutua.
Alibainisha kuwa uwanja huo ukikamilika, utakuwa kitovu cha ndege nyingi kutoka nchi za ukanda wa Maziwa Makuu na Afrika ya Kati kwenda Kusini na Kaskazini mwa Bara la Afrika na nje ya bara hilo.


KIGOMA UJIJI YATOA MWANAFUNZI BORA WA SAYANSI

SHULE ya Sekondari ya Kichangachui katika Manispaa ya Kigoma Ujiji imetoa mwanafunzi bora wa masomo ya sayansi kwa Kanda ya Magharibi katika mtihani wa majaribio (Mock Test) wa kidato cha nne uliofanyika hivi karibuni.
Akitoa taarifa kwa Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Chung IL aliyefika shuleni hapo kukabidhi rasmi maabara kwa uongozi wa shule hiyo Mkuu wa Shule hiyo, Harles Lugenda alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na kuanzishwa kwa maabara ya masomo ya sayansi katika shule hiyo.
Lugenda alimtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Justus Ferdinand ambaye aliongoza katika masomo ya Fizikia na Kemia ambapo alisema kwamba kuwepo kwa maabara hiyo iliyoanza kufanya kazi Januari mwaka huu kumeinuka ari ya wanafunzi wa shule hiyo kusoma masomo ya sayansi na kuahidi kufanya vizuri.
Maabara hiyo imetolewa na serikali ya Jamhuri ya Watu wa Korea kupitia Shirika lake la Maendeleo (KOICA) ambapo kiasi cha Sh milioni 25 zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa vyumba viwili vya madasara vinavyotumika kama vyumba vya maabara na vifaa vyake.
Sambamba na ujenzi wa vyumba hivyo vya maabara pia Serikali ya Korea kupitia shirika hilo inagharamia masomo ya wanafunzi wanane wanaosoma masomo ya sayansi shule hapo ambapo tayari wameshalipiwa ada kwa miaka minne ahadi watakapomaliza masomo yao ya sekondari.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Balozi Chung IL alisema kuwa msaada huo umelenga kunaimarisha ushirikiano wa kindugu uliopo baina ya serikali hizo mbili na watu wake.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispa ya Kigoma Ujiji , Alfred Luanda alisema kuwa pamoja na msaada huo bado Manispaa hiyo inakabiliwa na upungufu wa maabara za sayansi na vifaa vyake katika shule zake mbalimbali na kwamba kama ipo fursa ya kupata tena msaada zaidi aliomba serikali ya Korea kuangalia uwezekano huo.


BREAKING NEWS: MTU MMOJA AUWAWA KATIKA MAJIBIZANO YA RISASI KATI YA POLISI NA MAJAMBAZI KARIAKOO LEO HII

Mtu mmoja ameuwawa mida hii katika majibizano ya risasi yaliyotokea maeneo ya Msimbazi kariakoo, mtaa wa Livingstone kati ya Polisi na majambazi waliotaka kupora fedha zilizokuwa zinapelekwa benki ya NBC.

Majambazi hao waliokuwa wamevalia nguo za kiraia inasemekana walijua fedha hizo zinapelekwa leo hivyo walijiandaa kupora na Mapolisi nao waligundua hilo mapema hali iliyofanya majambazi hao kurusha risasi hovyo na kukimbia ili kukwepa kukamatwa.

Hadi sasa ni mtu mmoja anayeripotiwa kuuwawa ila bado haijajulikana kama ni raia au jambazi wale maana pia majambazi walivaa kiraia.


AKAMATWA NA UCHAWI MAHAKAMANI KISUTU

Kijana ambae ni mganga kutoka katika mkoa wa Tanga wilaya ya Muheza eneo la Kerege amekamatwa na vifaa ambavyo vinadaiwa kuwa vya kichawi ambavyo alikuwa akiingia navyo mahakamani ili kumfanyia uganga mmoja ya watu wanaokabiliwa na kesi katika mahakama hiyo. Polisi waliweza kugundua kupitia vifaa maalumu ambavyo vimefungwa mahakamani hapo. Picha hapo juu ni mganga huyo akiwa chini ya ulinzi wa polisi

Sunday, December 16, 2012

YANGA KUPAA DESEMBA 28, KULA MWAKA MPYA ULAYA



Kocha Brandts na wachezaji wake

MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC wanatarajiwa kuondoka Desemba 28, mwaka huu mjini Dar es Salaam, kwenda Uturuki kuweka kambi ya wiki mbili kujiandaa kwenda kutetea taji lao hilo mjini Kigali, Rwanda.
Habari kutoka ndani ya Yanga, zimesema kwamba wiki hii mwalimu, Ernie Brandts ataamua idadi na wachezaji wa kwenda ziara hiyo, ambayo ni maalum pia kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
Kocha huyo Mholanzi, kwa wiki zaidi ya mbili amekuwa akikinoa kikosi chake kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Dar es Salaam baada ya kumaliza likizo fupi ya baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
Yanga, chini ya Mwenyekiti wake, Alhaj Yussuf Manji imepania kurejesha utawala wake katika soka ya Tanzania na kwa kuanzia inataka kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu kwa kishindo mwishoni mwa msimu.
Yanga inataka pia kutetea Kombe la Kagame Januari mwakani mjini Kigali, katika michuano ambayo watakwenda na wapinzani wao wa jadi, Simba SC.
Yanga ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa inaongoza kwa pointi zake 29, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 24, wakati Simba ni ya tatu kwa pointi zake 23.     


Saturday, December 15, 2012

TAARIFA YA BAVICHA KUHUSU UNDUMILAKUWILI WA DR SLAA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI, WANACHADEMA NA UMMA WA WATANZANIA JUU YA MWENENDO WA UNDUMILAKUWILI WA BWANA WILBROD PETER SLAA KATIBU MKUU WA CHADEMA TAIFA Ndugu wanahabari, Rangi nyeupe katika bendera chama changu ninachokipenda (CHADEMA) chama changu ninachokipenda inasimamia ukweli na uwazi. Rangi hiyo inawataka wanachadema wote kuwa wazi katika kulinda, kusimamia falsafa, itikadi na sera za chama chetu. Nimehuzunishwa sana ka kukatishwa tama na kitendo cha undimilakuwili na umamluki wa Katibu Mkuu Bwana Slaa kwa kitendo chake cha kuendelea kumiliki kadi ya Chama cha Mapinduzi wakati akitambua kuwa yeye ni Kiongozu anyeongoza harakati za chama Kikuu cha Upinzani hivyo kutakiwa kuwa mfano bora wa kuigwa kwa kuonyesha mwenendo bora kwa kuishi maisha anayohubiri. Katiba ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) sura ya tano ibara ya kwanza ndogo ya 5.1.6 kinachosema “Mwanachama wa CHADEMA asiwe mwanachama wa chama kingine cha siasa baada ya kujiunga na CHADEMA” Akitambua kadi ndicho chombo kikuu kinachomtambulisha mwanachama ndani yachama hivyo, kitendo cha kuendelea kumiliki na kulipia kadi Chama cha Mapinduzi kimedhihirisha kuwa yeye ni mbwa mwitu aliyejivika ngozi ya kondoo ndani ya upinzani. Bwana Slaa amekuwa akiaminisha Umma kuwa yeye ni Kiongozi mzalendo safi huku akiendelea kuwatuhumu baadhi ya wanachama na viongozi wenzie kuwa ni mapandikizi,Hivyo kitendo hicho cha yeye kumiliki na kulipia ya CCM imeonyesha kuwa yuko CHADEMA kwa kazi maalum ya kuhujumu harakati za Ukombozi hivyo hana na amepoteza sifa ya kuwa Kiongozi wa Upinzani. Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA ibara ya tano, BWANA WILBROAD PETER SLAA NI PANDIKIZI kutokana na sababu zifuatazo, ambazo nimejiridhisha nazo bila chembe ya shaka yoyote hivyo tunamuomba apishe uchunguzi dhidi yake ili tukiona dhamira njema tuendeleze harakati za Ukombozi yeye amepoteza sifa, kwa kitendo cha kuwa na Kadi ya chama ambacho kimetesa Watanzania na kuwanyanyasa lakini yeye bila aibu kukusanya kadi za wananchi wanaojiunga na CHADEMA kuzichoma moto na huku yeye akiwa amebaki na yake kibindoni hii imepelekea yeye kufanya kazi na umamluki na kukivuruga Chama kama ifuatavyo:- Amekuwa akitumika kugawa Mabaraza ya chama kwa kuidhinisha kumlipa mshahara Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa Ndugu JOHN HECHE kinyume cha Katiba na mwongozo wa baraza la Chama ilihali Viongozi wengine wa Kitaifa wa mabaraza hata wale wa Mikoani na Wilayani hawalipwi chochote wakati wao ndio wanaohangaika kukijenga Chama. Hii inaonyesha Bwana Slaa analipa fadhila kwa mwenyekiti huyo ambaye maamuzi yote ya baraza huamiliwa na Bwana Slaa, Mfano huu wakulipana fadhila anaoufanya Bwana Slaa ni mfumo wa CCM ambako Slaa ni mwanachama na baada ya kukiri kwamba ni kweli anamiliki Kadi ya CCM hadi leo hii. Bwana Slaa ni Kiongozi anyejihusisha na vikundi vya majungu jambo ambalo ni kinyume na Katiba na kanuni ya Chama kwa kudhihirisha kwamba Bwana Slaa ni mamluki ndani ya CHADEMA aliyekuja kutimiza kazi maalumu amekuwa akichochea mgogoro na kuchukua maamuzi ya kuwafukuza baadhi ya vingozi ambao wamekiongoza chama kwa muda mrefu. Bwana Slaa alifukuza viongozi wa chama Geita. Alifukuza madiwani Arusha. Hapa Mwanza alishinikiza kufukuzwa kwa madiwani wawili CHAGULANI NA MATATAbila kuzingatia falsafa ya Chama kuamini katika nguvu ya umma kwamba wananchi ambao ndio wapiga kura wenye maamuzi juu ya hao Madiwani hawakushirikishwa katika kutoa maamuzi wakati wa kuwafukuza. Bwana Slaa amesababisha madiwani watatu kufukuzwa hapa Mwanza kwakuwakataza wasihudhurie vikao vya Halmashauri. Hivyo kwasababu kupoteza kata tatu (3) ambazo ni Ilemela, Nyamanoro na Kirumba. Kwa madai kwamba hawamtambui Meya MATATA. Pia Bwana Slaa amekuwa akivunja uongozi wa chama bila kuzingatia Katiba ya Chama kama Geita, Nyamagana, mvomero Morogoro Lindi na Mtwara bila kufata Katiba kama inavyoeleza Ibara ya 6.3 (b) mamlaka ya nidhamu na uwajibikaji, “kwamba kingozi aliyeteuliwa na vikao vya uongozi ataweza kusimamishwa au kuachishwa Uongozi na Kikao kilichomteuwa”Lakini yeye amekuwa akifukuza na kuvunja Uongozi katika sehemu mbalimbali za nchi bila kuzingaita misingi ya Katiba, Anaongoza Chama kwa Mfumo wa Hailakia kwamba atakalosema yeye ndio sheria na linalotakiwa kufuatwa na haitakiwi kuhoji. Slaa amekuwa akiwafukuza na kuwaita kwa kuwatukana mamluki Vingozi ambao wamejenga Chama kwa muda mrefu bila hata ruzuku leo hii chama kinapata ruzuku ya zaidi ya Milioni 200 wanaonekana hawafai licha ya kutopelekewa ruzuku majimboni mwao. Vilele Bwana Slaa amekuwa akilazimisha Viongozi wa Chama Mikoani kumpokea anaedaiwa kuwa mchumb wake bibi JOSEPHINE MSHUMBISI kama Kiongozi wa chama Taifa,mchumba wake amekuwa chanzo pia cha migogoro ndani ya chama kwani amekuwa akipeleka watu majimboni na kuagiza viongozi wa Chamawamtambue kama mgombea wa ubunge mwaka 2015, Pia amekuwa akitumia rasiliamali za chama vibaya katika ziara yake. Amekuwa akichangisha michango kwa kisingizio cha M4C ( vuguvugu la mabadiliko) Huku pesa hizo akizitumia kwa ajili ya taasisi yake yake binafsi iitwayo JUKWAA LA WANAWAKE kwa kifupi Josephine Mshumbusi haifahamiki kama ni mwanachama wa CHADEMA au La:- Hivyo Bwana Slaa hatuna imani nae kwani vitendo hivyo vyote vinatishia usalama wa Chama. Jambo lingine la kusikitisha kwa wana – nyamagana na Mwanza nzima kwa ujumla bwana Slaa amemteua Ezekiel wenje mbunge wa Nyamagana kuwa mkurugenzi wa mambo ya nje makao makuu ya chama Dar es salaam hivyo wananchi wa Nyamagana hawana mbunge kwani kwa sasa anaishi Dar es salaam na kufanya kazi huko. Sasa hivi wana- nyamagana hawana tena mbunge kwani yuko Dar es salaam amekuwa mbunge wa makao Makuu. Ndugu waandishi ,katika kudhihirisha kuwa Wenje sasa hivi sio mbunge wa wanachi bali mbunge wa Makao Makuu, Ndugu Wenje haelewi suala lolote linaloendelea jimboni kwake kwani ninyi wanahabari ni mashahidi alipotoa tamko la Uongo mbele yenu akidai machinga wa Mwanza wamesema wanampa siku 14 Mkurugenzi wa Jiji awe amejiuzuru , jambo ambalo lilithibitisha kuwa ni la uzushi kwani SHIUMA (Shirika la Umoja wa Wamachinga). Lilimjibu na kumtaka afute kauli yake kwani hajazungumza wala kuwahi kuonana na wamachinga aache kuwachonganisha na Serikali kwa manufaa yake binafsi kwani hao wameendelea kuchapa kazi ili kujiletea maendeleo wakishirikiana bega begani na Mstahiki Meya na madiwani wao. Ndugu wanahabari katika hili bwana Slaa hawezi kukwepa lawama hivyo basi kama ana uso wa aibu apishe kiti akae pembeni tujenge chama chetu. Ndugu wanahabari: Naamini mnakumbuka mwishoni mwa mwaka huu bwana Slaa alipokuwa anafanya ziara ya kukagua uhai wa Chama Mkoa wa Dar es saalm na majimbo yake alisikika akitekeleza na kuunga mkono mfumo kandamizi na unaofinya Demokrasia na utumiaji mbovu rasimali za nchi hii kwakuwa na wakuu wa Mkoa na Wilaya cha kustaajabisha na kushangaza bila aibu wala soni Bwana Slaa aliwataka viongozi wa Ngazi mbalimbali katika Jimbo la Kigamboni (Chadema) wawe tayari kupewa ukuu wa Wilaya na Mikoa Chadema itakapo kuchukua dola. Kitendo cha bwana Slaa kuendeleza sera za CCM kama kuwepo kwa wakuu wa Wilaya na Mikoa kinapingana moja kwa moja na sera na itikadi za CHADEMA. Kauli tata kama hii inamuhalalisha bwana Slaa kutumikia mabwana wawlili yaani CCM na CHADEMA ndio maana tunamtaka arudishe kadi ya Chadema na aendelee na Chama chake cha CCM anachotekeleza sera na itikadi zake. Ndugu Nadhani mnakumbuka tarehe 28 /10/2012 tulikuwa na uchaguzi mdogo wa madiwani baada ya nafasi hizo kuachwa wazi kwa sababu mbalimbali. Katikauchanguzi ule CHADEMA iliambulia viti 5 (vitano) kati ya viti 29. Lakini baada ya kufanya uchunguzi wa kina kwa nini CHADEMA ilifanya vibaya katika uchanguzi mpaka kupelekea kupata viti vichache kiasi hiki wakati CHADEMA kwa sasa ni chama pendwa kwa Watanzania uchunguzi unaonyesha kwamba katika uchaguzi ule wa madiwani Bwana Slaa ambae alizunguka katika kata zote zilizokuwa zimeachwa wazi hakuwa na agenda ya kuhakikisha CHADEMA inashinda bali alibeba agenda yake binafsi na chama chake pendwa CCM NDIO maana Kanda ya ziwa CHADEMA tulishinda kwa asilimia 99 kwa sababu ya hujuma ya undumilakuwili Bwana Slaa. Ndugu wanahabari: Vyanzo vya mapato katika Vyama vya Siasa ni ruzuku kutoka Serikalini, michango mbalimbali kwa wadau, ununzi wa kadi za vyama kwa wanachama na kulipia ada ya uanachama katika vyama vyao. Bwana Slaa anakichangia CCM ili kiendelee kujiimarisha zaidi kwa kulipia ada ya uanachama . Kwa hio ujenzi na uimarishaji wa CCM unasaidiwa na uwepo wa Bwana Slaa na michango yake katika CCM. HITIMISHO:- Kutokana na mwenendo wa Bwana Slaa Wilbroad ninataka mwenyekiti wa Chama Taifa achukue maamuzi sahihi ya kutuepusha na janga hili ndani ya Chamamaana ni bora uwe moto au baridi kuliko kuwa vugu vugu endapo akishindwa tutaitisha maandamo nchi nzima maana Ni watanzania wazalendo wengi walioumia, kifilisika, na hata kupoteza maisha wakipigania ukombozi wa nchi hii, leo hii mamluki kama WILBROAD PETER SLAA hatuweai kukubali waturudishe nyuma katikaharakati za Ukombozi. Tunamtaka ajiuzuru haraka iwezekanavyo. Hakuna kulala mpaka kieleweke. …………………………….. MIMI SALVATORY MAGAFU KATIBU BAVICHA MKOA WA MWANZA. nakala:wajumbe wote wa BAVICHA TAIFA

Friday, December 14, 2012

KOFFI OLOMIDE NDANI YA DAR

Millard Ayo Koffi Olomide na Ben Kinyaiya kwenye uwanja wa ndege wa Mwalimu JK Nyerere Dar es salaam decemba 14 saa saba na nusu usiku, Koffi Olomide amekuja Tanzania kupiga show mbili moja Leaders Dar decemba 15 2012 na 16 decemba Mwanza ambapo zote zimeandaliwa na Primetime promotions.
.


Monday, December 10, 2012

SHEREHE ZA MIAKA 51 YA UHURU KATIKA PICHA

IMG_1709
Askari wa kikosi cha kutuliza Ghasia (FFU) wakiwa katika mwendo wa haraka


Pg.1


Saturday, December 8, 2012

HATIMAE OKWI AONGEZA MKATABA SIMBA


MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi ameongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea Simba SC ya Dar es Salaam, baada ya kusaini jana usiku katika hoteli ya Sheraton mjini hapa.
Okwi alisaini mbele ya Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage ambaye ameongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.
Baada ya kusaini, Okwi alisema; “Nimefurahi kuongeza mkataba na klabu yangu na ninaahidi kuendelea kuitumikia kwa nguvu zangu zote,”alisema Okwi.
Kwa upande wake, Hans Poppe alisema kwamba anaamini kusaini na Okwi sasa kutawakata vilimilimi wapinzani wao, ambao walikuwa wanamuwania mchezaji huyo.
“Sisi tunajua yote yaliyokuwa yakiendelea kwenye Challenge, tunajua wapinzani wetu walimfuata Okwi huku, lakini huyu mchezaji ana mapenzi yeye mwenyewe na Simba SC,”alisema Hans Poppe.
Okwi aliyezaliwa Desemba 25, mwaka 1992 mjini hapa, alisajiliwa na Simba SC mwaka 2009 akitokea SC Villa ya hapa, baada ya klabu hiyo kumkosa mshambuliaji mwingine Mganda, Brian Umony aliyewahiwa na SuperSport United ya Afrika Kusini.
Tangu msimu uliopita, Okwi amekuwa akihusishwa na mpango wa kuhamia Yanga au Azam na akiwa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge iliyoanza Novemba 24 na inafikia tamati kesho, ziliibuka habari za klabu hizo kumfuata kumsainisha mjini hapa.
Okwi jana alifunga bao moja kati ya matatu ya Uganda kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa, yaliyozima ndoto za Tanzania Bara kurejea nyumbani na Kombe la Challenge.
Kwa matokeo hayo, Uganda itamenyana na majirani zao na wapinzani wao wakubwa, Kenya katika fainali Jumamosi, ambao katika mchezo wa kwanza waliitoa kwa mikwaju ya penalti 4-2 Zanzibar, kufuatia sare ya jumla ya 2-2 ndani ya dakika 120.
Zanzibar na Bara zitamenyana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu siku hiyo hiyo ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Namboole.
Hadi mapumziko, Uganda walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Emmanuel Okwi dakika ya 11, baada ta kuuwahi mpira mrefu uliopigwa na kipa wake, Hamza Muwonge na kufumua shuti kali la umbali wa mita 19, ambalo lilimshinda kipa Juma Kaseja.
Baada ya bao hilo, Okwi aliumia na kutoka nje dakika ya 36 nafasi yake ikichukuliwa na Hamisi Kiiza.
Uganda ndio waliouanza mchezo huo kwa kasi na kulitia misukosuko lango la Stars kwa takriban dakika 10 mfululizo, lakini baada ya hapo timu hizo zikaanza kushambuliana kwa zamu.
Timu zote zilikuwa zikishambulia kutokea pembeni, lakini Uganda ndio walioonekana kuzalisha mashambulizi ya hatari zaidi.
Kipa na Nahodha wa Stars, Juma Kaseja alitoka uwanjani baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza akilaumiana na mabeki wake kwa kufungwa bao la kutanguliwa.
Kipindi cha pili, Waganda walirudi na moto wao tena na kufanikiwa na kupata bao la pili dakika ya 51, safari hii Robert Ssentongo akimtungua Kaseja, baada ya mabeki wa Stars kudhani ameotea.
Pamoja na kufungwa bao la pili, Stars waliendelea kucheza kwa juhudi, ingawa Waganda waliendelea kutawala mchezo.
Mpira uliotemwa na Juma Kaseja kufuatia shuti la Moses Oloya, ulimkuta Ssentongo dakika ya 71 akaukwamisha nyavuni na kuipatia The Cranes bao la tatu. Kutoka hapo, hali ilikuwa mbaya kwa Stars.
Zikiwa zimesalia dakika tano mchezo kumalizika, taa za Uwanja wa Mandela zilizimika, lakini baada ya jitihada za pamoja za FUFA, CECAFA na uongozi wa Uwanja, ziliwaka baada ya dakika saba na mchezo kuendelea hadi filimbi ya mwisho.

Anasaini


Anasaini


Anaweka dole gumba

Thursday, December 6, 2012

DK. SLAA: NAPE ANAPIGA MAYOWE





KATIBU Mkuu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibroad Slaa, amemvaa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye akisema madai aliyoyatoa dhidi yake ni ya kipuuzi na yasiyokuwa na tija kwa Watanzania waliopigika na umasikini.

 
KATIBU Mkuu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibroad Slaa, amemvaa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye akisema madai aliyoyatoa dhidi yake ni ya kipuuzi na yasiyokuwa na tija kwa Watanzania waliopigika na umasikini.

Dk. Slaa alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya Nape kudai kuwa katibu huyo ni CCM damu ndiyo maana hata kadi yao ameendelea kuwa nayo hadi leo licha ya kuhamia CHADEMA.

Akifungua mkutano wa NEC Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza juzi, Nape alidai kuwa Dk. Slaa tangu aikimbie CCM na kuhamia CHADEMA hajarudisha kadi yao.

Hata hivyo, Dk. Slaa licha ya kukiri kuwa na kadi hiyo ya CCM hadi leo, alifafanua kuwa hiyo ni mali yake halali na ameihifadhi kwenye makumbusho kwa ajili ya kumbukumbu kwa ajili ya wajukuu zake na vizazi vijazo.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Dk. Slaa alisema madai ya Nape ni hoja ya kipuuzi isiyokuwa na tija kwa wananchi na kwamba hazina mashiko, bali zimelenga kupoteza muda na wananchi.
"Kadi ni mali yangu, na nimeihifadhi kwenye makumbusho kwa ajili ya historia ya wajukuu. CCM wanaweweseka kutokana na kushindwa kwake kuisimamia Serikali yao ili kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema.

Dk. Slaa alitamba kuwa Nape na wenzake waachwe wapige mayowe, lakini mwaka 2015 ndiyo wataisoma namba. Kwamba huo utakuwa mwisho wa CCM maana CHADEMA wanaandaa mipango bora zaidi ya kuwasaidia Watanzania kimaendeleo.

“Na Tanzania itakuwa mfano mkubwa wa kimaendeleo katika utawala wa CHADEMA," alisema Dk. Slaa huku akisisitiza kwamba umasikini uliowagubika Watanzania mwisho wake ni 2015.
CCM wavurugana

Jijini Arusha vita ya makundi ya urais 2015 ndani ya CCM, imeanza kujitokeza upya baada ya kuibuka mvutano mkali kati ya Mwenyekiti wa Jumiuya ya Wanawake (UWT) mkoani hapa, Florah Zelote na mbunge wa Viti Maalum, Catherine Magige.

Licha ya Magige kutoka mkoa huo akipitia kundi la vijana, mwenyekiti wa UWT anadai kuwa mbunge huyo anajipitisha na kutoa misaada kwa lengo la kusaka ubunge kupitia jumuiya hiyo mwaka 2015.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili, zinasema kuwa Zalote alitoa madai hayo kwenye kikao cha baraza la UWT wilaya ya Arumeru Novemba 30, mwaka huu, ambapo anadaiwa kuwaeleza wajumbe kuwa Magige hana jipya kwani misaada anayotoa ni ya kutaka kujijenga ili apate ubunge kupitia jumuiya hiyo.

Kwamba Mwenyekiti huyo aliweka wazi kuwa UWT mkoani Arusha inawakilishwa bungeni mmoja tu, Namelok Sokoine ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Sokoine.

Habari za ndani zinadai kuwa Zalote, alitumia kikao hicho kuwahamasisha wanawake kutohudhuria hafla ya uzinduzi wa taasisi ya Magige, iliyokuwa ikifanyika siku hiyo akidai kuwa kuhudhuria ni ‘kumpa ujiko’ mbunge huyo wa kuwania ubunge wa UWT 2015.

Akizungumza kwa simu na gazeti hili jana, Zelote alikiri kutohudhuria hafla hiyo iliyoandaliwa na Magige kutokana na kuwa na majukumu mengine ya kiofisi.

Hata hivyo alikanusha madai ya kumzungumzia Magige kwenye kikao hicho ingawa alikiri kuwa alikuwa na mwaliko wa hafla ya uzinduzi wa taasisi yake maendeleo lakini alishindwa kuhudhuria.

Alisema kuwa alitoa udhuru kupitia katibu wake ambaye alijibu barua ya mwaliko iliyofika ofisini kwake kwa kuwaarifu kuwa hataweza kuhudhuria kwani atakuwa wilayani Arumeru.

“Ninajua utawala bora na ninauheshimu sana, sijamtaja Magige popote, hata wakati wa kikao changu, nilimuongelea mwakilishi wetu wa UWT bungeni, Namelok Sokoine yeye ndiye nilimsemea kwa wajumbe kuwa kwa sasa hawamuoni kwani yuko nje ya nchi anamuuguza mama yake, lakini akirudi tutapita naye kwenye maeneo yao,” alisema.

Aliongeza kuwa ni vema Magige kama ana malalamiko afuate taratibu za chama badala ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari.

Naye Magige aliliambia gazeti hili kuwa ameamua kuzindua taasisi hiyo kwa ajili ya kusaidia jamii ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge.

Alisema kuwa akiwa ni mbunge anayetokana na CCM ana wajibu wa kutekeleza Ilani ya chama hicho jambo alilodai kuwa anaamini hata mwenyekiti huyo wa UWT anatakiwa kulifanya.

Kuhusu kugombea ubunge kupitia UWT mwaka 2015, Magige alisema hiyo ni haki yake kikatiba na akitaka hakuna wa kumzuia.



Saturday, December 1, 2012

RAIS JAKAYA KIKWETE AONGOZA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI YALIYOFANYIKA KITAIFA MKOANI LINDI LEO


Rais Jakaya Kikwete akiwahutubia wananchi katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kwenye uwanja wa Ilulu Mjini Lindi, huku wadau mbalimbali wa masuala ya mapambano ya ukimwi wakishiriki kwa kufanya maonyesho na kutoa elimu na maelezo mbalimbali yanayohusu mapambano ya ukimwi, Rais Pia ameshuhudia utiwaji saini wa msaada wa Dola za Kimarekani Milioni 308 kutoka mfuko wa Global Fund uliosainiwa kati ya Katibu katibu wa Ofisi ya rais Paniel Lyimo na Ramadhan Kijahkati Kabu Mkuu Wizara ya Fedha huku Mfuko wa Global Fund ukiwakilishwa na Christoph Benn Mkurugenzi wa mfuko huo. 
Christoph Benn Mkurugenzi wa mfuko Global Fund akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani iliyofanyika kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi.
Rais Jakaya Kikwete akipokea maandamano ya wananchi wa mkoa wa Lindi wakati wa maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani iliyofanyika mjini Lindi leo . kutoka kulia ni Mke wa Rais Mama Salma Kikwete, Mkurugenzi wa Tume ya kudhibiti Ukimwi TACAIDS Fatuma Mrisho na kushoto ni mkuu wa mkoa wa Lindi Ludovick Mwananzila
Rais Jakaya Kikwete akipokea maandamano ya wananchi wa mkoa wa Lindi wakati wa maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani iliyofanyika mjini Lindi leo . kutoka kulia ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Hussein Mwinyi, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete, Mkurugenzi wa Tume ya kudhibiti Ukimwi TACAIDS,Fatuma Mrisho. 
Rais Jakaya Kikwete akishuhudia Utiwaji wa Saini wa msaada wa dola za Kimarekani milioni 308 kwa ajili ya mapambano ya Ukimwi nchini, mkataba huo umesainiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Paniel Lyimo kushoto na Ramadhan Kijah katikati, kulia ni Christoph Benn mkurugenzi wa Mfuko wa Global Fund, waliosimama nyuma kushoto ni Mkewa Rasi Mama Salma Kikwete, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi na kulia ni Ursula Muller Mjumbe wa bodi ya The Global Fund,
Rais Jakaya Kikwete akiongozana na Mkewe Mama Salma Kikwete wakiingia kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi tayari kwa kushiriki katika maadhimisho ya siku ya ukimwi Duniani ambayo yamefanyika mkoani Lindi kitaifa.kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa TACAIDS Fatma Mrisho na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Ludovick Mwananzila
Rais Jakaya Kikwete akimuonyesha jambo Mkurugenzi wa tume ya kudhibiti Ukimwi Fatma Mrisho wakati alipotembelea mabanda mbalimbali katika maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani mjini Lindi leo.
Rais Jakaya Kikwete akipata maelezo kutoka kwa Bw.Rajab Mwenda afisa masoko wa Mpango wa damu Salama wakati alipotembelea katika banda hilo kwenye maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani mjini Lindi leo.
Baadhi ya viongozi wa Dini na waalikwa mbalimbali waliohudhuria katika maadhimisho hayo wakifuatilia kwa karibu matukio yaliyokuwa yakiendelea katika maadhimisho hayo.
Waheshimiwa viongozi wa serikali na baadhi ya wabunge wakiwa katika maadhimisho hayo kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi.
Mwakilishi wa mfuko wa bima ya Afya ya Jamii mjini Lindi NHIF Bi. Fortunata Raymond wa tatu kutoka kulia akiongoza maandamano ya wafanyakazi wa mfuko huo katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani.
Kikundi cha matarumbeta kikiongoza maandamano hayo yaliyokuwa yakipita mbele ya Rais kwenye uwanja wa Ilulu leo mjini Lindi.
Kikundi cha kuigiza kutoka mfuko wa bima ya afya ya Jamiii NHIF kikiwapa ujumbe wananchi wqa mkoa wa Lindikuhusu maambukizi ya ukimwi
Kikundi cha ngoza za asili kutoka mkoani Lindi kkitumuiza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU