
 Mwanasheria Mkuu wa Serikali JAJI FREDRICK WEREMA
Kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa itafanyika Machi 30 mwakani, Hayo 
yalisemwa jana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick 
Werema ambaye hata hivyo alisema kwamba kabla ya kura
 hiyo, "lazima daftari la kudumu la wapigakura liboreshwe kwanza" ili 
kuwapa fursa wapigakura wapya ambao hawamo kwenye daftari hilo.
"Kuboreshwa
 kwa daftari la wapigakura ni lazima kwa sababu kuna watu wengi 
wamefikisha umri wa kupiga kura tangu tulipofanya uchaguzi mkuu na 
hawamo kwenye daftari hilo, kwa hiyo hatuwezi kuwanyima fursa ya kupiga 
kura kwa sababu ni haki yao kikatiba," alisema Jaji Werema na kuongeza.
"Lakini 
lazima tujue pia kwamba kuboreshwa kwa daftari hilo kunahitaji fedha, 
kwa hiyo kuboreshwa kwake kutategemea kama Serikali itatoa fedha kwa 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kazi hiyo iweze kufanyika, 
tusipoboresha daftari tutasababisha kelele na malalamiko mengi".
Msimamo 
wa Jaji Werema ni sawa na ule wa Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva 
ambaye amesisitiza mara kadhaa kwamba tume yake haitoandaa uchaguzi 
wowote pasipo daftari la kudumu la wapigakura kuandikwa upya.
Jaji 
Werema alisema ikiwa Serikali itatoa fedha, uboreshaji wa daftari 
unaweza kukamilika ifikapo Februari 2015 na kwamba inatarajiwa 
Machi 30, mwakani kura ya maoni itapigwa kama kila kitu kitakwenda kama 
kilivyopangwa.
Alisema 
upigaji kura utatanguliwa na kampeni ambazo zitafanyika kwa siku 30 
kuanzia mwanzoni mwa Machi ili kushawishi Katiba inayopendekezwa iungwe 
mkono au kinyume chake kwa makundi yanayoipinga.
Hadi sasa gharama za kusimamia kura ya maoni kwa ajili ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa zimeendelea kuwa kitendawili.
Jana, 
Jaji Lubuva alisema asingeweza kuzizungumzia kwa kuwa yuko Dodoma kikazi
 na kuelekeza taarifa hizo zinaweza kupatikana kwa Mkurugenzi wa 
Uchaguzi, Julius Malaba.
Hata 
hivyo, alipotafutwa Malaba alisema anaweza kuzungumzia suala hilo katika
 mkutano na waandishi wa habari anaotarajia kuuitisha wiki hii.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog