ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Chama 
Mapinduzi (CCM) mkoani hapa na Diwani wa kata ya Kisesa wilayani Magu 
kwa sasa, Clement Mabina (pichani), ameuawa na wananchi wenye hasira 
kali kwa kipigo, kufuatia ugomvi wa shamba.
Kwa mujibu wa habari hizo, Mabina ambaye
 alikuwa Diwani wa Kata ya Kisesa (CCM) aliuawa kwa kushambuliwa kwa 
mawe na mapang, baada ya kutokea kutoelewana na wananchi wa eneo hilo la
 mlima ambapo alikwenda kupanda miti kwa madai kuwa lilikuwa shamba 
lake.
Mkuu wa polisi wa wilaya ya Magu (OCD) 
aliyejitambulisha kwa jina moja la Mkapa, alikiri kutokea kwa mauaji 
hayo na kudai kwamba awali ilisikika milio ya bunduki kwenye eneo la 
Kanyama kabla ya kumtuma Mkuu wa Upelelezi wa wilaya hiyo (OC CID) 
kwenda katika eneo la tukio, hivyo taarifa kamili itatolewa na polisi 
mkoani Mwanza.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya 
hiyo, Desdery Kiswaga wakati akielekea kwenye eneo la tukio hilo leo 
mchana(Jumapili), aliliambia Uhuru kuwa alipokea taarifa za kifo cha Mabina kwa 
masikitiko makubwa baada ya kusikia kauawa na wananchi wenye hasira kali
 wakati wakigombea shamba la mlima huo.
Taarifa zaidi kutoka katika eneo la 
Kanyama zimedai kuwa Mwenyekiti huyo wa CCM awamu iliyopita,leo(Jumapili) asubuhi 
alipofika kwenye eneo la mlima huo analolimiliki ambalo linadaiwa kuwa 
na mgogoro baina yake na baadhi ya wananchi wa Kanyama, wananchi walifika 
na kumhoji kwa nini anapanda miti.
Hali hiyo ilizua mabishano makali na 
kutoelewana na wananchi hao ambao baadhi walikuwa na mapanga na kuzidi 
kuongezeka huku wakimzingira.
Kutokana na hali hiyo, Mabina alifyatua 
risasi hewani kuwatawanya lakini wananchi hao walianza kumshambulia kwa 
mawe na ndipo alipojihami kwa kufyatua risasi nyingine ambazo kwa bahati
 mbaya, moja wapo ya risasi ilimpiga mtoto mmoja aliyekuwa kwenye tukio 
hilo na kusabaisha kifo chake.
Wananchi hao walizidi kumshambulia kwa 
mawe na kumjeruhi kichwani kabla ya kumuangusha chini na kumkata kwa 
mapanga na kusababisha kifo chake papo hapo.
Hadi tukienda mitamboni jana(Jumapili) mchana, 
habari kutoka ndani ya jeshi la polisi mkoani Mwanza zilisema kwamba, 
Kamanda mpya wa mkoa huo Varentin Mlowola, alikuwa katika eneo la tukio 
akiongoza timu ya askari kuwasaka wananchi hao waliojichukulia sheria 
mkononi.
Marehemu Mabina hadi anakumbwa na mauti 
hayo, alikuwa Diwani wa Kata ya Kisesa. Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa 
Halmashauri ya wilaya ya Magu na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Mwanza kwa
 kipindi cha miak mitano, kabla ya kushindwa na Dkt Anthon Diallo katika
 uchaguzi mkuu wa Chama mwaka jana.
CHANZO:CCM BLOG 
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog

