
Washington. Wanasayansi nchini Marekani wamegundua chanjo ambayo 
wanaamini itaweza kuangamiza Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa binadamu.
Katika majaribio ya chanjo hiyo, wanasayansi hao wameelezea kuwa 
imeonyesha mafanikio kwa kuangamiza kabisa virusi wanaofanana na VVU kwa
 nyani.
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limechapisha kwenye tovuti yake
 kuwa baada ya kubaini hilo sasa wamekusudia kufanya majaribio ya chanjo
 hiyo kwa binadamu.
Likinukuu taarifa iliyochapishwa kwenye jarida la kisayansi linaloitwa; 
Nature, lilimnukuu Mwanasayansi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha 
Oregon, nchini Marekani akisema walijiridhisha kuwa chanjo hiyo 
iliangamiza virusi vyote kwenye mwili wa nyani.
Virusi hao jamii yake inafanana sana na VVU wanajulikana kama Simian 
Immunodeficiency Virus (SIV) ikiwa na maana ni virusi vinavyosababisha 
upungufu wa kinga ya kujikinga na maradhi kwa nyani.
Taarifa za kisayansi zinaonyesha kwamba SIV ni virusi ambao wamekuwa 
wakienea kwa njia ya kujamiiana miongoni mwa vizazi vya nyani na 
vilibadilika baada ya kuambukizwa kwa binadamu vikawa vimezaa VVU.
Wanasayansi hao wanasema kati ya nyani 16 waliopewa chanjo hiyo, 
waliyoipa jina la Cytomegalovirus (CMV),tisa walipona kabisa maradhi ya 
SIV.
Mtaalamu wa Taasisi ya Chanjo na Jeni katika Chuo Kikuu cha Oregoni, 
ambaye alihusika kwenye utafiti huo, Profesa Louis Picker aliielezea 
chanjo hiyo kuwa ni ya kutia moyo ukilinganisha na nyingine ambazo 
zimewahi kufanyika.
“Katika chanjo nyingi ambazo ziliwahi kuonyesha mafanikio ya kuangamiza 
virusi ni kwamba kuna baadhi ya seli virusi walibakia,” alisema Profesa 
Picker, akifafanua:
“Lakini kwa chanjo hii tulichunguza sehemu nyingi nyeti katika mwili wa nyani tukagundua kwamba hakuna kirusi aliyebakia.”
Alisema chanjo yao wameiamini kutokana na uwezo wake wa kupenya maeneo 
mbalimbali ya mwili kiasi kwamba siyo rahisi kirusi kubakia.
Wanasayansi hao walisema kwa kawaida nyani ambaye ameambukizwa SIV hufa ndani ya kipindi cha miaka miwili
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog