
Polisi wamefanikiwa kumtia mbaroni mfanyabiashara tajiri wa 
madini ya Tanzanite huko Mirerani anayetajwa kuwa ndiye aliyepanga na 
kukodi watu waliomuua bilionea Erasto Msuya. 
Habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi 
zimedai kuwa mfanyabiashara huyo alikamatwa mwishoni mwa wiki na jana na
 juzi alikuwa akihojiwa na makachero.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, mfanyabiashara huyo 
ndiye aliyetoa fedha za kununulia pikipiki mbili zilizotumika katika 
mpango huo na pia alitoa fedha kwa ajili ya kununua simu mpya na laini 
mpya.
“Tumewakamata watu wametupa mwanga mzuri na huyo 
mfanyabiashara ndiye aliyetoa fedha za kununulia pikipiki na siku moja 
kabla ya tukio zilihifadhiwa nyumbani kwake,” alidokeza polisi mmoja.
Habari hizo zimedai kuwa polisi pia imewahoji 
mawakala wa kampuni za simu ambao walitumiwa kusajili laini mpya za simu
 zilizotumika kumpigia marehemu na kutumika kupanga mauaji hayo.
Pikipiki hizo mbili, zilinunuliwa siku moja kabla 
ya tukio kisha zikahifadhiwa nyumbani kwa mfanyabiashara huyo hadi siku 
iliyofuata ambapo aliwakabidhi wauaji na zote zimekamatwa.
Mahojiano kati ya mfanyabiashara huyo na Polisi 
yamekuwa yakifanyika kwa siri na katika kituo cha polisi (jina tunalo) 
na kwamba mambo ni mazuri ingawa jina lake halijatajwa.
 
 
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog