Johannesburg. Mke wa Nelson Mandela, Graca 
Machel kwa mara ya kwanza amejitokeza hadharani kuzungumzia hali ya 
kiafya ya mumewe kwamba kuna wakati anazidiwa lakini hajambo.
Graca alisema hayo jana kwenye sherehe za uzinduzi
 wa siku ya Utamaduni na Michezo ya Nelson Mandela iliyofanyika kwenye 
Kituo cha Kumbukumbu ya Rais huyo wa zamani wa Afrika Kusini.
Alieleza sababu za kuhudhuria sherehe hizo kwamba 
kubwa ni kuwashukuru kwa kuwa pamoja na kumwombea afya njema Mandela 
tangu alipolazwa hospitali Juni 8, mwaka huu.
Graca alisema pamoja na kwamba Mandela amelala 
akiugua hospitali, lakini ameendelea kutoa zawadi kwa wanajamii wote ya 
kuwaunganisha pamoja, ambayo ni michezo na utamaduni.
“Madiba kuna wakati hayuko vizuri. Wakati mwingine
 anakuwa na maumivu. Lakini hajambo,” alinukuliwa Graca akizungumza 
katika sherehe hizo.
Katika hatua nyingine mjini Pretoria, Rais Jacob 
Zuma juzi alisema kuwa hali ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini Nelson 
Mandela bado ni mbaya na hakuna mabadiliko.
Rais Zuma alisema hayo baada ya juzi (Jumatano) jioni kwenda hospitali kumjulia hali Mandela, ambapo alikuwa na msafara mkubwa.
Kiongozi huyo pia aliwaomba wananchi wa Afrika 
Kusini kutenga dakika 67 kwa ajili ya Siku ya Mandela ya Julai 18, 
ambayo ni siku yake ya kuzaliwa.
Alisema kauli mbiu ya siku hiyo ni “Chukua hatua; 
penda mabadiliko; fanya kila siku iwe siku ya Mandela kwa kujielekeza 
katika masuala ya chakula, makazi na elimu.
Wakati huohuo, kumekuwa na hali ya utulivu katika 
eneo la Hospitali ya Medi-Clinic aliyolazwa Mandela, tofauti na 
ilivyozoeleka kuwa na pilikapilika nyingi.
Kwa mujibu wa taarifa, watu wanaopita eneo hilo la
 hospitali wamekuwa wakionekana wakiwa na hali ya utulivu, huku wengine 
wakipiga picha kwenye kadi, maua, bendera, vipeperushi na mabango 
yaliyowekwa kandokando ya hospitali hiyo, yakiwa na ujumbe wa kumtakia 
nafuu ya kuumwa Madiba.
Wakati hali hiyo ikiendelea kutokea mjukuu wa 
Mandela, Mandla Mandela ameendelea kuikoroga familia hiyo, baada ya 
kuzungumza na waandishi wa habari akidai kushangazwa na mahakama 
ilivyoharakisha kesi hiyo kuhusu mvutano wa sehemu ya kuzikwa Mandela na
 siyo miaka miwili iliyopita baada ya yeye kufukua makaburi.
SOURSE: MWANANCHI
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog