![]()  | 
| Mbunge wa Singida Mashariki,Tundu Lissu akiwaonyesha waandishi wa habari miwani yake aliyodai kuvunjiwa na polisi. Lissu alipata dhamana katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati, jijini Arusha jana baada ya kukamatwa juzi. Picha na Moses Mashalla | 
Arusha/Dar es Salaam. Wabunge wanne wa Chadema, ambao waliachiwa
 na polisi kwa dhamana wamesimulia mateso waliyoyapata wakiwa rumande 
baada ya kukamatwa juzi.
                
              
Vigogo hao; Mbunge wa Mpanda Mjini Said Amour 
Arfi, Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce
 Mukya (Viti maalumu), walikamatwa juzi baada ya wao na wafuasi wa chama
 hicho kutawanywa kwa mabomu ya machozi na polisi kwenye Viwanja vya 
Soweto, Arusha.
Wabunge hao waliachiwa baada ya kujidhamini 
wenyewe huku watu wengine 65 waliokamatwa pamoja nao wakiachiwa baada ya
 kudhaminiwa.
Wote wanatakiwa kuripoti kwenye kituo hicho Julai 22, mwaka huu na wataelezwa hatma ya suala hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa 
Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja alisema jeshi lake 
linaendelea kuwasaka Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na 
Mbunge wa Arusha, Godbless Lema na kuwaonya kuwa wanatakiwa 
kujisalimisha mara moja.
Chagonja alisema Mbowe na Lema wanatafutwa kwa 
kosa la kufanya kusanyiko lisilo halali katika viwanja hivyo vya Soweto 
walipokuwa wakitaka kuomboleza vifo vya watu watatu; Judith Moshi, 
Ramadhan Juma na Amir Ally waliofariki dunia baada ya kuumizwa kutokana 
na mlipuko wa bomu, Jumamosi iliyopita.
Pia aliwaamuru Mbowe na Lema kuwasilisha mara moja
 ushahidi wa kuwahusisha polisi na shambulio la bomu na kama hawana 
imani na Polisi, basi wawasilishe ushahidi wao kwa Rais Jakaya Kikwete.
Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi 
ya Upinzani Bungeni, alilalamikia kitendo cha polisi kumwagia maji ya 
kuwasha baada ya kumkamata.
“Walinimwagia maji ya kuwasha kwa mfululizo 
nikalazimika kulala chini kifudifudi huku nikiwa nimefunika macho 
kukwepa yasiingie maji. “Kuna askari walitaka kunipiga lakini 
niliokolewa na mwenzao mmoja aliyenikinga nisishambuliwe. Kwa kweli 
ilikuwa hali ya hatari,” alisema.
Alisema polisi hao waliomkamata walivunja miwani yake kwa makusudi akisema aliikabidhi kaunta ikiwa haijavunjika.
                
              “Wakati naingia mahabusu nilikabidhi miwani yangu 
lakini ajabu wakati tukiachiwa ilikuwa imevunjika.” Alilalamikia hatua 
ya polisi kuwashambulia kwa mabomu, kuwamwagia maji ya kuwasha 
walipokuwa wakiwatawanya watu waliokusanyika Soweto akisema awali, 
waliwaruhusu.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
