Chama cha wananchi CUF kupitia katibu mkuu wa chama hicho ambae pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, kimemuhakikishia Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Tanzania , Jaji Joseph Warioba, kwamba Wazanzibari kwa umoja wao hawatokubali chochote kile ambacho kitasababisha kukosekana kwa Zanzibar yenye mamlaka kamili kitaifa na kimataifa itakayofuatiwa na mfumo mpya wa ushirikiano na Tanganyika kupitia Muungano.
Maalim Seif aliyasema hayo huko Makunduchi mkoa wa kusini Unguja 
alipokuwa akizungumza na wananchi mbali mbali kwenye mkutano wa hadhara 
wa chama hicho,amesema kutokana na matukio ya asilimia 66 ya maoni ya 
wazanzibar kutaka mamlaka kamili ya nchi yao basi hakun haja ya 
kutokuirjesha Zanzibar hadhi yake.
Kufuatia mkutano huo Maalim Seif amesema kuwa kwa sasa Zanzibar 
haiwezi tena kukubali kukosa mamlaka yake ya kuwa na udhibiti wa mambo 
ya nje na mahusiano ya kimataifa kwani imechoka na udhalilishaji 
inaofanyiwa na Tanganyika kupitia Serikali ya Muungano.
Aidha Maalim ametolea mifano mbali mbali ambayo Serikali ya Muungano 
imeilazimisha Zanzibar kujitoa katika Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC) 
mwaka 1993 pamoja na hatua ya hujuma iliyofanywa na Waziri wa Mambo ya 
Nje, Benard Membe, ya wiki iliopita ya kufuta maeneo ya ushirikiano 
yaliyohusu Zanzibar yaliyokuwa yawe sehemu ya makubaliano katika Mkataba
 wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Oman.
Sambamba na hayo Maalim Seif alitaja athari ya Zanzibar kukosa nafasi
 ya kufaidika na misaada ya kimataifa katika maeneo yote yasiyo ya 
Muungano kwani Tanganyika hutumia jina la Tanzania kujichukulia nafasi 
hiyo kwa manufaa na maslahi yake peke yake jambo ambalo limewatoa imani 
wazanzibar waliowengi kuendelea na Muungano huu uliopo sasa.
Maalim amefahamisha wazi kuwa kwa sasa Zanzibar inataka kuwa na 
Wizara na Waziri wake wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na 
haitokubali chochote chini ya hapo. Amesema kuwa “udhibiti wa mambo ya 
nje ndiyo kigezo cha nchi kukubalika na kutambulika kimataifa na 
Zanzibar inataka kurejesha mamlaka hayo na kurejesha kiti chake kwenye 
Umoja wa Mataifa”.
Facebook Comments Plugin Enhanced by Kitongoni blog
