Facebook Comments Box

Monday, February 16, 2015

MWADUI FC NA TOTO AFRICAN ZAKAMILISHA IDADI YA TIMU NNE ZILIZOPANDA LIGI KUU


MWADUI FC

Timu ya Mwadui yenye maskani yake Mwadui - Shinyanga imefanikiwa kurudi ligi kuu baada ya miaka 27 tangu iliposhuka daraja hilo. 

Timu hiyo inayofundishwa na Kocha JAMHURI KIWELU "JULIO ALBERTO" Imerudi ligi kuu baada ya kuichapa timu ya Bukinafaso kwa mabao 4-1 na kuongoza katika kundi lao kwa kufikisha point 46 kileleni huku Mshindi wa pili wakiwa wana kishamapanda Toto Africans wa Jijini Mwanza ambao nao walishinda mechi yao iliyopigwa katika uwanja wa CCM - KIRUMBA kwa kuwafunga Rhino Rangers mabao 2-0 na kufikisha point 45 baada ya kuongezwa point 3 za mechi iliyokwisha kwa vurugu ya Geita.

Kwa ujumla timu zilizopanda ligi kuu ni nne ambazo ni AFRICAN SPORTS(TANGA), MAJIMAJI(SONGEA), MWADUI FC(SHINYANGA) na TOTO AFRICANS(MWANZA). Ligi ya msimu ujao itakuwa na timu 16 baada ya kupanda hizo nne na kushuka timu mbili.




Saturday, February 14, 2015

HUU NDIO UKWELI KWA YANAYO ENDELEA AMBONI TANGA

Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo Paul Chagonja ametoa maelezo ya kile kinachoendelea Tanga. Kumekuwa na maneno mengi katika mitandao ya kijamii kuhusu yanayo endelea huko Tanga. Hii imepelekea Kamishna huyo kutoa taarifa

Katika taarifa yake ameelezea kuwa manamo tarehe 26 mwezi wa kwanza mwaka huu majira ya saa tano usiku polisi wakiwa katika doria walivamiwa na majambazi na kuporwa silaha na kujeruhiwa.Polisi wakishirikiana na Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) walifanya upelelezi na kugundua zilipofichwa silaha walipofika eneo la tukio ndio yakatokea majibizano ya risasi kati ya majambazi na polisi. Majibizano hayo ya risasi yamewajeruhi askari sita na mpaka sasa msako unaendelea.

Hapa chini ni taarifa ya Kamishna Chagonja





TAMBWE WA KIMATAIFA: APIGA MBILI ZILIZOIPA YANGA USHINDI DHIDI YA BDF YA BOTSWANA

Amis Joselyn Tambwe akishangilia goli lake pamoja na Simon Happygod Msuva
YANGA Leo ndani ya Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam imeichapa Klabu ya Botswana BDF XI Bao 2-0 katika Mechi ya Kwanza ya Raundi ya Awali ya Mashindano ya CAF ya Kombe la Shirikisho.
 
Bao zote za Yanga zilifungwa na Straika wao Amisi Tambwe anaetoka Burundi moja katika kila Kipindi.
Tambwe akishangilia goli lake na Mrisho Ngassa na Msuva ambao ndio wapishi wa magoli yake.

Tambwe alifunga Bao la Kwanza Dakika ya Kwanza tu ya Mchezo alipounganisha kwa Kichwa Krosi ya Simon Msuva na kupiga Bao la Pili katika Dakika ya 55 pia kwa Kichwa baada ya Krosi safi ya Mrisho Ngassa.
Mrisho Ngassa akichanja mbuga


Timu hizi zitarudiana huko Botswana Wiki mbili baadae na Mshindi wake atatinga Raundi ya Kwanza kucheza na Mshindi kati ya Sofapaka ya Kenya na FC Platinum ya Zimbabwe.
Hapo Kesho Jumapili, Mabingwa wa Tanzania Bara, Azam FC, watakuwa kwao Azam Complex huko Chamazi kwenye Viunga vya Jiji la Dar es Salaam kuivaa El Merreikh ya Sudan katika Mechi ya Raundi ya Awali ya CAF CHAMPIONZ LIGI.
Timu nyingine mbili za Tanzania ambazo pia zimo michuano ya CAF Barani Afrika ni KMKM na Polisi, zote za toka Zanzibar, Wikiendi hii zinaanzia Ugenini kwa KMKM kucheza Sudan na Al Hilal kwenye CAF CHAMPIONZ LIGI  na Polisi kucheza Nchini Gabon na CF Mounana kwenye Kombe la Shirikisho
Mchezaji wa BDF akimfanyia rafu Haruna Niyonzima



APPLE SASA WAJA NA GARI LISILOTUMIA MAFUTA

Gazeti la Wall Street Journal linayo ripoti kuwa watengenezaji wa simu maarufu ya iPhone na kifaa cha iPad, Apple wanajishughulisha kutengeneza gari litakalotumia umeme ikiwa ni changamoto kwa kampuni ya Telsa inayotawala soko hilo kwa sasa.

Taarifa hiyo ya WSJ haijamtaja mtoboa siri hiyo zaidi tu ya kusema kuwa ni mwajiriwa wa Apple anayefanya kazi katika mradi huo.

Mtoa habari huyo ametanabahisha kuwa wapo watu mamia kadhaa wanaofanya kazi kwa siri kutengeneza gari hilo la mradi uliopewa jina la "Titan" na tayari wameshaunda muonekano unaoelekea kabisa kufanana na 'minivan'. 

Msemaji rasmi wa kampuni ya Apple alipoulizwa kuhusu hilo alikataa kuthibitisha au kukanusha taarifa hizo.

Nalo gazeti la Financial Times lina habari ambayo chanzo chake ni mtu ambaye hakutaka kutajwa, akisema kuwa wafanyakazi wa Apple wamekuwa wakitafiti kuhusu vipuri vya magari katika eneo moja huko Silicon Valley.

Waajiriwa wa hivi karibuni katika kampuni ya Apple ni pamoja na mkuu wa kitengo cha utafiti cha Mercedes-Benz katika tawi la Silicon Valley.


BREAKING NEWS: MATOKEO YA KIDATO CHA NNE HAYA HAPA

Baraza la mitihani la taifa (NECTA) wameweka matokeo ya kidato cha nne kwa wanafunzi walio maliza kidato cha nne mwaka 2014.
Haya ni baadhi ya matokeo ya shule ya Mivumoni Islamic Secondary ambao imeshika nafasi ya 20 kitaifa. Wanafunzi wa shule hiyo wamepata Distinction 18 na Merit 21. matokeo mengine ingia kwenye link hapo chini.
BONYEZA HAPA KUPATA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE

PIKIPIKI YAO YACHOMWA BAADA YA KUKWAPUA SIMU YA MWANADADA MMOJA

 Pikipiki hiyo ikiteketea kwa moto.
 Wananchi wakishuhudia pikipiki hiyo ikiteketea.
Wananchi wakipiga picha pikipiki hiyo.

Kamera yetu mtaani:

Wizi wa kukwapua kwa kutumia Pikipiki umeshamiri sana Jijini Dar es Salaam kwa watumiaji hao wa pikipiki kukwapua vifaa kama simu za mikononi, mabegi ya wanawake maarufu kama "vipima joto", laptop na vitu kama hivyo.

Kuna vijana wawili waliwahi kuchomwa moto baada ya kutimiza siku zao arubaini kama msemo usemavyo kuwa "Za Mwizi arubaini" katika maeneo ya Tabata-Liwiti.

Hali hiyo ilitokea tena katika maeneo ya Hospitali ya Ocean Road ambapo wataalamu hao wa kuiba kwa pikipiki walipokutwa na zahma hiyo baada ya kumkwapulia simu mwanadada mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja na wao kukimbia ndipo msamaria mmoja akawakimbiza kwa gari lake na watu hao kuzidiwa ujanja na kukamatwa katika eneo hilo na pikipiki yao kuchomwa moto kama inavyoonekana pichani.






Friday, February 13, 2015

TFF YAIPA MATUMAINI MAKUBWA TOTO KURUDI LIGI KUU KWA KUIPA USHINDI DHIDI YA GEITA

Baraka-Kizuguto_3a74e.jpg
Afisa Habari wa TFF Baraka Kizuguto

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imethibitisha ushindi wa pointi 3 na mabao matatu kwa timu za Majimaji na Toto Africans baada ya mechi zao za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuvurugika kutokana na sababu mbalimbali.

Toto Africans imepewa ushindi huo kwa mujibu wa Kanuni ya 41(3) ya FDL baada ya vurugu za washabiki wa Geita Gold kusababisha mechi hiyo iliyochezwa Februari 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita kuvunjika dakika ya 12.

Pia Kamati hiyo iliyokutana Dar es Salaam jana (Februari 12 mwaka huu) imezuia mechi za FDL kuchezwa kwenye uwanja huo ambao hauna uzio wa kutenganisha wachezaji na washabiki kwa sababu za kiusalama.

Naye mchezaji Venance Joseph wa Geita Gold ambaye alimpiga kichwa refa akipinga adhabu ya penati iliyotolewa dhidi ya timu yake kwenye mechi hiyo amesimamishwa wakati akisubiri kosa lake kusikilizwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Malalamiko ya Friends Rangers kwenye mechi dhidi ya Majimaji yametupwa na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kusababisha mchezo huo uliochezwa Januari 29 mwaka huu Uwanja wa Majimaji mjini Songea kuvunjika dakika ya 39. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 28(4) ya FDL.

Friends Rangers imepoteza mechi hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 28(1) ya FDL, Majimaji kama ilivyo Toto Africans imepewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu.

Naye Kocha wa Friends Rangers, Herry Chibakasa (Mzozo) suala lake limepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF ili aweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni ya 39(8) ya FDL kwa kuhamamisha vurugu kwenye mechi dhidi ya Majimaji.

Mwamuzi John Mafuru wa Mbeya aliyechezesha mechi ya Majimaji na Friends Rangers amefungiwa miezi 12 (kumi na mbili) kwa kutozingatia sheria kiasi cha kuvuruga mchezo. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 37(1) ya FDL.

Pia Kamishna wa mechi hiyo Kim Rajab wa Dodoma amefungiwa miezi 12 (kumi na mbili) kwa mujibu wa Kanuni ya 38(1) ya FDL kwa kutoa taarifa zisizo sahihi.

Lipuli ya Iringa imepewa ushindi wa mabao matatu na pointi tatu baada ya timu ya KMC (Tessema) kumchezesha mchezaji Morris Paulo Katumbo aliyekuwa na kadi tatu za njano kinyume na Kanuni ya 41(12) ya FDL. Katumbo ambaye alipata kadi hizo kwenye mechi namba 85, 100 na 112 alicheza mchezo huo uliomalizika kwa timu ya KMC kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)


Tuesday, February 10, 2015

RAIS KIKWETE ALIPOFANYA MAZOEZI YA KUTEMBEA ASUBUHI





RAIS KIKWETE ZIARANI KILIMANJARO LEO

Jengo jipya la kisasa la kitega Uchumi la Mfuko wa Hifadhi ya Jami NSSF mkoani Kilimanjaro

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Kikwete leo anatarajia kuanza ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Kilimanjaro ambapo miongoni mwa shughuli anazotazamiwa kufanya ni pamoja na
kufungua jengo la kitega uchumi la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Mbali na ufunguzi huo Rais Kikwete pia anatarajia kufungua jengo la Upasuaji na kuweka jiwe la msingi katika jengo la wodi ya wazazi na watoto katika hosptali ya rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro ,Mawenzi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ,mkuu wa mkoa huo Leonidas Gama alisema Rais Kikwete atawasili mkoani humo leo jioni majira ya saa 11:00 jioni ambapo atapokelewa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kuelekea Ikulu ndogo kwa ajili ya kupokea taarifa ya Mkoa.

Alisema Kesho (February 10) Rais Kikiwete atafanya shughuli katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ikiwemo ufunguzi wa jengo la Upasuaji (Theater) ambalo limekuwa tatizo la muda mrefu katika hosptali hiyo.

“Kwanza kama mnavyo fahamu tumekuwa na tatizo la muda mrefu ya wodi ya upasuaji katika hospitali yetu ya Mawenzi,lakini kwa juhudi zilizofanywa na serikali na ushirikiano wa wadau mbalimbali lile jengo

la Upasuaji limekamilika na liko katika kiwango kizuri kwa hiyo shughuli ya kwanza atakuja kulifungua rasmi jengo la upasuaji.”alisema Gama.

Gama alisema pia Serikali tayari imefanya juhudi za kujenga jengo jipya la Wodi kwa ajili ya Wazazi na Watoto katika hosptali hiyo na kwamba Rais Kikwete ataweka rasmi jiwe la msingi kwa ajili ya muendelezo wa ujenzi wa jengo hilo.

Alisema kwa mujibu wa ratiba shughuli ya mwisho anayotazamia kufanya Rais Kikwete ni ufunguzi rasmi wa jengo la kitega Uchumi la NSSF, jengo ambalo litatumika kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi .

“Ufunguzi rasmi wa jengo hili utabadilisha taswira ya mji wetu,ni jengo la kisasa lenye Hotel,Maofisi mbalimbali,Kumbi za mikutano na maduka mbalimbali makubwa kwa madogo ambayo yatahudumia wananchi wote”alisema Gama.

Gama alitoa wito kwa viongozi na wananchi wote wa mkoa wa Kilimanjaro kujitokeza kwa wingi katika ufunguzi wa jengo hilo la NSSF majira ya saa 2:00 asubuhi ambapo rais Kikwete pia atapata nafasi ya kuzungumza na wananchi.

“Lengo la Rais Kikwete kuja ni kutuunga mkono sisi wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro katika miradi yetu ya maendeleo hivyo basi tufike mapema katika maeneo hayo ili tumsubiri na tumuone rais na kumshangilia”alisema Gama.
  • Dixon Busagaga, Moshi via Michuzi Blog


TEKNOLOJIA YATUMIKA KATIKA KESI YA SHEIKH PONDA

UPANDE wa Mashikata kesi inayomkabili Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shehe Ponda Issa Ponda umewasilisha ushahidi muhimu wa mkanda wa video unaodaiwa kuonesha uhalisia wa tukio zima la kesi yake inayomkabili ya kutoa maneno ya uchochezi.

Mkanda huo wa video uliletwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, Mary Moyo na kuoneshwa na shahidi wa tano wa kesi hiyo ambaye ni askari kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi kitengo maalumu cha uchunguzi wa picha,

Aristides alieleza vigezo alivyovitumia kuitambua uhalisia wa video hiyo iliyochukuliwa Agosti 10 mwaka 2013.
Shahidi huyo akiongozwa na Wakili wa Serikali, Benard Kongola alieleza mahakamani hapo kuwa video aliichunguza na kugundua kuwa ilichukuliwa katika eneo la tukio kupitia kamera ndogo aina ya JVC na kwamba baada ya kuichunguza aliandika hati na taarifa iliyoeleza vigezo alivyovitumia
katika uchunguzi huo na yale aliyoyaona na kuyasikia katika video hiyo ambayo aliitoa mahakamani kama kielelezo.
Pamoja na ushahidi wake, lakini pia aliionesha video hiyo mahakamani hapo ambapo ilionesha tukio zima pamoja na maneno aliyoyatoa Shehe Ponda ambayo yanadaiwa kuwa yalikuwa ya uchochezi na yaliyoumiza imani ya dini nyingine.
Shahidi huyo pia alitoa kamera, DVD, hati na taarifa ya uchunguzi wa video hiyo kama kielelezo na kupokewa na mahakama hiyo.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna msaidizi wa Polisi, Faustine Shilogile alikuwa shahidi wa nne katika kesi hiyo ambaye alieleza kuwa baada ya kupata taarifa za kutafutwa kwa Shehe Ponda kufuatia tuhuma mbalimbali zilizomkabili yeye kama kiongozi wa jeshi la polisi
mkoa aliandaa askari kwa ajili ya kumkamata baada ya kufika mkoani Morogoro.

Shahidi huyo alidai kuwa taarifa hizo za kiintelijensia zilimhusisha Ponda na tuhuma za kumwagia tindikali wasichana wawili raia wa Uingereza huko Zanzibar na tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi jijini Dar es Salaam na kwamba tuhuma hizo alizipata wakati akiwa kwenye adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja ambapo pia alitakiwa kutofanya kosa lolote katika kipindi hicho cha mwaka mmoja.

Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Juma Nasoro ulimuuliza maswali shahidi huyo, hata hivyo baadhi ya watu waliokuwepo mahakamani hapo walishindwa kuzuia vicheko vyao kutokana na aina ya maswali yaliyokuwa yakiulizwa pamoja na majibu yaliyokuwa yakitolewa.

Wakili wa utetezi: “Je wewe ulijuaje kama Shehe Ponda alitoa maneno ya uchochezi?”

Shahidi: “Niliambiwa na OCD wangu kupitia radio call (simu ya upepo) kwani alikuwepo eneo la tukio.”

Wakili: “Je, unayajua mashitaka yanayomkabili Shehe Ponda?”

Shahidi: ”Siyafahamu kwa kuwa mimi sio muandaaji wa hati ya mashitaka.”

Wakili: “Ni askari wangapi uliwaandaa kumkamata Shehe Ponda?”

Shahidi: “Sikumbuki”

Wakili: “Je, hukuandaa askari 25 hadi 30 kwa ajili ya kumkamata Shehe Ponda? “

Shahidi: “Wewe ndio utakuwa umeeleza hiyo idadi”

Wakili: ”Je, askari wako walikuwa na silaha na kama walikuwa nazo tunaweza kuamini kuwa wao ndio waliomjeruhi Shehe Ponda?”

 Shahidi: “Ndiyo baadhi ya askari wangu walikuwa na silaha lakini siwezi kufahamu Shehe Ponda
alijeruhiwa na nini.”

Wakili: “Je, unajua kama Msemaji wa Polisi, Advera Senso alitoa taarifa kuwa kuna askari alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi?”

Shahidi: “Sina taarifa na kama alitoa taarifa hizo basi ni yeye na sio mimi.”

Wakili: “Je, kibali cha kufanya kongamano kilitolewa na nani na je uliambiwa kama Shehe Ponda ni mzungumzaji katika kongamano hilo?”

Shahidi: “Kibali kilitolewa kwa OCD na sikuwa na taarifa kama Shehe Ponda atakuwa mzungumzaji.”

Awali, upande wa mashtaka ulipanga kusikiliza mashahidi watano hata hivyo mahakama ilishindwa kuendelea kusikiliza mashahidi wengine watatu kutokana na muda kuwa umekwisha hivyo mashahidi hao watatu wataendelea kusikilizwa leo Februari 10 katika mahakama hiyo.

Hata hivyo, kesi imeendelea kuvuta hisia za wakazi wengi wa mkoa wa Morogoro na maeneo mengine huku hali ya ulinzi katika viwanja vya mahakama hiyo ikiwa imaimarishwa na kufikia hatua ya kuweka vifaa maalumu vya kuwakagua watu wanaoingia katika mahakama hiyo.

 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU