Facebook Comments Box

Friday, January 11, 2013

LISSU: HAKUNA SABABU YA BAADHI YA WATU KUWA JUU YA SHERIA

Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu akiwaeleza waandishi wa habari kuwa Chama chake kimependekeza kuwepo kwa utawala wa majimbo utakaorahisisha shughuli za maendeleo kwa wananchi Picha na Salhim Shao 
Kwa ufupi
“Pia kinga ya Rais inatakiwa kuondolewa ili kuleta nidhamu ya utendaji katika ofisi hii ya umma. Akifanya makosa ya jinai ashtakiwe kama mhalifu mwingine, hakuna sababu ya baadhi ya watu kuwa juu ya sheria, kila mtu awe chini ya sheria,”


MCHAKATO wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi yatakayosaidia katika uundwaji wa Katiba Mpya unaendelea na safari hii ni zamu ya makundi maalumu vikiwemo vyama vya siasa ambavyo vimeanza kutoa maoni yao mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mikutano hiyo kati ya Tume na wawakilishi wa vyama vya siasa inafanyika katika Ofisi Kuu za Tume pamoja na Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Vyama vyote vimepewa fursa ya  kushiriki katika utoaji maoni na baadhi ya mambo ambayo wameyapendekeza kuwamo katika Katiba Mpya ni pamoja na utawala wa majimbo na kuwapo kwa mgombea binafsi.
Kimsingi hoja hizi zimekuwa zikitolewa maoni mara nyingi na wananchi katika mikutano mbalimbali ya Tume iliyokuwa ikifanyika nchi nzima kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, tofauti na sasa ni kwamba wanasiasa wamezieleza kwa undani zaidi na kuzifafanua namna gani zinavyoweza kuingia katika Katiba ijayo.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimejikita zaidi katika muundo wa Muungano na utawala wa majimbo, wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejielekeza kwenye hoja ya mgombea binafsi.
Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu anasema kuwa chama chake kinataka kuona Katiba Mpya inakuja na mfumo mpya ambao utaleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali zikiwamo utawala, rasilimali, ulinzi wa mali za umma, haki za binadamu, uwajibikaji serikalini na muundo wa Jamhuri ya Muungano ambao utasaidia kuunusuru usivunjike.
Lissu anasema kuwa kuna kila sababu ya Katiba Mpya kuleta mabadiliko katika muundo wa Muungano ambao Chadema wanapendekeza uwe Muungano wa Shirikisho wa Serikali tatu, yaani Serikali ya Jamhuri ya Tanganyika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ndogo ya Jamhuri ya Muungano.
“Hatuwezi kuendelea na mfumo uliopo wa Muungano kwani una upungufu mwingi. Ni fursa nzuri ambayo tumeipata ya kutengeneza Katiba Mpya ya nchi ambayo kimsingi inapaswa kuleta mabadiliko yatakayounusuru au kuuokoa Muungano usivunjike. Tukikosea tunaweza kujikuta tunatengana kama ilivyo kwa Ethiopia na Eritrea, Sudan na Sudan Kusini, Yugoslavia na Czechoslovakia,” anasema Lissu.
Pia anasema kwa kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni wa hiari kunatakiwa kuwe na haki ya kujitoa kwa upande usioridhika kuendelea kuwa kwenye Muungano.
Anasema utaratibu wa kujitoa uwe kwa njia ya kura ya maoni itakayopigwa na wananchi wa upande mmojawapo wa Muungano na ikiwa theluthi mbili ya wananchi wakikubali kujitoa basi iruhusiwe wajitoe kwa sababu Muungano huu haukuwa wa lazima.
Lissu anaongeza kuwa kwenye mambo ya Muungano wamependekeza yawemo mambo saba tu ambayo ni ulinzi na usalama, wizara zisizozidi 18, Bunge lisilozidi wawakilishi 300, mamlaka ya uteuzi ya Rais ambayo yanapaswa kupunguzwa, Rais ashtakiwe akifanya makosa ya jinai, pamoja na kuweka bayana suala la umilikaji wa rasilimali za nchi.
Kuhusu mamlaka ya uteuzi ya Rais anaeleza kuwa ni lazima yapunguzwe ili kuiondoa nchi kwenye mfumo wa urais wa kifalme.


POLISI WAKAMATWA WAKISAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA



Picha hii na Maktaba.

ASKARI polisi wawili wa wilayani Bunda, mkoani Mara, wanashikiliwa na jeshi la polisi katika mkoa wa Simiyu, kwa tuhuma ya kusafirisha madawa ya kulevya aina ya mirungi.

Kamanda wa polisi mkoani Simiyu Salum Msangi, amesema kuwa tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 7:30 mchana, katika kizuizi cha polisi kilichoko katika eneo la wilaya ya Busega, karibu na mji mdogo wa Lamadi, kwenye barabara kuu ya Mwanza-Musoma.

Kamanda Msangi amewataja asakari polisi hao kuwa ni pamoja na mwenye namba E. 4640 koplo Daniel na E. 6224 Koplo Mwinyihaji, na kwamba walikamatwa wakiwa na mirungi yenye uzito wa kilo 72 iliyokuwa imewekwa kwenye mabegi mawili.

Alisema kuwa askari hao walikuwa na gari binafsi yenye namba T. 168 DWB, aina ya Noah, ambapo pia walikuwa na wanawake wawili, Achien Aoko (30) na Penina Samson (20), ambao wote ni wakazi wa wilayani Tarime.

Aidha, alisema kuwa baada ya askari hao ambao walikuwa wamevaa kiraia kufika katika kizuizi hicho, gari yao ilipekuliwa na askari, na ndipo ikagundulika kwamba kulikuwa na mabegi mawili ya mirungi.

Kamanda Msangi alisema kuwa askari hao tayari wanaendelea na mashitaka ya kijeshi, ambapo wanawake waliokuwa nao jana wamefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Bariadi ambayo kwa sasa inafanya kazi kama mahakama ya mkoa wa Simiyu.




KESI YA DK. ULIMBOKA: MTUHUMIWA J. MULUNDI AMTAKA BALOZI WA KENYA KORTINI




Dk. Stephen Ulimboka baada ya kipigo kikali kutoka kwa J. Mulundi


Raia wa Kenya, Joshua Mulundi (21) anayekabiliwa na mashitaka ya kumteka na kutaka kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka, ameiomba Mahakama kumleta Balozi wa nchi yake mahakamani.

Mulundi alitoa ombi hilo jana mbele ya Hakimu Agnes Mchome wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya upande wa mashitaka kudai kuwa upelelezi wa kesi yake bado haujakamilika. Alihoji kwa nini upelelezi wa kesi hiyo unachelewa kukamilika na kwa nini upande wa mashitaka hawaleti mashahidi mahakamani ili kesi hiyo iishe?

Hakimu Mchome alisema jambo hilo liko nje ya uwezo wa Mahakama hiyo kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, isipokuwa Mahakama Kuu.

Mulundi aliiomba Mahakama kushinikiza Balozi wa Kenya aende mahakamani, huku akidai ameshaanza mgomo mahabusu na ataendelea nao. Hakimu Mchome alisema Mahakama hiyo haina uwezo wa kumshinikiza balozi wa nchi yake kufika mahakamani, lakini anaweza kufuata utaratibu kwa yeye kumuandikia Balozi wake barua.

Hata hivyo Mulundi hakuridhika na majibu hayo na kuomba apelekwe kwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mugeta ili akawasilishe malalamiko. Alitolewa katika chumba cha Hakimu Mchome na kupelekwa ofisini kwa Hakimu Mugeta ambako alidai upelelezi wa kesi yake unacheleweshwa.

Hata hivyo Hakimu Mugeta alisema Mahakama haina uwezo wa kuharakisha Polisi kukamilisha upelelezi kwa sababu kesi hiyo iko chini ya Polisi.

Hakimu Mchome ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 23 mwaka huu itakapotajwa tena. Upande wa mashitaka uliwasilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka.

Alipotoka mahakamani, Mulundi alikuwa anachechemea hasa mguu wa kushoto kitu ambacho kilisababisha ashuke kwa taabu katika ngazi za Mahakama. Pia alionesha sura ya huzuni, lakini Ofisa Magereza waliokuwa naye walishangaa na kudai alitoka mahabusu akitembea vizuri.

Inadaiwa kuwa, Juni 26 mwaka jana, katika eneo la Leaders Club, Mulundi alimteka Dk Ulimboka. Katika shitaka la pili anadaiwa Juni 26 mwaka jana, akiwa katika eneo la Msitu wa Mabwepande Tegeta, Dar es Salaam, kinyume cha sheria inadaiwa alijaribu kumsababishia kifo Dk Ulimboka. Kwa mara ya kwanza mshitakiwa huyo alipandishwa kizimbani mahakamani hapo Julai 13 mwaka jana.







Thursday, January 10, 2013

HAWA NDIO WANAFUNZI WALIONGOZA (VICHWA ) WALIOMALIZA DARASA LA SABA


Picture
Wanafunzi walioongoza mtihani wa taifa wa darasa la saba wa mwaka 2012, Janeth Kijazi (kushoto) Justina Kalala (katikati)na Kellen Mudogo wakiwa shule ya sekondari ya wasichana, St Marian Bagamoyo, jana, walikoanza kidato cha kwanza. Wanafunzi hao walihitimu elimu ya msingi katika Shule ya Tusiime ya jijini Dar es Salaam. (Picha: Florence Majani)



MGAO WA UMEME HAUPO NA HAUTAKUWEPO - PROF: MUHONGO


Picture


Wednesday, January 9, 2013

SALAMA NA SAJUKI NDANI YA MKASI




CCM WAKANUSHA TUHUMA ZA BAVICHA


 Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye  
---
 
SIKU moja baada ya Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), kudai CCM inashirikiana na baadhi ya viongozi wake kukisaliti chama hicho, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amekanusha tuhuma hizo.Nape alisema CCM haihusiki na mgogoro wowote ndani ya chama hicho, hivyo wanapaswa kumtafuta mchawi wao siyo kukilaumu chama chake.

“Mchawi wanaye wenyewe ndani ya chama chao, hatuhusiki na lolote hivyo wanapaswa kujipanga na kuulizana kubaini tatizo linalowasumbua,” alisema.

Aliongeza kuwa CCM haina muda wa kuhujumu chama hicho, ila wana muda wa kutekeleza ilani za chama maeneo mbalimbali nchini.

Nape alisema kutokana na hali hiyo, CCM imejipanga kuhakikisha ahadi zinatekelezwa kwa vitendo, ikiwamo maazimio yaliyotolewa kwenye mkutano mkuu wa chama hicho.Baadhi ya viongozi wa Bavicha wanaodaiwa kushirikiana na CCM kudhooficha Chadema na wengine walifukuzwa uanachama


SAKATA LA BASHE NA MEMBE LAFIKIA PATAMU

Picture
Bernard Membe (Mb, W)

MGOGORO wa makada wawili wa CCM; Benard Membe na Hussein Bashe umechukua sura mpya, baada ya mbunge huyo wa Mtama, kukiomba chama hicho tawala kuingilia kati ili kuupatia suluhu.

Mvutano wa Bashe na Membe ulianza wakati wa kampeni za uchaguzi wa ndani wa CCM hasa uchaguzi wa NEC baada ya Bashe kumtuhumu Membe kwa mambo mbalimbali ikiwamo kukigawa chama.

Kauli hiyo ya Bashe ilimkera Membe ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akisisitiza kuwa atamshughulikia mwanasiasa huyo chipukizi wa CCM ili amtambue.

“Nitashughulika na Bashe ndani ya chama kwa maana ya kumfikisha kwenye kamati zetu, ili ayaeleze vizuri ambayo amenipakazia na kunichafua sana… Lakini mambo mengine ambayo yamekaa kijinai sasa hayo ndiyo nitakayoyapeleka mahakamani,” alisema Membe baada ya taarifa hizo.

Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa Membe amemwandikia barua Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula kumwomba amtake Bashe athibitishe kauli zake mbalimbali dhidi yake.

Moja ya mambo Membe anamtaka Bashe ayathibitishe ni kwamba waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuwahi kusema kuwa akiwa Rais, atawafukuza watu kumi na moja nchini ambao anaamini kuwa siyo Watanzania, “Barua hii ina tuhuma nyingi, lakini kikubwa mheshimiwa huyo (Membe) amekiomba chama kimtake Bashe athibitishe tuhuma zake dhidi yake, ikiwamo hili la kuwafukuza Watanzania 11,” kilidokeza chanzo chetu cha habari ndani ya CCM.

Chanzo hicho kimeeleza kuwa baada ya makamu mwenyekiti huyo kupata barua ya Membe, ameipeleka katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa hatua zaidi. Habari zimeeleza kuwa tayari Kinana ameifanyia kazi barua hiyo kwa kumwandikia barua Bashe ili ajibu tuhuma zinazomkabili ifikapo kesho Januari 10.

Nakala ya barua hiyo ya Kinana imetumwa kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega ambako Bashe anatokea akiwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa kupitia wilaya hiyo, “Tayari Bashe ameandikiwa barua na CCM kumtaka ajibu malalamiko hayo ya mwenzake Membe,” kilieleza chanzo hicho cha habari.

Membe hakupatikana kwa siku tatu mfululizo, ili azungumzie suala hilo baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana na taarifa zilizopatikana ofisini kwake, zimeeleza kuwa yuko likizo jimboni kwake Mtama, Lindi.

Bashe hakuthibitisha wala kukanusha kupata barua hiyo ya CCM inayomtaka ajibu madai ya Membe, badala yake akasema: “Membe aliahidi kunishughulikia na mimi ninangoja anishughulikie.”

Mangula alipotafutwa juzi kuzungumzia suala hilo alisema asingeweza kusema chochote kwa kuwa alikuwa hajafika ofisini tangu alipokwenda kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, “Sijajua chochote kilichoendelea ofisini kwa sababu nilikuwa kijijini kwangu kwa ajili ya Sikukuu ya Krimasi na Mwaka Mpya. Nikiingia ofisini naweza kuwa katika nafasi ya kujua kilichoendelea,” alisema Mangula. Hata hivyo, alipopigiwa simu jana, iliita bila kupokewa na baadaye ikazimwa kabisa.

Kinana naye hakupatikana jana baada ya simu yake pia kuita na kupokelewa na mtu mwingine mara kadhaa ambaye alieleza kuwa alikuwa mkutanoni siku nzima.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alijibu kwa kifupi na kukata simu,” Sijapata wala kuona barua ya malalamiko ya Membe kwa Bashe.”

Novemba 10, mwaka jana Bashe akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, alimtuhumu Membe akidai kuwa ndiye anayehusika na vipeperushi vya kumhujumu mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete vilivyokuwa vimetawanywa na watu wasiojulikana siku chache kabla ya uchaguzi wa mwenyekiti na nafasi nyingine kufanyika.


HII NDIO SIRI YA FAST JET KUWA NA BEI RAHISI


Bei ya nauli ya chini ya fastjet yafafanuliwa
Tunajivunia kuwa shirika la kwanza la ndege linalotoa huduma kwa gharama nafuu kabisa.
Mfumo huu wa gharama nafuu katika mashirika ya ndege umekuwa maarufu sana ndani ya mabara ya Ulaya, Asia na Marekani kwa zaidi ya miaka 10. Kwa uhakika, Easyjet, ni moja kati ya mashirika ya gharama nafuu na ni shirika kubwa sana katika bara la Ulaya (ambaye mwanzilishi wake na mwanahisa mkubwa wa fastjet) na kubeba zaidi ya abiria milioni 55 ndani ya mwaka huu

Ni jinsi gani tunaweza kupata nauli chini mno?

Kuna njia kuu tatu tunazotumia kuwezesha nauli za ndege kuwa chini. Kwanza, tunaajiri watu wajanja na werevu, tunatumia mifumo na mikakati ambayo hupunguza gharama na kuongeza ufanisi wa kazi – hii hufanyika nyuma ya pazia na hutoweza kuona ikifanyika. Pia tunanunua sarafu yetu na mafuta ya ndege kabla, ili kuweka gharama zetu chini. Pia tunazingatia kwenye aina moja ya ndege, ambayo ni Airbus 319 katika kampuni yetu, hii inapunguza gharama pia kwani tuna aina moja ya vipuri na wataalamu wa ndege.
Njia mbili zingine utakazo zigundua, Kwanza, tunatumia mbinu ya 'lipia unachotumia' katika usafiri wetu wa anga.

Hii inamaanisha abiria analipia anachotumia wakati wa safari na si zaidi.

Unapolipia tiketi zetu unakuwa umelipia pamoja na siti kwenye ndege na mizigo moja wa kubeba mkononi. Kila kitu kingine cha ziada kwanzia gharama ya mizigo hadi vinywaji -  vitalipiwa kwa kutumia Mfumo wa” kulipa-kwa-matumizi”. Kama unataka chakula unaweza kulipa, na kama huhitaji chakula huna haja ya kukilipia. Katika mashirika mengine ya ndege unalazimika kulipia huduma ambazo hata hutotumia, mfano unakuta ndege zingine zina madaraja na huduma za gharama, lakini kwa fastjet tunatoa bidhaa zetu kwa gharama rahisi sana unaweza kulipia huduma Fulani kama unaitaka, kama huduma ya basi.
Njia ya tatu na mwisho tunayotumia kuifanya nauli yetu iwe chini ni kwa kuweka madaraja katika nauli zetu. Nauli zetu zinapatikana kati ya dola $ 20-150: Fanya mipango yako ya safari mapema, upate nauli ya chini. Hii inatusaidia kujaza ndege zetu (ni zaidi ya gharama nafuu) pia tunawapa fursa wateja wetu kupata bei nafuu sana, kinachotakiwa ni kufanya maandalizi ya safari mapema. Tumekuwa sana katika soko la Tanzania na tumefanikiwa kuwapa fursa maelfu ya watu ambao hakuwahi kusafiri kwa anga.
Mfumo wa Gharama nafuu ni muhimu sana kwa fastjet. Nauli zetu si tu za utangulizi, tunaahadi kuwa na nauli nafuu kadri tuwezavyo na kwa muda mrefu. Lengo letu ni kuanzisha aina ya usafiri wa anga wa gharama nafuu katika bara la Afrika kama ambavyo mabara ya Ulaya na Marekani wamekuwa wakifurahia huduma hii kwa miaka mingi.
Kusafiri kwa anga si tu kwa ajili ya matajiri na watu maarufu, Mfumo wetu wa nauli ya chini ina mpa kila mmoja fursa ya kusafiri kwa anga.

Tunapenda kuuita "Usafiri Makini"



Tuesday, January 8, 2013

BIRTHDAY YA KHAYRAT

Mtoto wa mmoja wa wadau wa Kitongoni Blog akijiandaa kukata keki katika sherehe yake ya kuadhimisha mwaka mmoja

Keki ya Khayrat ikiwa tayari kwa shughuli

Khayrat akiwa amebebwa na babu yake Injinia Yusuf Kabange



WATEJA WAKUU WA WANYAMAPORI NI VIGOGO SERIKALINI


RIPOTI MAALUMU ya gazeti la JAMHURI

Kipindi cha uwindaji kinachoruhusiwa kisheria kinachoanza Julai hadi Desemba kila mwaka kimekwisha. Hii haina maana kwamba ulaji wanyamapori umekoma.

Nipo njiani naelekea mkoani Iringa. Kilometa 40 hivi kutoka mjini Morogoro, tunafika katika eneo linaloitwa Lugano. Hapa kunachomwa nyama za kila aina, lakini zinazotawala zaidi ni za mbuzi na swala. Kwa kutambua kuwa naweza kupata nyama ya swala, najenga urafiki na wauza nyama hawa. Nao, bila hiyana wanakuwa wachangamfu kwangu.

Swali langu la kwanza kwao ni, “Naweza kupata nyama ya swala?” Mmoja wa vijana hawa anajibu, “Sema jingine kaka, nyama umepata.” Nauliza swali la pili, “Naweza kupata nyama ya nyati au aina nyingine tofauti na swala?” Najibiwa, “Hapa nyati hupati, labda uende Mkata. Mkata ndiyo kwenye kila kitu.”

Naelekezwa kwamba kutoka hapa Lugano hadi Mkata ni mwendo kama wa kilometa 10 na ushei hivi. Maneno ya vijana hawa ya kwamba Mkata ndiyo kila kitu, yananifanya niwe na shauku ya kufika katika kijiji hicho. Kweli, napanda basi tayari kuelekea Iringa. Punde si punde, kwa msaada wa kondakta na kibao cha utambulisho, napaona Mkata. Naendelea na safari yangu hadi Iringa, lakini akili yangu inanisukuma niandae siku maalumu kwa ajili ya kufuatilia taarifa hizi.

Nasukumwa na ukweli kwamba vijiji kama Lugano, Mkata na Doma vipo jirani kabisa na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. Vijiji hivi vinapitiwa na barabara kuu ya Morogoro-Iringa. Wakubwa wanapita hapa kila siku. Kama hivyo ndivyo, iweje ujangili ushamiri kwa kiasi hiki cha kutisha?

Mwishoni mwa Desemba naamua kufunga safari kutoka Dar es Salaam kwenda Mkata na Doma. Kabla ya safari nampigia simu Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Ujangili katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Faustine Masalu.

“Kamanda naelekea mkoani Morogoro kufuatilia taarifa za ujangili. Nakupa taarifa hizi kwa sababu huko naweza kukutana na mambo yasiyokuwa ya kawaida. Lakini kubwa itanipasa niweze kushiriki kununua nyamapori na hata kusafiri nayo bila kibali, kisheria nikikamatwa naweza kushitakiwa. Nakupa taarifa hii kama kinga kwa linaloweza kunipata,” huu ndiyo uliokuwa ujumbe wangu kwa Masalu, kabla ya kuanza safari kwa kutumia gari langu.

Muda ni saa tano asubuhi. Naanza safari ya kwenda Morogoro. Kwa kutambua ugumu wa kazi ninayokwenda kuifanya, namchukua mwandishi mwenzangu, Edmund Mihale.

Tunakwenda hadi Lugano. Hapa tunaegesha gari pembeni kwa ajili ya kuanza kazi. Mvua kubwa inanyesha. Majiko ya nyama ni mengi. Tunaomba tuuziwe nyamapori, lakini kwa hadaa, baadhi ya wauzaji wanatupatia nyama ya mbuzi. Wote tunashituka. Kuona hivyo, mmoja anatuelekeza kwenye jiko lake.

Kweli, tunakula nyama yenye ladha na sifa zote za swala. Kazi imeanza. Nakumbuka kwamba nilishaelezwa na hawa hawa vijana kwamba nyama za kila aina zinapatikana Mkata, mahali ambako sifa zake zinafanana na Mkata ya Handeni, mkoani Tanga, ambako kunauzwa nyama nyingi za mbuzi, lakini si swala na wanyamapori wengine.

Tunaanza safari kwenda Mkata. Si mbali. Baada ya kilometa tano hivi, tunakuta gari la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aina ya Land Rover likiwa limepinduka na kuwaumiza askari na raia waliokuwamo. Ni mali ya Kikosi cha 401.

Wanajeshi hawa walikuwa wakitoka kumzika mwenzao Kigamboni, Dar es Salaam, na sasa walikuwa njiani kurejea Songea. Kama ilivyo ada, tunashiriki kutoa huduma kwa wapiganaji na makamanda hawa. Magari mengi yanafika, yanasimama na kuuliza aina ya msaada unaotakiwa. Mwisho, majeruhi wote, isipokuwa mmoja, wanapelekwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.

Kuona hivyo, tunashawishika kuendelea na safari yetu. Vijana wawili wanaomba lifti. Nawauliza wanakokwenda. Wanajibu kwamba wao ni wakazi wa Mkata. Kusikia hivyo, haraka haraka nawakaribisha waingine katika gari. Njiani naanza kuwauliza kama wana uwezo wa kuniwezesha kupata nyama ya swala. Mmoja anajibu, “Sisi hatuuzi swala, lakini tunaweza kukupeleka kwa wanaouza.” Namwuliza kama naweza kupata aina nyingine ya wanyamapori.

“Hapo kila kitu utapata, hakuna wasiwasi,” anajibu kwa lafudhi ya Kimaasai. Baada ya kilometa kama saba hivi, tunafika Mkata. Nashangaa kuona magari mengi yakiwa yameegeshwa kando ya barabara. Nauliza kama kuna sherehe mahali hapa. Mmoja wa vijana hawa anajibu, “Siyo sherehe, watu wanakuja wote kula nyama hapa.”

Tunakwenda moja kwa moja hadi mahali kunakouzwa. Wenyeji wetu hapa hawana wasiwasi, pengine kutokana na hawa vijana wawili wenyeji waliotufikisha hapa. Tunawakuta wateja wengi wakila nyama. Jiko limejengwa ndani ya nyumba mbovu ya miti na kuezekwa kwa nyasi.

Anayechoma nyama hapa ni maarufu kwa jina la Mangi. Baadaye tunamwuliza jina lake halisi na anajitambulisha kuwa anaitwa Mrosso Anthony. Kuna nyama ya nyati, swala na pofu. Pande linauzwa kuanzia Sh 10,000. Mimi nasita kuchukua nyama kubwa, naomba atutengee ya Sh 5,000. Wateja wote tuliokutana hapa ni kama vile tulishaonana siku nyingi, maana wengine wanakata "kilaji" (bia). Wanatukaribisha tunywe. Ni katika mazingira ambayo watembezi huyaita “adventure”.

Upande wa pili wa nyumba hii, kuna nyama mbichi iliyotundikwa. Inavutia kweli kweli. Inavuja damu mbichi kabisa. Kuna miguu na mikono. Pembeni mwa hiyo nyama, kuna kijana mmoja mwenye uso uliojaa makovu. Anaitwa Pengo. Sijui kwanini anaitwa Pengo, pengine ni kutokana na kutokuwa na meno mengi mdomoni. Namwuliza; “Pengo, vipi bwana, mbona uso umeharibika, wewe ni mgomvi au ulikuwa ukipambana na nyati?” Anajibu kwa tabasamu, “Siyo nyati mkuu, hii kitu ndiyo imefanya yote haya,” anasema huku akinionesha pikipiki.

Wageni wanazidi kumiminika hapa, na nyama zinauzwa kwa kasi. Ghafla, Pengo na Mangi wanaonekana kuhamaki baada ya kuwaona wateja wengine wawili wasiowajua wakija mahali tulipo. “Wale nani?" Anahoji Mangi. Pengo anajibu, “Ni wateja tu, siyo watu wabaya.”

Nyama tuliyoilipia ipo tayari. Tunaanza kula, lakini ni ngumu. Yaelekea ni ya upande wa shingo.  Nimeshindwa kutelemka na kamera yangu kubwa. Hali hii inalilazimu nitumie kamera maalumu kupata picha za hapa na pale.

Ili nisiweze kushitukiwa, nauliza bei ya mguu wa pofu. Naambiwa kuwa bei yake ni Sh 120,000. Naomba niuziwe kipande cha Sh 20,000. Pengo anachukua mguu wa pofu. Anaupeleka nje kwenye gogo maalumu. Anakata. Kuona hivyo, walaji wenzetu nao wanaanza kununua. Wanakatiwa kadiri ya fedha zao. Wengine wanaingia wakiwa na bia zao kabisa. Nyama ni nyingi na hakuna mwenye wasiwasi.

Mwisho, nikiwa nimeshajiridhisha kuwa nyama inayouzwa ni ya pori, namwuliza Pengo wapi wanakopata nyama. “Hii nyama tunanunua kwa Waarabu wa Morogoro wanaokuja kuwinda huku.” Namwuliza, “Mbona muda wa kuwinda umekwisha?” Anakosa jibu.

Tumeshajiridhisha pasi na shaka kuwa hapa ni kwenye mnada wa wanyamapori. Tunaaga, lakini kabla ya kuondoka, Mangi anatupatia namba yake ya simu. “Chukua namba yangu ya simu, ukiwa unahitaji kabla ya kufika hapa wewe piga simu kabisa tukuandalie. Namba yangu ni 0655 093795. Karibu sana,” anasema.

Ingawa mwanzoni alinieleza kwamba jina lake ni Mrosso Anthony, usajili wa namba hii unaonesha kuwa ni ya Christian Joseph. Hii inazidi kunipa shaka.

Baada ya hapo naanza uchunguzi wa hapa na pale. Najiridhisha kuwa pikipiki iliyopo hapa ni moja ya zana zinazotumika kusafirisha nyama. Naelezwa na mmoja wa vijana kwamba pamoja na kuwapo kundi la vijana wanaoendesha ujangili, baadhi ya nyama wanazipata kutoka kwa askari wanyamapori wa Mikumi.

Wiki ijayo naendelea kueleza vituo vingine vya uuzaji wanyamapori. Ushiriki wa maofisa na askari wanyamapori katika biashara hii haramu. Je, Mkurugenzi na mwenye dhamana ya kupambana na ujangili nchini, Paul Sarakikya; Kamanda Masalu, Mkuu wa KDU (Kikosi Dhidi ya Ujangili), Majid Lalu; Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi; Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mvomero, Sarah Limuna; Ofisa Wanyamapori Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa.

Nao, Askari Wanyamapori Wilaya ya Mvomero aliyepewa dhima ya kusimamia wanyamapori eneo la Doma, Peter Mayapila; Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Paschal Shelutete; wanasemaje?  Je, kuwapo kwa huduma za mitandao ya simu hifadhini na katika mapori pamoja na kuruhusu matumizi ya bodaboda kunachangiaje wimbi la ujangili nchini?

...Usikose toleo lijalo la gazeti JAMHURI.



 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU