Facebook Comments Box

Wednesday, January 9, 2013

SALAMA NA SAJUKI NDANI YA MKASI




CCM WAKANUSHA TUHUMA ZA BAVICHA


 Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye  
---
 
SIKU moja baada ya Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), kudai CCM inashirikiana na baadhi ya viongozi wake kukisaliti chama hicho, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amekanusha tuhuma hizo.Nape alisema CCM haihusiki na mgogoro wowote ndani ya chama hicho, hivyo wanapaswa kumtafuta mchawi wao siyo kukilaumu chama chake.

“Mchawi wanaye wenyewe ndani ya chama chao, hatuhusiki na lolote hivyo wanapaswa kujipanga na kuulizana kubaini tatizo linalowasumbua,” alisema.

Aliongeza kuwa CCM haina muda wa kuhujumu chama hicho, ila wana muda wa kutekeleza ilani za chama maeneo mbalimbali nchini.

Nape alisema kutokana na hali hiyo, CCM imejipanga kuhakikisha ahadi zinatekelezwa kwa vitendo, ikiwamo maazimio yaliyotolewa kwenye mkutano mkuu wa chama hicho.Baadhi ya viongozi wa Bavicha wanaodaiwa kushirikiana na CCM kudhooficha Chadema na wengine walifukuzwa uanachama


SAKATA LA BASHE NA MEMBE LAFIKIA PATAMU

Picture
Bernard Membe (Mb, W)

MGOGORO wa makada wawili wa CCM; Benard Membe na Hussein Bashe umechukua sura mpya, baada ya mbunge huyo wa Mtama, kukiomba chama hicho tawala kuingilia kati ili kuupatia suluhu.

Mvutano wa Bashe na Membe ulianza wakati wa kampeni za uchaguzi wa ndani wa CCM hasa uchaguzi wa NEC baada ya Bashe kumtuhumu Membe kwa mambo mbalimbali ikiwamo kukigawa chama.

Kauli hiyo ya Bashe ilimkera Membe ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa akisisitiza kuwa atamshughulikia mwanasiasa huyo chipukizi wa CCM ili amtambue.

“Nitashughulika na Bashe ndani ya chama kwa maana ya kumfikisha kwenye kamati zetu, ili ayaeleze vizuri ambayo amenipakazia na kunichafua sana… Lakini mambo mengine ambayo yamekaa kijinai sasa hayo ndiyo nitakayoyapeleka mahakamani,” alisema Membe baada ya taarifa hizo.

Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa Membe amemwandikia barua Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula kumwomba amtake Bashe athibitishe kauli zake mbalimbali dhidi yake.

Moja ya mambo Membe anamtaka Bashe ayathibitishe ni kwamba waziri huyo wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuwahi kusema kuwa akiwa Rais, atawafukuza watu kumi na moja nchini ambao anaamini kuwa siyo Watanzania, “Barua hii ina tuhuma nyingi, lakini kikubwa mheshimiwa huyo (Membe) amekiomba chama kimtake Bashe athibitishe tuhuma zake dhidi yake, ikiwamo hili la kuwafukuza Watanzania 11,” kilidokeza chanzo chetu cha habari ndani ya CCM.

Chanzo hicho kimeeleza kuwa baada ya makamu mwenyekiti huyo kupata barua ya Membe, ameipeleka katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kwa hatua zaidi. Habari zimeeleza kuwa tayari Kinana ameifanyia kazi barua hiyo kwa kumwandikia barua Bashe ili ajibu tuhuma zinazomkabili ifikapo kesho Januari 10.

Nakala ya barua hiyo ya Kinana imetumwa kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nzega ambako Bashe anatokea akiwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa kupitia wilaya hiyo, “Tayari Bashe ameandikiwa barua na CCM kumtaka ajibu malalamiko hayo ya mwenzake Membe,” kilieleza chanzo hicho cha habari.

Membe hakupatikana kwa siku tatu mfululizo, ili azungumzie suala hilo baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana na taarifa zilizopatikana ofisini kwake, zimeeleza kuwa yuko likizo jimboni kwake Mtama, Lindi.

Bashe hakuthibitisha wala kukanusha kupata barua hiyo ya CCM inayomtaka ajibu madai ya Membe, badala yake akasema: “Membe aliahidi kunishughulikia na mimi ninangoja anishughulikie.”

Mangula alipotafutwa juzi kuzungumzia suala hilo alisema asingeweza kusema chochote kwa kuwa alikuwa hajafika ofisini tangu alipokwenda kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, “Sijajua chochote kilichoendelea ofisini kwa sababu nilikuwa kijijini kwangu kwa ajili ya Sikukuu ya Krimasi na Mwaka Mpya. Nikiingia ofisini naweza kuwa katika nafasi ya kujua kilichoendelea,” alisema Mangula. Hata hivyo, alipopigiwa simu jana, iliita bila kupokewa na baadaye ikazimwa kabisa.

Kinana naye hakupatikana jana baada ya simu yake pia kuita na kupokelewa na mtu mwingine mara kadhaa ambaye alieleza kuwa alikuwa mkutanoni siku nzima.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alijibu kwa kifupi na kukata simu,” Sijapata wala kuona barua ya malalamiko ya Membe kwa Bashe.”

Novemba 10, mwaka jana Bashe akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, alimtuhumu Membe akidai kuwa ndiye anayehusika na vipeperushi vya kumhujumu mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete vilivyokuwa vimetawanywa na watu wasiojulikana siku chache kabla ya uchaguzi wa mwenyekiti na nafasi nyingine kufanyika.


HII NDIO SIRI YA FAST JET KUWA NA BEI RAHISI


Bei ya nauli ya chini ya fastjet yafafanuliwa
Tunajivunia kuwa shirika la kwanza la ndege linalotoa huduma kwa gharama nafuu kabisa.
Mfumo huu wa gharama nafuu katika mashirika ya ndege umekuwa maarufu sana ndani ya mabara ya Ulaya, Asia na Marekani kwa zaidi ya miaka 10. Kwa uhakika, Easyjet, ni moja kati ya mashirika ya gharama nafuu na ni shirika kubwa sana katika bara la Ulaya (ambaye mwanzilishi wake na mwanahisa mkubwa wa fastjet) na kubeba zaidi ya abiria milioni 55 ndani ya mwaka huu

Ni jinsi gani tunaweza kupata nauli chini mno?

Kuna njia kuu tatu tunazotumia kuwezesha nauli za ndege kuwa chini. Kwanza, tunaajiri watu wajanja na werevu, tunatumia mifumo na mikakati ambayo hupunguza gharama na kuongeza ufanisi wa kazi – hii hufanyika nyuma ya pazia na hutoweza kuona ikifanyika. Pia tunanunua sarafu yetu na mafuta ya ndege kabla, ili kuweka gharama zetu chini. Pia tunazingatia kwenye aina moja ya ndege, ambayo ni Airbus 319 katika kampuni yetu, hii inapunguza gharama pia kwani tuna aina moja ya vipuri na wataalamu wa ndege.
Njia mbili zingine utakazo zigundua, Kwanza, tunatumia mbinu ya 'lipia unachotumia' katika usafiri wetu wa anga.

Hii inamaanisha abiria analipia anachotumia wakati wa safari na si zaidi.

Unapolipia tiketi zetu unakuwa umelipia pamoja na siti kwenye ndege na mizigo moja wa kubeba mkononi. Kila kitu kingine cha ziada kwanzia gharama ya mizigo hadi vinywaji -  vitalipiwa kwa kutumia Mfumo wa” kulipa-kwa-matumizi”. Kama unataka chakula unaweza kulipa, na kama huhitaji chakula huna haja ya kukilipia. Katika mashirika mengine ya ndege unalazimika kulipia huduma ambazo hata hutotumia, mfano unakuta ndege zingine zina madaraja na huduma za gharama, lakini kwa fastjet tunatoa bidhaa zetu kwa gharama rahisi sana unaweza kulipia huduma Fulani kama unaitaka, kama huduma ya basi.
Njia ya tatu na mwisho tunayotumia kuifanya nauli yetu iwe chini ni kwa kuweka madaraja katika nauli zetu. Nauli zetu zinapatikana kati ya dola $ 20-150: Fanya mipango yako ya safari mapema, upate nauli ya chini. Hii inatusaidia kujaza ndege zetu (ni zaidi ya gharama nafuu) pia tunawapa fursa wateja wetu kupata bei nafuu sana, kinachotakiwa ni kufanya maandalizi ya safari mapema. Tumekuwa sana katika soko la Tanzania na tumefanikiwa kuwapa fursa maelfu ya watu ambao hakuwahi kusafiri kwa anga.
Mfumo wa Gharama nafuu ni muhimu sana kwa fastjet. Nauli zetu si tu za utangulizi, tunaahadi kuwa na nauli nafuu kadri tuwezavyo na kwa muda mrefu. Lengo letu ni kuanzisha aina ya usafiri wa anga wa gharama nafuu katika bara la Afrika kama ambavyo mabara ya Ulaya na Marekani wamekuwa wakifurahia huduma hii kwa miaka mingi.
Kusafiri kwa anga si tu kwa ajili ya matajiri na watu maarufu, Mfumo wetu wa nauli ya chini ina mpa kila mmoja fursa ya kusafiri kwa anga.

Tunapenda kuuita "Usafiri Makini"



Tuesday, January 8, 2013

BIRTHDAY YA KHAYRAT

Mtoto wa mmoja wa wadau wa Kitongoni Blog akijiandaa kukata keki katika sherehe yake ya kuadhimisha mwaka mmoja

Keki ya Khayrat ikiwa tayari kwa shughuli

Khayrat akiwa amebebwa na babu yake Injinia Yusuf Kabange



WATEJA WAKUU WA WANYAMAPORI NI VIGOGO SERIKALINI


RIPOTI MAALUMU ya gazeti la JAMHURI

Kipindi cha uwindaji kinachoruhusiwa kisheria kinachoanza Julai hadi Desemba kila mwaka kimekwisha. Hii haina maana kwamba ulaji wanyamapori umekoma.

Nipo njiani naelekea mkoani Iringa. Kilometa 40 hivi kutoka mjini Morogoro, tunafika katika eneo linaloitwa Lugano. Hapa kunachomwa nyama za kila aina, lakini zinazotawala zaidi ni za mbuzi na swala. Kwa kutambua kuwa naweza kupata nyama ya swala, najenga urafiki na wauza nyama hawa. Nao, bila hiyana wanakuwa wachangamfu kwangu.

Swali langu la kwanza kwao ni, “Naweza kupata nyama ya swala?” Mmoja wa vijana hawa anajibu, “Sema jingine kaka, nyama umepata.” Nauliza swali la pili, “Naweza kupata nyama ya nyati au aina nyingine tofauti na swala?” Najibiwa, “Hapa nyati hupati, labda uende Mkata. Mkata ndiyo kwenye kila kitu.”

Naelekezwa kwamba kutoka hapa Lugano hadi Mkata ni mwendo kama wa kilometa 10 na ushei hivi. Maneno ya vijana hawa ya kwamba Mkata ndiyo kila kitu, yananifanya niwe na shauku ya kufika katika kijiji hicho. Kweli, napanda basi tayari kuelekea Iringa. Punde si punde, kwa msaada wa kondakta na kibao cha utambulisho, napaona Mkata. Naendelea na safari yangu hadi Iringa, lakini akili yangu inanisukuma niandae siku maalumu kwa ajili ya kufuatilia taarifa hizi.

Nasukumwa na ukweli kwamba vijiji kama Lugano, Mkata na Doma vipo jirani kabisa na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. Vijiji hivi vinapitiwa na barabara kuu ya Morogoro-Iringa. Wakubwa wanapita hapa kila siku. Kama hivyo ndivyo, iweje ujangili ushamiri kwa kiasi hiki cha kutisha?

Mwishoni mwa Desemba naamua kufunga safari kutoka Dar es Salaam kwenda Mkata na Doma. Kabla ya safari nampigia simu Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Ujangili katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Faustine Masalu.

“Kamanda naelekea mkoani Morogoro kufuatilia taarifa za ujangili. Nakupa taarifa hizi kwa sababu huko naweza kukutana na mambo yasiyokuwa ya kawaida. Lakini kubwa itanipasa niweze kushiriki kununua nyamapori na hata kusafiri nayo bila kibali, kisheria nikikamatwa naweza kushitakiwa. Nakupa taarifa hii kama kinga kwa linaloweza kunipata,” huu ndiyo uliokuwa ujumbe wangu kwa Masalu, kabla ya kuanza safari kwa kutumia gari langu.

Muda ni saa tano asubuhi. Naanza safari ya kwenda Morogoro. Kwa kutambua ugumu wa kazi ninayokwenda kuifanya, namchukua mwandishi mwenzangu, Edmund Mihale.

Tunakwenda hadi Lugano. Hapa tunaegesha gari pembeni kwa ajili ya kuanza kazi. Mvua kubwa inanyesha. Majiko ya nyama ni mengi. Tunaomba tuuziwe nyamapori, lakini kwa hadaa, baadhi ya wauzaji wanatupatia nyama ya mbuzi. Wote tunashituka. Kuona hivyo, mmoja anatuelekeza kwenye jiko lake.

Kweli, tunakula nyama yenye ladha na sifa zote za swala. Kazi imeanza. Nakumbuka kwamba nilishaelezwa na hawa hawa vijana kwamba nyama za kila aina zinapatikana Mkata, mahali ambako sifa zake zinafanana na Mkata ya Handeni, mkoani Tanga, ambako kunauzwa nyama nyingi za mbuzi, lakini si swala na wanyamapori wengine.

Tunaanza safari kwenda Mkata. Si mbali. Baada ya kilometa tano hivi, tunakuta gari la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aina ya Land Rover likiwa limepinduka na kuwaumiza askari na raia waliokuwamo. Ni mali ya Kikosi cha 401.

Wanajeshi hawa walikuwa wakitoka kumzika mwenzao Kigamboni, Dar es Salaam, na sasa walikuwa njiani kurejea Songea. Kama ilivyo ada, tunashiriki kutoa huduma kwa wapiganaji na makamanda hawa. Magari mengi yanafika, yanasimama na kuuliza aina ya msaada unaotakiwa. Mwisho, majeruhi wote, isipokuwa mmoja, wanapelekwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.

Kuona hivyo, tunashawishika kuendelea na safari yetu. Vijana wawili wanaomba lifti. Nawauliza wanakokwenda. Wanajibu kwamba wao ni wakazi wa Mkata. Kusikia hivyo, haraka haraka nawakaribisha waingine katika gari. Njiani naanza kuwauliza kama wana uwezo wa kuniwezesha kupata nyama ya swala. Mmoja anajibu, “Sisi hatuuzi swala, lakini tunaweza kukupeleka kwa wanaouza.” Namwuliza kama naweza kupata aina nyingine ya wanyamapori.

“Hapo kila kitu utapata, hakuna wasiwasi,” anajibu kwa lafudhi ya Kimaasai. Baada ya kilometa kama saba hivi, tunafika Mkata. Nashangaa kuona magari mengi yakiwa yameegeshwa kando ya barabara. Nauliza kama kuna sherehe mahali hapa. Mmoja wa vijana hawa anajibu, “Siyo sherehe, watu wanakuja wote kula nyama hapa.”

Tunakwenda moja kwa moja hadi mahali kunakouzwa. Wenyeji wetu hapa hawana wasiwasi, pengine kutokana na hawa vijana wawili wenyeji waliotufikisha hapa. Tunawakuta wateja wengi wakila nyama. Jiko limejengwa ndani ya nyumba mbovu ya miti na kuezekwa kwa nyasi.

Anayechoma nyama hapa ni maarufu kwa jina la Mangi. Baadaye tunamwuliza jina lake halisi na anajitambulisha kuwa anaitwa Mrosso Anthony. Kuna nyama ya nyati, swala na pofu. Pande linauzwa kuanzia Sh 10,000. Mimi nasita kuchukua nyama kubwa, naomba atutengee ya Sh 5,000. Wateja wote tuliokutana hapa ni kama vile tulishaonana siku nyingi, maana wengine wanakata "kilaji" (bia). Wanatukaribisha tunywe. Ni katika mazingira ambayo watembezi huyaita “adventure”.

Upande wa pili wa nyumba hii, kuna nyama mbichi iliyotundikwa. Inavutia kweli kweli. Inavuja damu mbichi kabisa. Kuna miguu na mikono. Pembeni mwa hiyo nyama, kuna kijana mmoja mwenye uso uliojaa makovu. Anaitwa Pengo. Sijui kwanini anaitwa Pengo, pengine ni kutokana na kutokuwa na meno mengi mdomoni. Namwuliza; “Pengo, vipi bwana, mbona uso umeharibika, wewe ni mgomvi au ulikuwa ukipambana na nyati?” Anajibu kwa tabasamu, “Siyo nyati mkuu, hii kitu ndiyo imefanya yote haya,” anasema huku akinionesha pikipiki.

Wageni wanazidi kumiminika hapa, na nyama zinauzwa kwa kasi. Ghafla, Pengo na Mangi wanaonekana kuhamaki baada ya kuwaona wateja wengine wawili wasiowajua wakija mahali tulipo. “Wale nani?" Anahoji Mangi. Pengo anajibu, “Ni wateja tu, siyo watu wabaya.”

Nyama tuliyoilipia ipo tayari. Tunaanza kula, lakini ni ngumu. Yaelekea ni ya upande wa shingo.  Nimeshindwa kutelemka na kamera yangu kubwa. Hali hii inalilazimu nitumie kamera maalumu kupata picha za hapa na pale.

Ili nisiweze kushitukiwa, nauliza bei ya mguu wa pofu. Naambiwa kuwa bei yake ni Sh 120,000. Naomba niuziwe kipande cha Sh 20,000. Pengo anachukua mguu wa pofu. Anaupeleka nje kwenye gogo maalumu. Anakata. Kuona hivyo, walaji wenzetu nao wanaanza kununua. Wanakatiwa kadiri ya fedha zao. Wengine wanaingia wakiwa na bia zao kabisa. Nyama ni nyingi na hakuna mwenye wasiwasi.

Mwisho, nikiwa nimeshajiridhisha kuwa nyama inayouzwa ni ya pori, namwuliza Pengo wapi wanakopata nyama. “Hii nyama tunanunua kwa Waarabu wa Morogoro wanaokuja kuwinda huku.” Namwuliza, “Mbona muda wa kuwinda umekwisha?” Anakosa jibu.

Tumeshajiridhisha pasi na shaka kuwa hapa ni kwenye mnada wa wanyamapori. Tunaaga, lakini kabla ya kuondoka, Mangi anatupatia namba yake ya simu. “Chukua namba yangu ya simu, ukiwa unahitaji kabla ya kufika hapa wewe piga simu kabisa tukuandalie. Namba yangu ni 0655 093795. Karibu sana,” anasema.

Ingawa mwanzoni alinieleza kwamba jina lake ni Mrosso Anthony, usajili wa namba hii unaonesha kuwa ni ya Christian Joseph. Hii inazidi kunipa shaka.

Baada ya hapo naanza uchunguzi wa hapa na pale. Najiridhisha kuwa pikipiki iliyopo hapa ni moja ya zana zinazotumika kusafirisha nyama. Naelezwa na mmoja wa vijana kwamba pamoja na kuwapo kundi la vijana wanaoendesha ujangili, baadhi ya nyama wanazipata kutoka kwa askari wanyamapori wa Mikumi.

Wiki ijayo naendelea kueleza vituo vingine vya uuzaji wanyamapori. Ushiriki wa maofisa na askari wanyamapori katika biashara hii haramu. Je, Mkurugenzi na mwenye dhamana ya kupambana na ujangili nchini, Paul Sarakikya; Kamanda Masalu, Mkuu wa KDU (Kikosi Dhidi ya Ujangili), Majid Lalu; Mkuu wa Hifadhi ya Mikumi; Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mvomero, Sarah Limuna; Ofisa Wanyamapori Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa.

Nao, Askari Wanyamapori Wilaya ya Mvomero aliyepewa dhima ya kusimamia wanyamapori eneo la Doma, Peter Mayapila; Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Paschal Shelutete; wanasemaje?  Je, kuwapo kwa huduma za mitandao ya simu hifadhini na katika mapori pamoja na kuruhusu matumizi ya bodaboda kunachangiaje wimbi la ujangili nchini?

...Usikose toleo lijalo la gazeti JAMHURI.



BAVICHA YA CHADEMA YAZIDI KUMEGUKA

Ndugu waandishi wa habari, baadhi yenu mnafahamu kuwa Baraza la Vijana la Chadema Taifa (BAVICHA), limefanya kikao cha kawaida cha Kamati Tendaji, juzi 5 Januari 2013, katika Hotel ya Benzi Garden jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine, kilijadili masuala matatu mazito.

Kwanza, Kamati Tendaji ilijadili kwa kina suala la kuporomoka kwa elimu nchini, ambapo serikali imepunguza alama za viwango vya kufaulu, jambo ambalo limesababisha mamia ya wanafunzi waliochaguliwa kutokuwa na sifa.
Pili, Kamati Tendaji ilijadili jinsi Bavicha itakavyoshiriki katika maandilizi ya utekelezaji wa maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema yalioeleza kuwa mwaka 2013 ni mwaka wa nguvu ya umma.

Tatu, Kamati Tendaji ilijadili kwa kina “Tuhuma za usaliti na njama za kuvuruga chama, kutukana viongozi wakuu wa chama na kuvuruga wanachama wa Chadema na Baraza kwa ujumla.”
Ndugu waandishi wa habari, yapo baadhi ya vyombo vya habari jana na leo vimeripoti kwa upotoshaji mkubwa wa baadhi ya masuala yaliyojadiliwa na kikao hicho. 

Kwa mfano, gazeti moja la kila siku limemtaja mwanachama wetu mmoja kuwa ndiye aliyekuwa mtoa taarifa wetu muhimu na kusema mbunge mmoja wa CHADEMA alijadiliwa katika kikao hicho kuwa ni miongoni mwa kundi hili la MASALIA na kufika mbali zaidi kwa kusema, “…sasa amekalia kuti kavu.”
Lakini ukweli wa kilichojadiliwa kikaoni ni huu ambao tunaueleza sasa:

Kwanza, kuhusu ajenda ya kuporomoka kwa elimu: Kamati Tendaji imeagiza kuwa utafiti uliofanywa na BAVICHA katika ngazi ya sekondari, ambao umegundua madudu mbalimbali, uongezwe hadi shule za Msingi na taarifa yake ililetwe kwenye kikao kijacho cha Kamati Tendaji.
Kwenye ajenda ya pili: Kamati ya Utendaji BAVICHA, ilipokea na kujadili agizo la Kamati Kuu ya Chama iliyoeleza kuwa mwaka 2013 ni mwaka wa nguvu ya umma. 

Katika ajenda ya tatu juu ya tuhuma za usaliti na njama za kuvuruga chama, kutukana viongozi wakuu wa chama na kuvuruga wanachama wa CHADEMA, na Baraza, Kamati ya Utendaji ilipokea taarifa ya Kamati Ndogo ya Kamati Tendaji iliyoundwa Septemba mwaka jana kwenye kikao chake kilichofanyika mjini Morogoro. Kamati ilipewa muda wa mwezi mmoja kukamilisha kazi hii.
Katika hili, watuhumiwa wakuu walikuwa ni kama ifuatavyo:

  1. Juliana Shonza, Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa
  2. Habib Mchange, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
  3. Mtela Mwampamba, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
  4. Gwakisa Burton Mwakasendo, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA
  5. Joseph Kasambala, mwanachama wa BAVICHA na CHADEMA


Aidha, baada ya Kamati iliyoundwa kuwahoji baadhi ya watuhumiwa na wanachama wengine mbalimbali, ilibaini kwamba wapo baadhi ya wanachama wa BAVICHA ambao wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika tuhuma hizi. Hao ni pamoja na Ben Saanane – maarufu kama Eight Oclock.

Katika orodha hiyo, wakatajwa pia Exaud Mamuya lakini kamati ikashindwa kumpata Mamuya kwa kuwa hakukuwa na mawasiliano ya kutosha.

Ndugu waandishi wa habari, hizi sasa ni tuhuma za kila mmoja:

Ndugu Juliana Shonza:

Alituhumiwa akiwa katika nafasi yake ya Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA, amekuwa akishirikiana na baadhi ya watu kupanga njama na kufanya usaliti dhidi ya Baraza, Chama na vijana wenzake wapenda mabadiliko nchini.

Amekuwa akifanya mikutano na vikao vya siri, kwa manufaa ya CCM, akiwakusanya vijana wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali waliosimamishwa masomo au kufukuzwa vyuoni kwa kutimiza wajibu wao wa kudai haki zao za msingi na uwajibikaji wa serikali na ambao ni wanachama wa CHASO.

Juliana alifanya kazi yake hiyo kwa ushawishi wa hongo, ili wakubali kuitisha mkutano na waandishi wa habari, watoe matamko machafu dhidi ya CHADEMA na viongozi wake wakuu, akiwamo Dk. Willibrod Slaa na Freeman Mbowe.

Mfano dhahiri hapa ni kikao alichofanya Baa ya Highland iliyoko maeneo ya Makumbusho, majira ya saa 9 hadi saa 11, ambapo aliwaita viongozi wa CHASO, akawashawishi kuwa watakuwa na maisha mazuri, watarudishwa vyuoni na kutunzwa vizuri hapa mjini kama anavyoishi yeye, endapo tu watakubali kufanya press conferences na kuisema CHADEMA kuwa inawavuruga vijana walioko vyuoni.

Tarehe 6, Desemba, 2012 Hotel MIC, kuanzia saa 10 hadi saa 12, aliwaita baadhi ya vijana ambapo yeye na wenzake walipanga njama za kukichafua chama na kutukana viongozi, kwa manufaa ya CCM.
Ifuatayo hapa chini ni moja ya sms ambazo Juliana Shonza alikuwa akiwaandikia vijana katika ushawishi wake wa usaliti kwa mapambano haya ambayo chama chetu kinafanya, kuwapigania Watanzania maskini na wanyonge katika nchi yao;

“jembe chukua bodaboda basi jamaa washatia timu hela yako yakulinda mfuko wako utaikuta tumempa eddo mnaetoa naye tamko tutalindana tu jembe usijali.”

Huu ni moja tu kati ya ushahidi mwingi, wa meseji, simu, sauti, video, picha na vikao kadhaa katika maeneo mbalimbali, unaomwingiza Shonza na wenzake wengine katika sifa mbaya ya usaliti wa chama, baraza na viongozi wake na wanachama wenzao na umma wa Watanzania kwa ujumla.

Hapo alikuwa akimwandikia mmoja wa viongozi wetu ili ashiriki katika press conference ambayo yeye Makamu Mwenyekiti kwa kushirikiana na wenzake wengine, walikuwa wameiandaa kwa nia ya kuchafua chama, kulichafua baraza, kutukana viongozi waandamizi pamoja na kuvuruga na kuchonganisha wanachama wa CHADEMA.

Matokeo ya kikao hicho cha MIC Hotel, yalionekana siku moja baada ya kikao hicho, ambapo mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Edo Mwamalala, aliyeshiriki kikao hicho cha MIC Hotel, aliitisha mkutano na waandishi wa habari, akijitambulisha kuwa ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CHADEMA, cheo ambacho hakuwa nacho.

Aidha, Shonza amekuwa akikutana na kufanya vikao vya siri na wenzake, wakipanga njama za kufanya kazi na majukumu ya CCM kuhujumu BAVICHA pamoja na CHADEMA. Mikakati ya kuvuruga baraza, kuchonganisha wanachama na kutukana chama na viongozi wakuu, kwa siri na hadharani, imekuwa ikipangwa katika vikao hivi.

Amebainika kukiuka kipengele cha 10.1(x) cha Maadili ya Viongozi, cha Katiba toleo la mwaka 2006, kinachomtaka kiongozi yeyote asitoe tuhuma zozote juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali, kwa kuzingatia taratibu na kanuni za chama.

Ameonesha ubaguzi wa kikabila na kikanda kupitia maandiko yake kwenye mtandao kwa kutumia jina lake, anapungukiwa na sifa muhimu na mahsusi za kuwa kiongozi, kwa mujibu wa kipengele cha 10.1(iv) kinachomtaka kiongozi yeyote asijihusishe na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini au ukanda vinavyolenga kuleta ubaguzi ndani ya chama.

Kwa kushiriki vikao vya kuanzisha chama kipya kinachoitwa CHAUMMA, kushiriki katika makundi yaitwayo MASALIA na PM7 ambayo yote yalikuwa na lengo la kuvuruga chama na wanachama, kukosanisha na kutukana viongozi wa chama, ndugu Shonza amevunja kipengele cha 10.1(i),(viii)(ix) na ibara ya 10.2(iv).

Kwa kushiriki vikundi hivyo hapo juu, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya BAVICHA wamejiridhisha pasi na shaka kuwa Shonza haendani na katiba, falsafa, sera na maadili ya chama makini na tumaini la watu, CHADEMA. Hivyo kwa mujibu wa ibara ya 5.1.4 na 5.1.5 anakosa sifa za kuwa mwanachama wa Baraza la Chama.

Kwa kutoa tuhuma za uongo dhidi ya wanachama na viongozi wenzake, ameendelea kuvunja kanuni za uendeshaji kazi za chama ibara ya 10.1(viii).

Amehusika katika kuanzisha, kujihusisha na kuratibu moja kwa moja kundi la vijana waliokuwa wakizunguka mikoani na kushawishi viongozi wa vijana kutoa matamko kwa kutumia jina la CHADEMA kufanya kazi na majukumu ya CCM ya kukichafua chama, kugombanisha wanachama na kumtukana Katibu Mkuu kwa kutumia propaganda za CCM.

Kamati Ndogo ilimuita Ndugu Shonza ili kumhoji. Lakini aligoma kwa madai kuwa haitambui kamati hiyo na wala hajui kuwa kuna mgogoro, jambo ambalo limetushangaza wengi kwa kuwa Ndugu Shonza alikuwapo katika kikao cha Morogoro kilichounda Kamati hii.

Ndugu Shonza pia hakuhudhuria kikao cha Kamati Tendaji cha juzi kwa madai kuwa amebanwa na shughuli za familia. Baada ya kupitia maelezo yote hayo, Kamati Tendaji iliamua yafuatayo:

Ndugu Juliana Shonza, amepoteza sifa na uhalali wa kuwa mwanachama wa Chadema kwa kukiuka ibara ya 5.3.4 na ibara ya 10.1(ix) ya katiba ya CHADEMA na hivyo imeamua kumuondoa katika nafasi yake ya makamu mwenyekiti na kumfuta uwanachama wake.

Hivyo basi, kwa maamuzi hayo ya Kikao cha Kamati ya Utendaji ya BAVICHA, kuanzia juzi tarehe 5 Januari 2013, Ndugu Juliana Shonza, si mwanachama wa BAVICHA na hivyo moja kwa moja amepoteza sifa za kuwa kiongozi wa baraza na kwa nafasi yake aliyokuwa nayo ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara.

Habib Mchange:

Huyu alituhumiwa kutoa tuhuma za uongo, zikiwemo za mauaji, kinyume na maadili ya Wanachama (kipengele cha 10.3(3); kuunda vikundi vinavyojulikana kwa majina ya MASALIA na PM7 – Pindua Mbowe.

Pia Ndugu Mchange alituhumiwa kuwavuruga wanachama, kuwachonganisha na kuwatukana viongozi, kisha kushiriki vikao vya kuanzisha chama kingine cha siasa cha CHAUMMA.

Alituhumiwa pia kupotosha maamuzi halali ya vikao vya chama na Baraza hivyo kuendelea kukipaka chama matope.

Kamati ilimuita Mchange, na kumhoji juu ya tuhuma zinazomkabili. Hakufika. Badala yake, aliandika barua kueleza kuwa hana imani na kamati:

Aidha, pamoja na Mchange kugoma kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Kamati Tendaji, Sekretarieti ya Kamati Tendaji Taifa, ilimuita Ndugu Mchange kuhudhudhuria mkutano wa Kamati Tendaji ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mwaliko huu ulifanywa kwa njia ya barua na simu. Njia hizo ndio zilizotumika kualika wahusika wote wakiwamo wajumbe wa Kamati Tendaji,

Ndugu waandishi wa habari, baadhi yenu mnafahamu kwamba Ndugu Mchange alikuwa miongoni mwa wanachama wa BAVICHA waliotaka kuwania nafasi ya uenyekiti wa taifa wa baraza hili. Jina lake liliondolewa na Kamati Kuu ya CHADEMA, kutokana na kukosa maadili ya uongozi.

Kamati Tendaji baada ya kusikiliza hoja yake hii, ikajiridhisha kuwa mtuhumiwa ameamua kuibuka hoja hiyo ili kutaka Kamati Tendaji isimjadili ili aendeleze mradi wake wa kukichafua chama akiwa ndani ya chama.

Hivyo Kamati Tendaji imefanya yafuatayo: Imempata na hatia ya kuvunja ibara ya 10.3(iii) na kwenda kinyume na kanuni za uendeshaji wa chama ibara ya 10.3(4), kinyume na Maadili ya Wanachama (kipengele cha 10.3(3); uendeshaji wa chama ibara ya 10.3(4) na kwamba mambo yote haya yanadhihirisha kuwa Ndugu Mchange hayuko tayari kushirikiana na viongozi wake kama mwanachama, hivyo kukiuka katiba ya chama ibara ya 5.3.4 na kuafikiwa uamuzi wa kumfukuza uwanachama wa Bavicha na Chadema.

Mtela Mwampamba:

Huyu ametuhumiwa kutoa tuhuma nzito za uongo hadharani, zikiwemo za mauaji, kinyume kabisa na Maadili ya Wanachama (kipengele 10.3(3).

Kuvunja katiba ya chama ibara ya 5.3.4 na Kanuni za Uendeshaji kazi za chama Ibara ya 10.3(4) kwa kupotosha maamuzi halali ya vikao vya chama na baraza na kukipaka matope chama pamoja na kudhihirisha kuwa hayuko tayari kushirikiana na viongozi wake kama mwanachama.

3.Amevunja Katiba ya CHADEMA ibara ya 5.3.3 na 5.3.4 kwa kutoa kauli za kichochezi dhidi ya chama, kuwachonganisha wanachama na kuwatukana viongozi.

4.Kwa kujiunga na vikundi vinavyoitwa MASALIA NA PM7 na baadae kushiriki vikao vya kuanzisha chama cha CHAUMMA, Ndugu Mwampamba amevunja ibara ya 10.3(iii).

5.Kinyume na ibara ya 5.3.3 na 5.3.4 ya Katiba ya CHADEMA na Ibara ya 4.3(g) na (i) ya kanuni za BAVICHA, zinazopinga ubaguzi wa aina yoyote ile, Ndugu Mwampamba ameonesha hisia za ubaguzi wa kikabila na kikanda.

Gwakisa Burton Mwakasendo:

Huyu amekuja kwenye kikao na kukiri kutenda makosa yake ambayo takriban yote ni sawa yanayowahusu watuhumiwa waliotangulia hapo juu. Mbele ya kikao cha Kamati ya Utendaji alikiri kushiriki vikao, akisema kuwa ‘lakini’ alilazimika ‘kuikimbia’ dhambi kwa kuondoka katika baadhi ya mikutano na watu hao, wakati mwingine hata nyumbani kwake hakuweza kulala akihisi ‘dhambi’ hiyo anayoikimbia itamfuata nyumbani.

Kamati Tendaji, iliamua kumpa adhabu ya kuwekwa chini ya uangalizi kwa mwaka mzima, katika wakati wote huo amezuiwa kugombea nafasi yoyote ndani ya BAVICHA na onyo kali la barua.

Ben Saanane:

Huyu pamoja na kwamba hakuwa miongoni mwa watuhumiwa alipewa adhabu ya onyo kali na uangalizi wa miezi 12, kutokana na makosa yafuatayo. Kutoa tuhuma nzito, zinazomhusu pia Kiongozi wa juu mwandamizi wa chama, Ben amekiuka Maadili ya Wanachama (kipengele 10.3(3).

Kukiri kuwa mmoja wa waanzilishi wa vikundi vinavyoitwa MASALIA na PM7 na kisha kushiriki vikao vya kuanzisha chama kingine cha CHAUMMA, amevunja ibara ya 10.3(iii), kwa nia ya kuvuruga chama na kutukana viongozi wake:

Mbele ya Kamati Tendaji, Ben alikiri makosa na akaomba radhi.

Aidha, Ben alitoa ushirikiano mkubwa kwa Kamati Ndogo jinsi ya kupatikana kwa taarifa na ushahidi wa namna wanachama wa BAVICHA walivyokuwa wanafanya kazi za kundi hili la MASALIA na PM 7 na hasa juu ya majina wanayotumia katika mitandao mbalimbali ya kijamii, wakifanya juhudi za kuivuruga CHADEMA, kuvuruga BAVICHA, kutukana viongozi na kuwavuruga wanachama, lakini kikubwa wakionesha kila dalili ya tabia ya usaliti.

Exaud Mamuya:

Huyu hajapata nafasi ya kusikilizwa kwenye vikao. Hivyo suala lake litaendelea kufanyiwa kazi na uongozi wa BAVICHA.

Aidha, kikao cha Kamati ya Utendaji pia kilipitisha kwa kauli moja, moja ya maazimio ya BAVICHA Mkoa wa Mwanza, waliopendekeza kufukuzwa uanachama kwa aliyekuwa Katibu wa Mkoa wa Mwanza, Salvatory Magafu, kwa tuhuma za kukiuka Kanuni ya 10.1(xii) kwa kutoa tamko kwenye vyombo vya habari kwa nia ya kumfarakanisha Katibu Mkuu na wanachama wa CHADEMA na umma wa Watanzania, ikiwa ni sehemu ya uratibu wa kundi lililokuwa likiendeshwa na watuhumiwa wengine hapo juu.

Kamati ya Utendaji pia ilimkuta na makosa ya kiuongozi katika tuhuma zilizowasilishwa vikaoni na kufanyiwa kazi na Kamati Ndogo, Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Mbeya, Joseph Kasambala na hivyo amepewa adhabu ya onyo kali.

Hitimisho
Tunaomba kuwahakikishia vijana wenzetu wa CHADEMA na wengine wote wapenda mabadiliko nchini, hakuna kijana mwanachama wa BAVICHA, atafanya kazi za kuhujumu baraza na chama kwa ujumla na kusaliti matumaini pekee ya Watanzania, akifanya kazi za mahasimu wetu, kisha akaachwa.

Ni lazima na muhimu tuoneshe kuwa tuna uthubutu kwa kuchukua hatua kadri inavyotakiwa, pale panapotakiwa. Tuliopewa dhamana za uongozi, tutatimiza wajibu kuhakikisha hakuna mtu ataonewa wala kupunjwa haki yake katika kusimamia utendaji na utoaji utumishi bora wa baraza kwa wanachama wake na chama kwa ujumla.

Daima tutasimamia katiba ya chama, maadili, kanuni, taratibu, itifaki na miongozo ya mabaraza. Baraza hili halitakuwa tayari kuwa sehemu ya kuruga matumaini makubwa ya Watanzania waliyonayo juu ya CHADEMA.

Baraza liko imara. Wanachama wetu wasifadhaishwe na upotoshaji unaofanywa na wasaliti kuwa tumevurugika au ‘kumechafuka’. Hatuwezi kuchafuka wala kuvurugika kwa kuchukua maamuzi dhidi ya watu wabinafsi wanaotaka kukwamisha mapambano ya awamu ya pili, kupigania mabadiliko ya kweli ya kimfumo na kiutawala, kwa ajili ya Watanzania.

Historia inatuonesha kuwa mara zote ambapo mapambano yamefikia hatua ya juu ya kutimiza malengo, ndipo ambapo wasaliti hujitokeza. Hivyo vikwazo hivi vya baadhi yetu kuanza kugeuka nyuma ni dalili za mwisho mwisho kuwa ushindi unakaribia. Ni lazima kama vijana tuendelee kujenga imani na matumaini ya Watanzania waliyonayo juu ya CHADEMA kutukabidhi dola mwaka 2015.

Mwisho

Imetolewa leo Januari 7, 2013, Dar es Salaam na;
John Heche
Mwenyekiti wa Taifa, 

Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA)


RAIS AKIWA NZEGA LEO


Picture
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na mmoja wa wahandisi wa kutoka China waliopata kandarasi ya kujenga barabara baada ya kuzindua rasmi ujenzi wa barabara hiyo akiwa katika ziara yake ya siku nne ya mkoa wa huo ambapo anazindua miradi kadhaa ya maendeleo ikiwemo barabara, daraja na maji.



Sunday, January 6, 2013

MCHUNGAJI AMBILIKILE AOTA TENA DAWA MPYA

Mchungaji Mstaafu Ambilikile Mwaisapile wa KKKT Loliondo ameitaka serikali kukaa mkao wa tayari tayari maana anadai ameoteshwa dawa mpya ambayo atakapo itangaza na kuanza kutoa tiba itajaza watu wengi katika kijiji hicho cha Loliondo. Hakuwa tayari kuweka wazi ni dawa aina gani ambayo ameoteshwa sasa hivi na itatibu magonjwa gani. Pamoja na kumdadisi ili aeleze kama masharti ni yaleyale au yamebadilika Mchungaji Mwaisapile hakuwa tayari kuweka wazi mpaka muda utakapofika.
Hii inaonekana inaweza ikawa neema tena kwa wafanyabiashara ya usafiri wa mkoa wa Arusha na Manyara pamoja na wakazi wa kijiji hicho cha Loliondo maana kwa idadi kubwa inayoenda huko biashara huwa inakuwa kubwa sana.
Mchungaji Ambilikile aliteka vichwa vya habari vya vyombo mbalimbali kwa dawa ambayo aliota mara ya kwanza kwa kipindi hiki umaarufu wake na jina lake lilikuwa likitoweka katika midomo na vichwa vya watanzania tusubiri kuona kama atarudi tena kwenye chati kama zamani.

Saturday, January 5, 2013

VILIO VYATAWALA UJIJI: BOTI LAZAMA NA KUUWA

Mh Zitto Kabwe ametuabarisha kupitia ukurasa wake wa facebook Kuwa boti limezama ziwa Tanganyika eneo la herembe kusini mwa Ziwa Tanganyika. Mpaka sasa watu 14 wamefariki na miili imeanza kutambuliwa



RAIS KIKWETE KUZINDUA MIRADI MINNE TABORA




 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU