TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUFAFANUA KUHUSU
MIRADI YA UTAFUTAJI NA UVUNAJI WA GESI ASILIA NCHINI
1.0 UTANGULIZI
Wizara
ya Nishati na Madini inapenda kutoa ufafanuzi wa miradi ya Gesi Asilia
ambayo itatekelezwa kwa kushirikiana na wawekezaji katika Sekta ndogo
ya Gesi Asilia na kueleza manufaa makubwa yatakayopatikana kwa wananchi
wote wa Tanzania wakiwemo wale wa Mikoa ya Mtwara na Lindi.
Siku
ya Alhamisi, tarehe 27 Disemba 2012, baadhi ya Vyama vya Siasa vya
Upinzani viliratibu na kuhamasisha baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara,
wengi wao wakitokea Mtwara Mjini kufanya maandamano ya kudai raslimali
ya Gesi Asilia iwanufaishe wakazi wa Mtwara na kupinga mradi mkubwa wa
ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Wizara
ya Nishati na Madini inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa Wa-Tanzania
wote kwa kupitia vyombo vya habari.
Tokea Uhuru, uchumi wa
Tanzania umetegemea kilimo cha mazao ya biashara kama vile katani (Tanga
na Morogoro), pamba (Mwanza, Mara na Shinyanga), kahawa (Kilimanjaro,
Kagera, Ruvuma na Mara), chai (Iringa) na tumbaku (Tabora). Fedha za
mazao haya zimewanufaisha wakazi wa mikoa yote ya nchi yetu bila
ubaguzi wo wote wala wakulima wa kutoka mikoa hiyo hawajawahi kufanya
maandamano wakidai upendeleo (dhidi ya Wa-Tanzania wengine) wa aina yo
yote ile.
Mapato yatokanayo na uchimbaji wa dhahabu (Mwanza,
Geita, Mara, Shinyanga na Tabora), almasi (Shinyanga) na tanzanite
(Manyara) yamewanufaisha Wa-Tanzania wote bila ubaguzi wo wote ule!
Minofu ya samaki wa Ziwa Victoria (Mara, Mwanza na Kagera) imeliingizia
Taifa letu fedha nyingi ambazo zimetumiwa na wakazi wa nchi nzima
bila ubaguzi wo wote.
Aidha kuna mikoa ambayo inazalisha mazao ya chakula kwa wingi kwa manufaa ya Wa-Tanzania wote. Mahindi kutoka
Rukwa,
Mbeya, Ruvuma na Iringa yanasafirishwa kwenda mikoa yote ya nchi yetu
bila kujali eneo yanakolimwa na wakazi wa mikoa hiyo hawajawahi kudai
mahindi hayo ni kwa ajili ya watu wa mikoa hiyo pekee. Sukari ya
Kilombero, Mtibwa na Kagera inatumiwa na wakazi wa mikoa yetu yote bila
ya kuwepo madai ya mikoa inayozalisha sukari hii kupewa upendeleo wa
aina yo yote ile. Maji ya Mto Ruvu yanatumiwa na wakazi wa Dar Es Salaam
bila manung’uniko yo yote kutoka kwa wakazi wa eneo la chanzo cha
Mto Ruvu.
Umeme wa kutoka Mtera, Kidatu na Kihansi (Dodoma na
Morogoro), Hale (Tanga), na Nyumba ya Mungu (Kilimanjaro) unatumiwa na
wakazi wote wa Tanzania bila ubaguzi au malalamiko ya wenyeji wa
sehemu ambazo umeme huo unafuliwa na kusafirishwa kwenye Gridi ya
Taifa.
Kwa hiyo, kutokana na mifano hii michache, ni wajibu wa
wazalendo na wapenda maendeleo wa kweli na hasa Wa-Tanzania wanaopinga
ubaguzi wa aina yo yote ile kujiuliza kwa kina sababu zilizopelekea
Vyama Siasa vya Upinzani kupanga, kuhamasisha, kushabikia na
kuongoza maandamano ya tarehe 27 Disemba 2012 pale Mtwara Mjini.
2.0 RASLIMALI YA GESI ASILIA TANZANIA
Gesi
Asilia ilianza kugundulika hapa nchini tangu mwaka 1974 kwenye Kisiwa
cha Songo Songo, Mkoani Lindi. Baada ya hapo Gesi Asilia imegundulika
maeneo ya Mtwara Vijijini, yaani Mnazi Bay (1982) na Ntorya (2012),
Mkuranga (Pwani, 2007), Kiliwani (Lindi, 2008). Kiasi cha Gesi Asilia
iliyogunduliwa katika maeneo haya inakadiriwa kuwa Futi za Ujazo Trilioni 4.5 – 8.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kumekuwa na kasi kubwa ya
utafutaji Mafuta na Gesi Asilia uliojikita zaidi kwenye maji ya kina
kirefu cha bahari. Kiasi cha Gesi Asilia iliyogundulika katika kina
kirefu cha maji inafikia takribani Futi za Ujazo Trilioni 27. Kiasi cha wingi wa Gesi Asilia yote iliyogunduliwa nchi kavu na baharini inafikia takribani Futi za Ujazo Trilioni 35.
Kufuatana
na Sheria za nchi yetu zinazotumiwa kugawa mipaka ya mikoa iliyopo
kando kando mwa bahari (isivuke 12 nautical miles au 22.22 km kuingia
baharini), Gesi Asilia iliyogunduliwa hadi sasa katika Mkoa wa Mtwara pekee ni asilimia 14 tu ya gesi yote iliyogundulika nchini. Kwa kutumia kigezo hicho cha Sheria za mipaka ya ki-utawala ya mikoa yetu, Lindi inayo 7% ya gesi yote, Pwani 1% na huku Kina Kirefu cha Bahari (Deep Sea) ndicho chenye gesi nyingi (78%)
kuliko mikoa yote ikiwekwa pamoja! Kwa hiyo, hakukuwa na haja ya
kufanya maandamano kwa sababu Gesi Asilia nyingi inapatikana kwenye
bahari ya kina kirefu ambayo iko ndani ya mipaka ya nchi yetu bila
kujali mipaka ya mikoa yetu. Isitoshe Gesi Asilia imegundiliwa kwenye
miamba tabaka (sedimentary rocks) yenye umri wa Miaka kati ya Milioni 199.6 hadi 23.03. Mipaka ya Bara la Afrika, ya nchi yetu na ile ya mikoa yetu haikuwepo wakati huo!
Utafutaji
wa Mafuta na Gesi Asilia pia unaendelea tukiwa wa mategemeo makubwa ya
upatikanaji wa raslimali hizi katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro,
Tanga, Manyara, Kigoma, Mbeya, Njombe, Rukwa, Katavi, Morogoro na Tabora
pamoja na kwenye kina kirefu cha maji baharini kuanzia mpaka wetu na
Msumbiji hadi mpaka wetu na Kenya. Hatutarajii mikoa hii nayo ifanye
maandamano ya kutaka kuhodhi raslimali za Gesi Asilia na Mafuta
zitakapogunduliwa mikoani mwao.
3.0 MATUMIZI YA GESI ASILIA YA MNAZI BAY (MTWARA) NA SONGO SONGO (LINDI)
Mpaka
hivi sasa Gesi Asilia inayozalishwa na kutumika nchini ni kutoka Mnazi
Bay (Mtwara Vijijini) na Songo Songo (Kilwa, Lindi). Gesi ya Mnazi Bay
kwa sasa huzalisha umeme kwa ajili ya Mikoa ya Mtwara na Lindi tu.
Mitambo ya kufua umeme kutokana na Gesi Asilia iliyopo Mtwara Mjini inao
uwezo wa kuzalisha MW 18 lakini matumizi ya umeme ya Mikoa ya Mtwara na Lindi haijavuka MW 12.
Umeme huo wa Mtwara unafuliwa na TANESCO huku Kampuni za Wentworth na
Maurel & Prom zikizalisha Gesi Asilia (inayotumiwa na TANESCO)
kiasi cha Futi za Ujazo Milioni 2 kwa siku. Ikumbukwe kwamba ufuaji wa
umeme wa hapo Mtwara Mjini ulikuwa mikononi mwa Kampuni ya
Artumas iliyofilisika. Tangu Desemba 2006 hadi leo hii kiasi cha gesi kilichotumika kufua umeme kwa ajili ya mikoa hiyo miwili ni chini ya asilimia 1 ya gesi yote iliyogundulika Mnazi Bay (Mtwara Vijijini). Vilevile
ikumbukwe kwamba kuna visima vinne vya Gesi Asilia pale Mnazi Bay
(Mtwara Vijijini) na kinachotumika kwa sasa na tena kwa kiwango cha
chini kabisa ni kimoja tu!
Aidha ni vizuri ndugu zangu
Wa-Tanzania wakaelewa kuwa Gesi Asilia hii inatafutwa na kuchimbwa na
wawekezaji wenye mitaji mikubwa, wataalamu na teknolojia ya utafutaji na
uchimbaji wa Gesi Asilia ambao wanapaswa kurejesha mitaji yao.
Uchorangaji wa kisima kimoja cha utafutaji wa Gesi Asilia nchi kavu
unahitaji Dola za Marekani Milioni 40, na kwenye kina kirefu cha maji baharini zinahitajika zaidi ya Dola za Marekani Milioni 100.
Ikumbukwe kwamba, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Mafuta la
Tanzania (TPDC), inatumia fedha za walipa kodi wa nchi nzima kwa
shughuli za kuvutia, kuratibu na kusimamia utafutaji na uendelezaji wa
Gesi Asilia nchini kote ikiwemo Mikoa ya Mtwara na Lindi. Walipa kodi
Wa-Tanzania bado hawajalalamika wala hawajafanya maandamano ya kudai
fedha zao za kodi zisitumike huko Mtwara!
Ni muhimu pia
tukaelewa kwamba Gesi Asilia iliyopo Mnazi Bay (Mtwara Vijijini)
inazalisha umeme peke yake kwa ajili ya Mikoa ya Mtwara na Lindi. Gesi
Asilia ya Songo Songo (Kilwa, Lindi) ndiyo
inayotumika kuzalisha umeme kwa ajili ya Gridi ya Taifa, na pia kwa
ajili ya wananchi wa Kisiwa cha Songo Songo (Lindi), maeneo ya Somanga
4 Fungu
(Lindi) na viwandani (Dar Es Salaam). Tangu Oktoba 2004 ambapo mitambo
ya kufua umeme ilipoanza kazi hadi leo hii, kiasi cha Gesi Asilia ya
Songo Songo kilichotumika ni asilimia 7 tu ya Gesi
Asilia yote iliyogunduliwa huko. Kwa hiyo, takwimu zinaonyesha kwamba
hata uchumi wa Jiji la Dar Es Salaam unatumia kiasi kidogo sana cha
Gesi Asilia (7%) iliyopo Songo Songo (Kilwa, Lindi).
Ikumbukwe kwamba waajiriwa kwenye viwanda vya Dar Es Salaam wamo wanyeji
wa kutoka Mtwara Mjini ambako maandamano yalifanyika na vilevile
wamo wafanyakazi ambao ni wanachama wa Vyama vya Siasa vya
Upinzani vilivyopanga, ratibu na kushabikia maandamano ya Mtwara Mjini
ya tarehe 27 Disemba 2012.
4.0 MIPANGO YA MATUMIZI YA GESI ASILIA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA 5 HADI 10
(a) Ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia hadi Dar Es Salaam:
Kuuza
Gesi Asilia Jijini Dar es Salaam, kitovu cha uchumi wa Tanzania (80% ya
mapato ya nchi yetu yanazalishwa Dar Es Salaam) ni uamuzi mzuri wa
ki-uchumi. Tayari kuna viwanda 34 vinatumia Gesi Asilia ambavyo
vinahitaji kupanua shughuli zao endapo gesi zaidi itapatikana. Soko
kubwa la Gesi Asilia lipo tayari Dar es Salaam (na siyo Mtwara), ambapo
ipo mitambo ya kufua umeme kwa kutumia mafuta. Serikali inatumia fedha
nyingi za kigeni kununulia mafuta ya kufua umeme tunaoutumia kila siku.
Takribani Dola za Marekani Bilioni Moja (sawa na Shilingi Trilioni 1.6)
kwa mwaka zitaokolewa kutokana na mitambo iliyopo nchini ikifua
umeme kwa kutumia Gesi Asilia na kuachana na mafuta ambayo ni ya bei
kubwa sana. Bei ya umeme kwa uniti moja (KWh) ya umeme unaofuliwa
kutumia dizeli na mafuta ya aina nyingine ni kati ya Senti za Marekani 30 hadi 45 na huku bei ya uniti moja hiyo hiyo ni Senti za Marekani 6-8 kwa umeme utokanao na Gesi Asilia na zinapungua na wakati wa matumizi. Vilevile, takribani Dola za Marekani millioni 202
kwa mwaka zitaokolewa iwapo Jiji la Dar Es Salaam litatumia Gesi
Asiliabadala ya mafuta katika magari, taasisi na majumbani. Fedha hizi
zikiokolewa zitatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa letu kwa
manufaa ya Wa-Tanzania wote wakiwemo wale waliondamana na wale
walioratibu maandamo ya Mtwara Mjini ya tarehe 27 Disemba 2012.
(b) Umeme mwingi zaidi kutokana na Gesi Asilia:
Bomba
la Gesi Asilia linalojengwa litasafirisha gesi nyingi zaidi ambayo
itawezesha mitambo mipya itakayojengwa Kinyerezi (Dar Es Salaam) kufua
umeme wa zaidi ya MW 990. Umeme mwingine utafulia Somanga Fungu (Lindi)
wa kiasi kisichopungua MW520.
(c) Usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini mwetu:
Dar
es Salaam ndiko kuna miundombinu mikubwa ya usafirishaji na usambazaji
wa umeme kuliko mikoa mingine yote, hivyo ni uamuzi wa ki-uchumi
unaotulazimisha kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mikoa ya Lindi na Mtwara
na kuipeleka Dar Es Salaam ambako itatumika kufua umeme, na kutumika
moja kwa moja viwandani, majumbani na kwenye magari.
(d) Kwa kuzingatia mahitaji ya Gesi Asilia yatakayojitokeza:
Bomba
la kusafirisha gesi litawekewa matoleo ya kuchukulia gesi (tie-off)
katika maeneo ya Mtwara, Lindi, Kilwa na Mkuranga ili kuhakikisha kuwa
miji hii inakuwa na Gesi Asilia ya uhakika wakati wowote
itakapohitajika. Kwa hiyo kuweka mitandao ya usambazaji wa gesi kutoka
kwenye Bomba la Gesi Asilia linalojengwa kutarahisisha matumizi ya Gesi
Asilia viwandani na majumbani katika Mikoa ya Mtwara na Lindi, na kwenye
mikoa mingine kwa siku za baadae.
(e) Serikali imetenga maeneo katika pwani ya Mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) kwa ajili ya uanzishwaji wa maeneo ya viwanda (Industrial Parks/Estates) vikiwemo viwanda vya mbolea, Liquefied Natural Gas (LNG) na Petrochemicals. Ujenzi wa kiwanja cha sementi uko katika hatua za mwisho za maandalizi.
(f)
Ili kutengeneza mazingira mazuri ya biashara ya Gesi Asilia na Mafuta
kwa kampuni za huduma, malighafi na vitendea kazi, Serikali imetenga eneo maalumu Mtwara, ambalo litawekewa miundombinu ya msingi ili kutoa vivutio mbalimbali kwa makampuni hayo. Eneo hilo litapewa hadhi ya Ukanda Huru wa Bandari (Freeport Zone).
Ni
lazima shughuli za kusafisha na kusafirisha Gesi Asilia zitatoa
ajira katika maeneo husika. Kwa mfano kwa mitambo ya kusafishia
gesi inayojengwa Madimba (Mtwara Vijijini) na SongoSongo (Kilwa, Lindi),
kila mtambo utahitaji wafanyakazi na wengine watatoka Mikoa ya Lindi
na Mtwara.
Watanzania wanakumbushwa kuwa raslimali zilizopo
nchini ikiwemo gesi asilia, madini, makaa ya mawe, wanyama pori, misitu,
milima ya utalii, mito, maziwa, bahari n.k ni za Wa-Tanzania wote kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Raslimali
hizi zinapatikana, zinatunzwa na kuzalishwa maeneo mbalimbali
nchini mwetu na mapato yake yanatumika kwa maendeleo ya Wa-Tanzania wote bila kujali maeneo raslimali hizo zilipo.
Tusikubali kuvunja nchi yetu vipande vipade kwa kisingizio cha raslimali zilizopo mikoani mwetu.
Tusikubali kuvunjavunja mikoa yetu kwa kisingizio cha raslimali zilipo kwenye wilaya zetu.
Tusikubali kuvunjavunja wilaya zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye tarafa zetu.
Tusikubali
kuvunjavunja tarafa zetu kwa kisingizio cha raslimali zilizopo kwenye
kata zetu. Tusikubali kuvunjavunja kata zetu kwa kisingizio cha
raslimali zilizopo kwenye vijiji vyetu na mitaa yetu.
MUNGU IBARIKI TANZANIA, DUMISHA UHURU NA UMOJA WETU
Prof Dr Sospeter Muhongo (Mb)
WAZIRI YA NISHATI NA MADINI
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA