Mbunge
wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (kushoto) akizozana na wabunge wa
Chadema, Mchungaji Peter Msigwa(kulia)mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje
(wa pili kulia) na Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (wa pili
kushoto) baada ya kukutana nje ya ukumbi wa mikutano wa St Gasper,Dodoma
jana wakati wa semina ya wabunge ya kuhusu UKIMWI. (picha: Fidelis
Felix/MWANANCHI)
Mbunge
wa Jimbo la Iringa Mjini (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa na mbunge wa
Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba jana nusura wachapane makonde
baada ya kutupiana maneno ya kashfa, wakituhumiana kuhusika na mlipuko
wa bomu uliotokea Jumamosi iliyopita mkoani Arusha.
Tukio hilo
lilitokea katika viwanja vya Hoteli ya St Gasper nje kidogo ya mji wa
Dodoma, walipohudhuria semina ya wabunge wapambanaji na UKIMWI, ambapo
baadhi ya wabunge wa CHADEMA walihudhuria.
Malumbano hayo
yanatokana na Nchemba kuituhumu CHADEMA kuhusika na mlipuko wa bomu huko
Soweto, Arusha (kwenye mkutano wao wa kufunga kampeni za Uchaguzi wa
Madiwani katika Kata za mkoa huo, siku ya Jumamosi ya Juni 25, 2013),
Juni 20 mwaka huu wakati akichangia hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali ya
mwaka 2013/2014, akisema chama hicho kilipanga kulipua bomu hilo ili
kuwafanya Watanzania waamini kuwa Serikali ya CCM ndiyo inayohusika na
tukio hilo.
Msigwa akiingia katika ukumbi huo akiwa ameongozana
na Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA), Ezekiah Wenje, walikutana uso kwa uso
na Nchemba ambaye alikuwa akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA,
Said Amour Arfi. Baada ya Nchemba kumwona Msigwa alimkaribisha mchungaji
huyo akisema;
“Karibu sana bwana, salama lakini?”
Hata
hivyo, badala ya kujibu salamu hiyo ya Nchemba, Msigwa alikuja juu na
kumtuhumu Nchemba kwamba anatoa kauli zinazoweza kuvuruga amani ya
nchi: “Wewe ni mtu hatari sana, haya yote yanasababishwa na wewe, mnatumia damu za watu kutafuta madaraka,” alisema Msigwa akimtupia maneno Mwigulu.
Baada ya kauli hiyo Nchemba alihoji akisema: “Ki-vipi? Hayo mambo tuyaache, Msigwa achana na haya mambo!”
Baada
ya Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM kujibu, Msigwa
alimsogelea karibu na kumnyooshea kidole, huku akiendelea kumtuhumu kuwa
ana siasa chafu zinazopandikiza chuki kwa jamii.
Malumbano
hayo pia yaliingiliwa na Mbunge wa Musoma Mjini (CHADEMA), Vicent
Nyerere ambaye alimuunga mkono Msigwa, huku akimtuhumu Nchemba kuwa ni
mtu mbaya katika siasa za Tanzania.
Katika kile kilichoonekana
kutaka kuweka mambo sawa, Wenje alimvuta Msigwa na kumpeleka ukumbini
ili kuepusha shari baada ya wabunge hao kuzidi kurushiana maneno. Hata
walipoingia ndani ya ukumbi huo wabunge hao waliendelea kulumbana,
lakini wakatulizwa na baadhi ya wabunge waliokuwa karibu yao.
Alipotakiwa kueleza sababu za mzozo huo na Nchemba, Mchungaji Msigwa alisema, “Achana
na yule mpuuzi, mimi siwezi kuzungumza na mtu mnafiki, mkatili na yeye
ndiye alihusika na mipango mibaya dhidi ya CHADEMA hata mlipuko wa
Arusha hivyo kutesa watu wa CHADEMA.”
Alisema
kuwa yeye haoni sababu ya mtu mwenye mipango mibaya na wananchi wa
Tanzania pamoja na chama chake (CHADEMA), kuwafuata na kujikomba.
Kwa
upande wake Nchemba alipoulizwa alisema kuwa alichokizungumza ni
mtazamo wake na kwamba ikiwa kuna mtu anayeona kuwa alizungumza uzushi,
ajitokeze na kupinga: “Nilichokizungumza ndicho kilichofanyika kwa matukio yote niliyoeleza bungeni,”alisisitiza Nchemba.