Facebook Comments Box

Thursday, October 31, 2013

BARAZA LA MITIHANI LATOA VIWANGO VIPYA VYA UFAULU; SASA KUNA DARAJA LA TANO (DIVISION FIVE)


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome akifafanua kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya upangaji wa viwango vya alama, matumizi ya alama endelevu  ya mwanafunzi  na ufaulu leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Kamishna wa Elimu Profesa Eustella Bhalasesa.


 Baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Sifuni Mchome (hayupo pichani).




Waandishi wa habari na maafisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome(hayupo pichani). Picha zote na Eliphace Marwa (MAELEZO).






========  =======  ========



UPANGAJI WA VIWANGO VYA ALAMA, MATUMIZI YA ALAMA ENDELEVU YA MWANAFUNZI NA UFAULU

UTANGULIZI

Wizara imekusanya maoni ya Wadau wa Elimu kuhusu Upangaji wa Viwango vya Alama (Grade Ranges) katika Mitihani ya Kuhitimu Kidato cha Nne na cha Sita pamoja na Matumizi ya Alama za Tathmini Endelevu ya Mwanafunzi (Continuous Assessment ama CA) kwa ajili ya kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi. Maoni ya wadau yamekusanywa kwa sababu kwa muda mrefu sasa upangaji wa viwango vya alama vinavyotumika na utaratibu wake katika mitihani ya kuhitimu Kidato cha Nne na Kidato cha Sita umekuwa haufanani pamoja na kwamba mitihani hiyo yote ni ya elimu ya sekondari. Pia mfumo masuala mbalimbali ya mitihani katika elimu ya sekondari umekuwa na miundo tofauti ikiwemo ule unaotumika shuleni na ule wa Baraza la Mitihani la Taifa. Kwa sasa kuna miundo mikuu miwili katika mfumo huo.

Muundo wa Kwanza ni upangaji wa viwango katika ngazi ya Shule ambapo Alama Mgando (Fixed Grade Ranges) zifuatazo hutumika kupanga madaraja: A = 81 – 100; B = 61 – 80; C = 41 – 60; D = 21 – 40 na F = 0 – 20. Muundo huu umetumika kwa muda mrefu na umezoeleka kwa walimu na wanafunzi wa elimu ya sekondari kwa ujumla.

Muundo wa Pili ni wa viwango vinavyotumiwa na Baraza la Mitihani la Taifa ambapo ambapo kabla ya mwaka 2012 muundo wa viwango nyumbufu (flexible grade ranges) ulitumika. Katika muundo huu uwigo wa alama ulibadilika badilika kulingana na hali ya matokeo ilivyokuwa kwa mwaka husika. Lakini kuanzia mwaka 2012, Serikali iliamua kutumia mfumo wa Upangaji wa Alama Mgando (Fixed Grade Range) kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita. Katika mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 Baraza lilitumia mfumo huu wa alama mgando ambapo: A = 80 – 100, B = 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49, F = 0 – 34. Kwa upande wa Kidato cha Sita Baraza lilitumia mfumo wa A = 80 – 100; B = 75 - 79; C = 65 – 74; D = 55 – 64; E = 45 – 54; S = 40 – 44 na F = 0 – 39. Mifumo hii ya Baraza haikuwa inafahamika kwa wadau na hivyo kuwa sehemu ya malalamiko katika sekta ya elimu na mafunzo.

Vilevile, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 imeelekeza kwamba katika kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi wa elimu ya sekondari, Alama za CA zitachangia asilimia hamsini (50%) na Mtihani wa mwisho utachangia asilimia hamsini (50%). Kwa upande wa Zanzibar, CA zimekuwa zikiandaliwa kwa mfumo wa asilimia arobaini (40%) na mtihani wa mwisho asilimia sitini (60%). Pamoja na kwamba Baraza halijawahi kuutumia mifumo hii tangu ilipowekwa, kumekuwa na mitazamo, maoni na mapendekezo tofauti katika muundo na matumizi ya alama za CA. Kuna mawazo pia kwamba mfumo wa CA kuchangia matokeo ya mwisho ya mwanafunzi pia utumike kwa watahiniwa wa kujitegemea (private candidates). Kwa sasa matokeo ya mitihani ya watahiniwa hawa yamekuwa yakitumia alama za mtihani wa mwisho tu na hivyo kutafsiriwa kama utaratibu ambao unamwonea mwanafunzi ambaye anahamu ya kujiendeleza kielimu lakini anakwama kwa sababu mfumo unaotumika siyo rafiki kwa mtahiniwa.

Kwa mantiki hii, Wizara imedhamiria kufanya harmonization ya masuala ya alama katika mitihani ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita ili kupata muundo mmoja na ulio wazi kwa wadau wote wa elimu ya sekondari. Lakini pia serikali imedhamiria kuhakikisha tathmini za wanafunzi katika ngazi mbalimbali zinakwenda sambamba na matarajio ya mitaala inayotumika na ambayo inahuishwa mara kwa mara ili iendane na wakati na mahitaji ya elimu katika ngazi mbalimbali.



VIWANGO NA UTARATIBU KUANZIA MWAKA 2013 KWA KIDATO CHA NNE NA

MWAKA 2014 KIDATO CHA SITA

Baada ya kufanya tathmini ya maoni mbalimbali ya wadau, misingi ifuatayo ilizingatiwa katika maamuzi kuhusu makundi ya alama na muachano wake:

a)      Alama zitakazotumika zitakuwa A, B, C, D, E na F. Muachano wa alama kati ya kundi moja hadi jingine utafanana, isipokuwa tu pale ambapo itaonekana kuna sababu na hakuna athari za kuwa na muachano tofauti na ule ambao umetumika katika makundi mengine.

b)      Makundi ya alama hayatakuwa na clusters isipokuwa pale ambapo itaonekana kufanya hivyo kunaleta tija katika kupata picha ya wahitimu kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Kwa mantiki hii

(i)         makundi ya alama A, C, D, E na F yabaki na cluster moja moja bali kundi la alama B litakuwa na clusters mbili. Kundi la kwanza litakuwa la wale ambao wamepata alama kati ya 50 mpaka 59 na litaitwa B na lingine litakuwa la wale ambao wamevuka uwigo wa 50 hadi 59 na kuelekea uwigo wa 60 hadi 74 na hili litaitwa B+ (angalia jedwali hapo chini).

(ii)        Pamoja na kuwa na muachano wa alama 26 kama jedwali linavyoonesha hapo chini, alama A kwa miaka mingi imekuwa ikianzia alama 75 hadi 100 na kwamba pamoja na uwigo huo bado wanaofaulu kwa kiwango hicho ni wachache sana. Kwa mantiki hii, hakuna haja ya kubadilisha uwigo ila juhudi ziendelee katika ufundishaji na ujifunzaji ili kiwango cha ufaulu kiongezeke na kupata wanafunzi wengi zaidi wanaofaulu katika kundi hili.

(iii)       Pia, pamoja na kuwa na muachano wa alama 20 kama jedwali linavyoonesha hapo chini kwa miaka mingi, huko shuleni mwanafunzi aliyepata alama 21 na hadi 30 alihesabiwa kuwa na ufaulu wa chini kabisa au hafifu kwa kiwango cha alama D na ingawa ilikubalika ufaulu wa aina hiyo kwa mazingira ya nchi yetu unaridhisha. Alama F ilikuwa ni kwa wale waliopata chini ya hapo. Hivyo, alama F itaendelea kuwepo na itaanzia alama 0 hadi 19 na E itaanzia alama 20 hadi 29 na D – 30 -39. Lengo la muundo huu ni kuwa alama mbalimbali, isipokuwa kwa makundi machache, zianzie kwenye 0 yaani 0, 10, 20, 30, 40 na kuendelea badala ya kuanzia kwenye moja yaani 1, 11, 21, 31, 41 na kuendelea. Hii ni kwa ajili ya kuleta mtizamo unaofanana katika ngazi mbalimbali za elimu ambapo kwa sasa ngazi ambazo siyo za elimu msingi na sekondari zinatumia muundo wa kuanzia kwenye 0 badala ya 1.

c)      Uwigo wa jumla wa alama kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita utaendelea kuwa wa alama 0 hadi 100 na kila kundi katika uwigo huu limepewa tafsiri kwa ajili ya kuamua mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya mwanafunzi kulingana na malengo ya mtihani husika. Kimsingi, tafsiri zifuatazo zitakatumika

(i)         Alama A itakuwa na maana ya ufaulu uliojipambanua (distincion or outstanding performance),

(ii)        Alama B+ itakuwa na maana ya ufaulu bora sana (excellent performance),

(iii)       Alama B itakuwa na maana ya ufaulu mzuri sana ( very good perfomance),

(iv)       Alama C itakuwa na maana ya ufaulu mzuri (good performance);

(v)        Alama D itakuwa na maana ya ufaulu wa wastani (low performance),

(vi)       Alama E itakuwa na maana ya ufaulu hafifu (very low performance), na

(vii)      Alama F itakuwa na maana ya ufaulu usioridhisha (unsatisfactory performance).

Wataalamu katika maeneo mbalimbali ya elimu na ulimwengu wa kazi, kwa kushirikiana na Wizara, watatoa maana ya tafsiri hizi kiutendaji katika maeneo yao kulingana pia na mahitaji yao.

d)      Alama C iwe ndiyo alama ya ufaulu mzuri ambao hauhitaji urekebu wa lazima, wakati alama D na E ni alama za ufaulu unaohitaji urekebu kadri mwanafunzi atakavyokuwa anaendelea na masomo ili kuthibitisha kama mlengwa anaweza na kulingana na mahitaji ya eneo husika (targeted remediation). Alama F iwe alama ya eneo linalohitaji urekebu wa hali ya juu (intesive remediation) ili mwanafunzi huyo aweze kumudu masomo kadri anavyoendelea kukua kielimu ama atakapoingia katika ulimwengu wa kazi.

e)      Makundi ya alama yatajumuisha CA kwa kiwango cha asilimia isiyozidi 40 na mtihani wa mwisho kwa asilimia isiyozidi 60 kwa makundi yote ya watahiniwa ikiwemo wale wa kujitegemea (private candidates). Hii ni kwa kuzingatia kwamba CA siyo vizuri izidi uwigo wa alama ya ufaulu mzuri unapoanzia ambayo ni C au 40.

f)       CA kwa upande wa Kidato cha Nne zitokane na mtihani wa Kidato cha Pili (alama 15), matokeo ya Kidato  cha Tatu (alama 5 kwa kila muhula, na hivyo jumla ya alama 10), mtihani wa Mock (alama 10) na kazi mradi  au Projects (alama 5). Kwa upande wa Kidato cha Sita, CA iendelee kutokana na muundo unaotumika sasa.

g)      CA zitumike pia kwa watahiniwa wa kujitegemea. Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea ambao wanarudia Mitihani, CA zao  zitumike zile zilizotumika kutoa matokeo yake ya mitihani ya awali.  Kwa watahiniwa wa kujitegemea waliopitia mfumo wa Qualifying Test (QT), matokeo ya QT yatumike kama CA na mtihani wa mwisho uchangie alama 60.

h)      Kwa vile alama endelevu kwa mwaka 2013 kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne tayari zimeshawasilishwa Baraza la Mitihani  Tanzania, alama hizo zichangie asilimia 40 katika mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2013.

i)        Muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Points Average ama GPA) utaandaliwa na kuanza kutumika pale utakapokuwa tayari na wadau wataelimishwa kuhusu muundo huo ili wapate kuufahamu na manufaa yake katika elimu ya sekondari.

j)        Muundo huu mpya wa alama utatumika kwa mzunguko wa miaka minne kabla haujahuishwa tena ili kuupa muda wa kutosha kuona aina ya changamoto zinazojitokeza na jinsi ya kuzishughulikia. Aina hii ya muda itaruhusu vidato vinne vya elimu ya sekondari ya kawaida na nane ya elimu ya sekondari ya juu kupimwa. Hata hivyo, uhusihaji wa masuala ya mitihani unaweza ukafanyika iwapo matokeo ya uhuishaji wa mitaala kwa ujumla utahitaji pia eneo la mitihani liguswe na kuhuishwa pia.









Kwa mantiki hii, viwango vya alama na ufaulu ni kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 1 hapa chini:

Jedwali Na 1

MUUNDO WA ALAMA NA UFAULU

ALAMA
UWIGO WA ALAMA
IDADI YA ALAMA
TAFSIRI
A
75 - 100
26
Ufauli Uliojipambanua
B+
60 - 74
15
Ufaulu bora sana
B
50- 59
10
Ufaulu mzuri sana
C
40 - 49
10
Ufaulu mzuri
D
30 - 39
10
Ufaulu Hafifu
E
20 - 29
10
Ufaulu hafifu sana
F
0 - 19
20
Ufaulu usioridhisha



Kwa aina hii ya muundo wa alama, na kwa kuwa muundo wa GPA utaanza kuandaliwa na wadau kuelimishwa kabla haujaanza kutumika, katika kipindi hiki mpaka wakati huo, muundo wa madaraja utakuwa kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 2 hapa chini.

Jedwali Na 2

MUUNDO WA MADARAJA

MUUNDO WA ZAMANI
MUUNDO MPYA
MAELEZO
POINTI
DARAJA
POINTI
DARAJA
7-17
1
7-17
I
Kundi la ufaulu uliojipambanua na bora sana
18-21
II
18-24
II
Kundi la ufaulu mzuri sana
22-25
III
25-31
III
Kundi la ufaulu mzuri na wa wastani
26-33
IV
32-47
IV
Kundi ufaulu hafifu
34-35
0
48-49
V
Kundi la ufaulu usioridhisha



Wataalamu wa mifumo ya mitihani watalifanyia kazi zaidi jedwali hili la madaraja ili liweze kutumika kwa ufanisi katika kipindi hiki cha mpito.

Kwa mantiki hii, Daraja Sifuri linafutwa na kuwekwa daraja litakalojulikana kama Daraja la Tano na ambalo litakuwa ndilo la mwisho kabisa katika ufaulu.

HITIMISHO

Mabadiliko haya yamefanyika ili kuendelea kuimarisha mfumo wetu wa elimu na kuweka wazi taratibu mbalimbali kwa ajili ya mitihani na masuala mengine. Yako mambo mengi mengine ambayo hayana budi kuendelea kuimarishwa ikiwemo mfumo wa mitaala, walimu, mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na vitabu na vifaa vingine muhimu katika elimu. Masuala haya yanaendelea kuangaliwa kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ama Big Results Now (BRN). Ushirikiano wa wadau wote ili kuleta tija kwenye elimu ni muhimu sana na hivyo wizara itaendelea kuwashirikisha wadau wote kwa kadri itakavyohitajika na wadau pia wanaombwa wasiache kuishirikisha wizara pale watakapokuwa na jambo lolote ambalo linahitaji ushirikiano ili kwa pamoja tuweze kupata mafanikio katika sekta ya elimu.



Imetolewa,


KATIBU MKUU  
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI


Tuesday, October 29, 2013

MTOTO WA DARASA LA SITA APOOZA MIGUU MARA BAADA YA KUCHAPWA FIMBO NA MWALIMU WAKE

Mtoto Ismail
Godfrey akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar.
MWANAFUNZI wa darasa la sita, Ismail Godfrey (13)
anayesoma katika Shule ya Msingi Maendeleo Sinuka iliyopo
mkoani Kigoma amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya
kudai kutandikwa viboko na Mwalimu Muige Joseph na
kupooza miguu.
Mtoto huyo ambaye kwa sasa anapata matibabu katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar baada ya kukosa
matibabu ya kina mkoani Kigoma alipokutana na mwandishi
wetu alikuwa na haya ya kusema:
“Awali sikuwa na matatizo yoyote ya kiafya hususan katika
viungo vya mwili, isipokuwa haya yalinipata baada ya
kuchapwa fimbo na mwalimu wangu ndipo nikapooza ghafla.



KING'AMUZI CHA AZAM

Hiki ndio king'amuzi cha Azam ambacho kwa shilingi elfu 95 za kitanzania utakipata pamoja na dishi lake na huduma ya kufungiwa nyumbani kwako.
 Ukifungiwa king'amuzi hiki utapata chaneli 35 bure na ukilipia 12, 500 utapata chaneli zaidi ya 50.
 Azam Tv itaanza kurusha matangazo yake katikati ya mwezi wa novemba.








Monday, October 28, 2013

MSIMAMO WA LIGI KUU TANZANIA BARA BAADA YA MECHI ZA LEO




KIBONZO: WATAFITI NA TANZANIA YETU




HIZI NDIO CHANELI ZINAZO PATIKANA KWENYE KING`AMUZI CHA AZAM MEDIA

Leo katika ukurasa wa Facebook wa Azam TV wameweka idadi na majina ya chaneli zinazopatikana kwenye king`amuzi chao. Chaneli zilizo orodheshwa zipo 45 ikiwa ni kinyume na tangazo lao linalo onesha zitakuwa chaneli kuanzia hamsini. Vilevile bado hawajaeleza kinaanza kupatikana lini na wapi na gharama zake za uwekaji na kwa mwezi. Ila katika maelezo hayo wameainisha chaneli za kulipia na za bure
Chaneli walizo weka ni hizo hapo chini:


FILAMU:
 

1.Sinema Zetu  2.MGM Movies  3.African Movie Channel  4.Zee Cinema  5.Star Gold

BURUDANI:
 

1.Azam 1  2.Azam 2  3.Fox Entertainment  4.FX  5.e.tv  6.ZOOM  7.Star Plus  8.Zing  9.Colours  10.Euro Channel

MICHEZO:

 

1.Setanta Africa  2.Kombat Sports  3.MCS Compact  4.MCS Extreme

MUZIKI:
 

1.MTV BASE  2.MTV India  3.Box TV

MAARIFA:
 

1.Nat Geo  2.Discovery Investigation  3.Discovery Science

MAISHA:
 

1.Fine Living  2.Outdoor  3.Landscape

HABARI:
 

1.BBC News  2.Al-Jazeera - English  3.Al-Jazeera - Arabic  4.ENCA  5.Times Now

WATOTO:
 

1.Kids Co  2.Nickelodeon  3.Al-Jazeera - Kids

CHANELI ZA BURE:
 

1.TBC  2.Clouds TV  3.ZBC  4.Channel 10  5.Mlimani TV  6.KBC  7.Citizen  8.K24  9.KTN
Tangazo la Azam Tv linalo onesha kuwa kutakuwa na Chaneli kuanzia hamsini

Picha ya maelezo ya facebook ya ukurasa wa Azam TV


PICHA: AJALI MBAYA KWENYE MPAKA WA SONGWE NA MBOZI: WATANO WAPOTEZA MAISHA


Basi la abiria aina ya coaster lenye namba za usajili  T378ADR likiobnekana muda mchache baada ya kupata ajali.
 Basi la abiria aina ya coaster lenye namba za usajili  T378ADR  likiwa limeharibika vibaya mara baada ya kupata ajali hiyo
Kiatu cha Abiria kikiwa kimebaki baada ya ajali hiyo 
 Wakazi mbalimbali wa mpakani mwa Mbozi na Songwe wakishuhudia Ajali hiyo 
 Hapa Basi la abiria aina ya coaster lenye namba za usajili  T378ADR baada ya kupata ajali 
 Baadhi ya watu wakiangalia kama kutakuwa na watu wamebakia katika ajali hiyo 
 Usukani wa Dereva ukiwa umetoka mara baada ya ajali hiyo 
 Basi la abiria aina ya coaster lenye namba za usajili  T378ADR  linavyo onekana kwa mbele 
 Hivi ndivyo Basi la abiria aina ya coaster lenye namba za usajili  T378ADR lilivyo haribika 
 Wananchi Mbalimbali wakiwa wanashuhudia ajali hiyo na kutoa msaada 
 Mmoja ya Majeruhi baada ya kufikishwa hospitali

CHANZO: MBEYA YETU BLOG

BABA AWACHOMA WATOTO MOTO BAADA YA KUZIDIWA NGUVU NA MAMA YAO



 Mtoto aliyefariki
Mtoto Matrida Michael mwenye umri wa miaka 9, mkazi wa Mtoni kwa Azizi Ally, wilayani Temeke jijini  Dar es Salaam, amefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Oktoba 23, mwaka huu kufuatia majeraha ya moto aliyoyapata. 

Marehemu Matrida na watoto wenzake wawili, Tatu Mapunda (9) na Flora Mapunda (7), waliungua moto Oktoba 16, mwaka huu saa tano usiku wakiwa wamelala baada ya chumba chao kulipuliwa kwa petroli na mtu anayedaiwa kwa ni Brighton Mnamwa.

Inadaiwa kwamba chanzo cha Mnamwa kuamua kulipua watoto hao ni ugomvi baina yake na mkewe Janeth Lwena, waliyekuwa katika mzozo wa kumgombea mtoto wao wa miaka mitatu aitwaye Tulizo.

Watoto ambao wako hoi

Mama mdogo wa marehemu Mary Ivo ambaye alikuwepo msibani hapo, alisema kwamba dada yake yupo Muhimbili anawauguza majeruhi wawili waliobakia na kwamba wakati wa ugomvi wao, mke alimzidia nguvu mumewe.
Aidha aliendelea kueleza kwamba baada ya mke kumzidi nguvu, mume alizusha ugomvi mkubwa huku akitishia kumuua kwa panga, hata hivyo mke alimdhibiti.

‘Baadaye mume huyo inadaiwa kwa aliondoka hapo nyumbani na haikujulikana alikoenda, ndipo mke alienda chumba cha jirani na kumuomba Matrida abakie na watoto pale chumbani akatoe taarifa polisi lakini mtoto aliyekua akigombewa alienda naye kituoni,’ alisema mama mdogo.

Habari zinasema kwamba yule mume alienda kituo cha mafuta kununua petroli ili aweze kuwatekezeza wote, lakini hakujua kama mkewe pamoja na mtoto aliyekua akigombewa hawakuwepo.

Taarifa zaidi zinaeleza kwamba baada ya mume huyo kurudi, alimimina mafuta hayo katika chumba hicho kisha kukilipua wakati watoto hao watatu wakiwa katika usingizi na wananchi walipojitokeza walikuta chumba kikiteketea huku sauti ya watoto ikisikika wakiomba msaada.

Wananchi waliokuwepo kwenye eneo la tukio walisema kwamba walipatwa na uchungu hivyo walijitosa kuuzima moto ule na kuwaokoa watoto hao watatu huku wakiwa wameungua vibaya, waliwakimbiza Hospitali ya Temeke na kutokana na hali yao kuwa mbaya walipelekwa Muhimbili ambapo Matrida alifariki dunia.

Naye Michael Melkiori Kess, baba wa marehemu alisema kwamba amesikitishwa na kitendo hicho na amedai ni cha kinyama hivyo ameiomba dola kumsaka mtu huyo hatari kwani huko aliko kwa sasa bado anaweza kusababisha majanga megine.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mtoni Sabasaba, Mwita Mang’ana alisema kwa kitendo hicho ni cha kinyama kwani amesababisha kujeruhi watoto wasiokua na hatia na amewataka wananchi kushirikiana na jeshi la polisi kuhakikisha kuwa mtuhumiwa anapatikana .

Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba msako wa kumtafuta mtuhumiwa unaendelea sambamba na uchunguzi wa tukio.


NI JAMAL MALINZI




Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kagera, Jamal Malinzi amechaguliwa kuwa Rais Mpya wa shirikisho la soka nchini, TFF. 

Malinzi ameshinda uchaguzi huo wa leo uliokuwa ukifanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa NSSF, Water Front jijini Dar es Salaam kwa kupata asilimia 78 ya kura na kumbwaga mpinzani wake Athuman Nyamlani. 

Malinzi atachukua nafasi ya Leodegar Tenga aliyekuwa Rais wa TFF tangu mwaka 2005. Taarifa za kuchaguliwa kwa Malinzi kuwa rais mpya wa TFF, zimepokelewa kwa furaha na binti yake, mtangazaji wa Clouds FM, Loveness aka Diva aliyetweet: 

My dad is the new president TFF¦.. What a good news. Cant wait to get home and give him a big hug and a kiss. Gooooo Daddy” Diva (@DivaBos) October 27, 2013

Malinzi alishika nyadhifa mbalimbali Yanga zikiwemo seneta, mkurugenzi wa kuchaguliwa, kaimu katibu mtendaji na katibu mkuu. 

Amekuwa mwenyekiti wa mashindano ya mpira wa miguu mkoa wa Pwani (2009-2011) na mjumbe wa Baraza la Michezo la Mkoa wa Dar es Salaam (2009-2012). 

Toka 2011 hadi sasa ni mjumbe kwenye Kamati ya Utendaji ya Chama cha Mpira wa Miguu wilaya ya Misenyi, pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Kagera.


HOTUBA YA KWANZA YA JAMAL MALINZI BAADA YA KUSHINDA UCHAGUZI

 Hatimaye Tumechagua Mabadiliko,
 
Salamu kwa wanafamilia wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Salamu kwa wapenda michezo wa ndani na nje ya nchi yetu Tanzania.

Naanza kwa kumshukuru Mungu kwa hekima, busara, akili, vipaji na uwezo aliotujaalia kutuwezesha kutenda yote haya kwa amani na utulivu.

Shukrani za dhati zimwendee Bw. Leodegar Tenga, rais wa TFF 2005 - 2013 anayekabidhi madaraka kwa rais mpya wa TFF. Yeye na timu yake kwa hakika wanastahili pongezi kwa mengi mazuri waliyofanya.

Shukrani kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi 2013 kwa kunikubali, mimi Jamal E. Malinzi niwe Rais wa TFF kwa kipindi kijacho cha miaka minne.

Kweli dunia imekuwa kijiji, kwani kipindi cha masaa 72 baada ya kuzindua ilani yangu ya uchaguzi, nimepokea salamu, maoni na mapendekezo toka ndani na nje ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Burundi, Ivory Coast, Denmark na NewZealand.

Kupitia www.jamalmalinzi.com, twitter @jamalmalinzi, Jamii Forum, Facebook na mitandao mingine, naomba tuendelee kuwasiliana, kutoa maoni, kukosoa na kuchangia mijadala yenye tija na ufanisi ili Tanzania yote ipate neema ya mpira wa miguu.

Safari ni ndefu na wasafiri ni wengi kwenye vyombo vichache vya usafiri. Kwa wale ambao tayari wana ramani ya safari yetu, sote bila kujali tofauti zetu hasa wakati wa kuwania uongozi, tutoe mchango wake ili Tanzania isonge mbele katika ulimwengu wa soka.

Naam, kuna msemo wa Kiswahili unaosema 'kukata tamaa ukingali unaishi ni dhambi'. Naomba msemo huu na utuongoze kila tunapojikwaa tunanyuke na kuendelea na safari hadi tufike tulipopakusudia.

Historia imeshaanza kuandikwa, mwaka 2013 ni Tumechagua Malinzi, Tumechagua Mabadiliko na sasa tunasonga mbele.
 
Jamal E. Malinzi
Oktoba 27, 2013


 

USISAHAU KU LIKE PAGE YETU