HATIMA ya
kesi ya ugaidi inayowakabili makada watano wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), sasa ipo mikononi mwa Mahakama Kuu baada ya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora ilikofunguliwa kusema haina uwezo wa
kusikiliza kesi ya ugaidi.
Wakati
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Tabora, Issa Magoli, akiisukumia Mahakama
Kuu kesi hiyo, wakili wa watuhumiwa hao, Peter Kibatala, aliliambia
Tanzania Daima kuwa wameshafanya utaratibu wa kupeleka shauri lao
Mahakama Kuu baada ya kupewa nakala ya uamuzi huo.
Makada
hao wa CHADEMA wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi ni Katibu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Henry Kilewo, Evodius Justinian, Oscar Kaijage , Seif Kabuta
na Rajab Daniel, wanaotuhumiwa kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa
Tesha, katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga mwaka 2011.
Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Magoli alisema mahakama hiyo haina uwezo kisheria kusikiliza kesi hiyo,
hivyo akaiahirisha kesi hiyo hadi Julai 22, mwaka huu.
Hakimu
Magoli kabla ya kuahirisha shauri hilo aliwashauri mawakili wa upande
wa utetezi wawasilishe hoja zao Mahakama Kuu ya Tanzania ambapo
watapatiwa ufumbuzi wa kisheria.
Akizungumza kwa simu na gazeti
hili, wakili wa washtakiwa hao, Peter Kibatala, saa chache baada ya
uamuzi huo, alisema wameshapeleka Mahakama Kuu Kanda ya Tabora maombi
kwa hati ya dharura ya kutaka iipitie upya kesi hiyo ya ugaidi.
Aliongeza
kuwa maombi hayo yamepokewa katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na
wanasubiri kupangiwa tarehe nyingine na Mahakama Kuu ili kesi hiyo
isikilizwe.
Alisema katika maombi yao wameomba Mahakama Kuu
ipitie shauri hilo, pia kuona kama ni halali kisheria kwa washtakiwa hao
kufunguliwa kesi hiyo baada ya awali watuhumiwa wanne (isipokuwa
Kilewo), mashtaka yao yaliondolewa na kisha kukamatwa na kufunguliwa
mashitaka mapya.
Kwa mara ya kwanza watuhumiwa hao walisomewa
shitaka la ugaidi Juni 24, mwaka huu, wakidaiwa walimteka na kummwagia
tindikali kada wa CCM, Musa Tesha, katika kampeni za uchaguzi mdogo wa
Igunga uliofanyika mwaka 2011.
Awali kabla ya kusomewa shitaka la
ugaidi ambalo kwa sasa mahakama inasema haina uwezo wa kusikiliza,
mwanzoni walifunguliwa shitaka la kushambulia na kudhuru mwili, ambapo
Mahakama ya Wilaya ya Igunga iliwaona hawana hatia, hivyo kuwaachia huru
lakini walikamatwa tena.
Kesi hiyo ilisikilizwa mbele ya Hakimu
wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora mjini. Jocktan Rushwera, ndiye
aliyesikiliza hoja za mawakili wa utetezi, waliomtaka kuifuta kesi hiyo.
Hata hivyo haijulikani kwanini kesi ilisikilizwa halafu baada ya
kubadilisha hakimu, kwa kesi hiyo hiyo mwingine akasema mahakama hiyo
haina uwezo wa kuisikiliza.
Upande wa serikali uliwakilishwa na Wakili Juma Massanja na Ildefons Mukandara.
Awali
watuhumiwa hao waliposomewa shitaka, jopo la mawakili wa utetezi,
Abdalah Safari na Peter Kibatala, liliomba mahakama hiyo iyafute
mashitaka hayo kwa sababu ya kutokuwa na uhai.
Mawakili hao wa
utetezi walidai kuwa mashitaka hayo hayana uhai kwa sababu yamefunguliwa
bila ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Pia
mawakili hao walidai kuwa sheria za uendeshaji wa makosa kama hayo hapa
nchini zinadai kuwa mashitaka kama hayo yanapofunguliwa ni lazima ridhaa
ya DPP iwepo, lakini ridhaa hiyo haipo, hivyo yatupwe.
Waliongeza
sababu ya pili kuwa maelezo hayaoneshi kosa husika ni la kigaidi,
tofauti na makosa mengine ya kawaida kwa mujibu wa sheria za Tanzania,
hivyo waliomba yafutwe au yafunguliwe kama kosa la kawaida.
Upande
huo wa utetezi pia ulidai kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai,
inaelekeza kuwa mshitakiwa ashitakiwe katika mahakama yenye mamlaka na
hadhi kama ile waliyopelekwa katika maeneo yale walikokamatwa.
Hivyo
mawakili waliiomba mahakama itupilie mbali shitaka, kwani washitakiwa
kama walikuwa na hatia walipaswa kushitakiwa katika maeneo yao
walipokamatwa.
Upelelezi wa Lwakatare badoWakati
huo huo, mkoani Dar es Salaam, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,
imeahirisha kesi ya kula njama na kutaka kumuua kwa sumu Mhariri
Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Denis Msacky, inayomkabili Mkurugenzi
wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA),Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.
Hakimu Mkazi, Alocye, aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 22, mwaka huu kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.
Awali, Wakili Mkuu wa Serikali, Ponsia Lukosi, aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Lwakatare
yupo nje kwa dhamana, Ludovick bado yupo gerezani baada ya kushindwa
kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni mshitakiwa kuwa na wadhamini
wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika kisheria ambapo kila mdhamini
atatakiwa asaini bondi ya sh milioni 10 pamoja na washitakiwa wenyewe.
Pia
mshitakiwa anatakiwa kusalimisha hati yake ya kusafiria mahakamani na
kutotoka nje ya Jiji la Dar es Salaam bila ya kibali cha mahakama.
Taarifa hii imeandaliwa na Happiness Katabazi (Dar), Thomas Murugwa na Josephat Isango (Tabora).
---
Picha via
JamiiForums.comMaandishi via
TanzaniaDaima